Mwanafunzi bora nafasi ya tatu kitaifa katika masomo ya biashara wa shule ya Tusiime, Rashid Abdalah aliyevaa flana, akifurahia na kupongezwa na wanafunzi wa kidato cha tano wa shule hiyo alipokwenda kuwatembelea na kuwadokeza siri ya magfanikio yake.
MWANAFUNZI wa shule ya Sekondari ya Tusiime, Rashid Abdalah, aliyeshika nafasi ya tatu kitaifa kwa masomo ya biashara amesema nia yake ni kusoma hadi ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD).
Akizungumza leo shuleni hapo Rashid amesema ndoto yake ya miaka mingi ni kuwa mkaguzi wa hesabu hivyo amenuia kusoma kwa bidii hadi afikie ngazi hiyo.
“Naamini nitafikia malengo yangu kwa kuwa najua siri ya kufika huko ni juhudi, kujitambua na kuwasikiliza walimu, hakuna kingine zaidi ya kuwa makini na masomo na kuwa makini,” alisema Rashid ambaye alianzia kidato cha pili shuleni hapo mwaka 2012.
Amesema juhudi za walimu katika kufuatilia maendeleo ya wanafunzi na mazingira mazuri ya shule, ushirikiano mzuri na wanafunzi wenzake ni baadhi ya mambo ambayo yamekuwa chachu ya mafanikio yake.
Aidha amewaasa wanafunzi waliobaki shuleni hapo kujitambua wamefuata nini shuleni na kufuatilia kila wanachofundishwa na walimu wao ili mwisho wa siku wapate mafanikio kama yake.
“Kufaulu haiwezi kuwa muujiza ni juhudi tu na kusikiliza mafundisho na maelekezo ya walimu, lazima mtambue kuwa walimu wanataka mfaulu hivyo mkiwasikiliza na kuwafuata mtafaulu kwa viwango vya juu sana,” amesema Rashid alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa kidato cha tano shuleni hapo.
Mkuu wa shule hiyo, Emil Rugambwa, amesema mafanikio ya shule hiyo kwenye matokeo ya kidato cha sita ni mwendelezo wa mafanikio kwenye matokeo ya kitaifa ambayo shule imekuwa ikiyapata kuanzia yale ya darasa la nne, darasa la saba, kidato cha pili na cha nne.
Kwenye matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, Tusiime imefanikiwa kufanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) hivi karibuni kwa kufaulisha wanafunzi wote 518.
No comments:
Post a Comment