HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

MAHAKAMA YA JUU NCHINI KENYA YAFUTA MATOKEO YA UCHAGUZI ULIOMPA USHINDI UHURU KENYATTA

Mahakama ya Juu nchini Kenya imefuta matokeo ya urais yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta kuwa madarakani kwa muhula wa pili.

Mgombea wa Muungano wa Nasa, Raila Odinga alifungua kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Agosti 8, akisema ulitawaliwa na udanganyifu ikiwemo kuchezewa mitambo ya kujumlishia matokeo.

Katika uamuzi wake, Mahakama imesema uchaguzi huo ulikuwa na dosari nyingi, hivyo kukiuka misingi ya uchaguzi huru na wa haki kama ilivyoelekezwa katika Katiba ya nchi hiyo.
 Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Taifa hilo kwa Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya uchaguzi na inaweka rekodi mpya katika historia ya uchaguzi barani Afrika ndani ya mfumo wa vyama vingi.

Katika uchaguzi uliopita, Odinga alienda mahakamani kupinga matokeo lakini Mahakama hiyo ilitupilia mbali hoja zake na kuridhia matokeo yaliyompa ushindi Rais Kenyatta.
Katika uchaguzi wa Agosti 8, Kenyatta alitangazwa mshindi kwa kupata kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27, huku mpinzani wake Odinga akipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74.

Kwa uamuzi uliotolewa na mahakama, uchaguzi mwingine unapaswa kufanyika katika kipindi cha siku 60. Iwapo ushindi wa Kenyatta ungeidhinishwa angepaswa kuapishwa Septemba 12.

Kumekuwa na shamrashamra katika mitaa mbalimbali ya Nairobi na Mombasa kushangilia uamuzi huo, huku Odinga akiwa na wanasiasa wenzake wamepongeza wakisema watatoa taarifa zaidi baadaye.

MAHAKAMA YASEMA YUSUF MANJI ANAKESI YA KUJIBU SAKATA LA MADAWA YA KULEVYA

Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu leo August 25, 2017 imesema Mfanyabiashara Yusuf Manji ana kesi ya kujibu katika kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkeha, wakati kesi hiyo ilipoitishwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi.

Hakimu Mkeha alisema kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka na kwamba mshtakiwa ana haki ya kujitetea kutokana na mkojo wake kukutwa na dawa aina ya Morphine ambayo zao lake ni Heroin.

“Hivyo mshtakiwa anapaswa kujitetea kwa sababu Mahakama imemkuta na hatia,”

Baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi Hudson Ndusyepo alidai kuwa mshtakiwa atajitete kwa hati ya kiapo ambapo watakuwa na mashaidi 15.

Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi August 30 Na 31, 2017 ambapo itasikikizwa mfululizo.

Mahakama Yaelezwa Jinsi MKOJO Wa Yusuf Manji Ulivyochukuliwa na Kupimwa

Mashahidi wawili akiwemo Naibu Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ofisa wa Polisi, Ramadhan Kingai leo  wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi Mfanyabiashara Yusuf Manji alivyopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kupimwa mkojo.

Mbali ya Kingai ambaye ni Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo ya dawa za kulevya inayomkabili Manji, Shahidi mwingine ni E.1125 Copro Detective Sospter.

Mashahidi hao walitoa ushahidi wao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha baada ya Wakili Mkuu wa Serikali, Timony Vitalis kueleza kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya ushahidi.

Akiongozwa na Wakili Vitalisi, Shahidi Kingai amedai kuwa February 9, 2017 akiwa Ofisini kwake Central alikuwa na kazi mbalimbali ikiwemo ya kuripotiwa kwa watuhumiwa wa Dawa za kulevya waliotajwa na RC Makonda.

Amedai katika watuhumiwa hao alimpokea Yusuf Manji na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima baada ya kuripoti wenyewe kituoni hapo.

“Baada ya kufika nikiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Uchunguzi wa dawa za kulevya nilielekeza Manji na Gwajima wapelekwe kwa Mkemia Mkuu kupimwa, kwa sababu tuhuma zao ni za dawa za kulevya, ambapo pia walienda kupekuliwa nyumbani mwao”

Shahidi huyo akadai kuwa amri ya kupimwa ilitekelezwa na Detective Copro Sospeter, ambapo baada ya kufanyika uchunguzi akapewa taarifa kwamba Manji anatumia Dawa za kulevya aina ya Benzodiazepines na Gwajima hatumii.

“Nikiwa kama Mpelelezi Mkuu niliichukua ripoti hiyo kisha nilielekeza Manji afunguliwe jalada la kutumia dawa za kulevya ambapo baada ya kufunguliwa lilipelekwa kwa DPP”.

Baada ya kueleza hayo, Wakili wa Manji, Hudson Ndusyepo alimuuliza shahidi huyo kwa nini dawa za kulevya (Benzodiazepines) alizozitaja Mkemia Mkuu ni tofauti na zilizotajwa kwenye hati ya Mashtaka (Heroin) ambapo shahidi huyo alijibu hajui na yeye hakuandaa hati ya mashtaka.

Shahidi wa pili, Detective Copro Sospeter akiongozwa na Wakili Vitalis alidai kuwa February 9, 2017 saa 5 asubuhi alikuwa Ofisini na alimpeleka Manji kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuchubguzwa.

Alidai kuwa maelezo ya kumpeleka Manji kwa Mkemja aliyapata kwa Kingai, ambapo alimpeleka kwa tuhuma za kutumia dawa za kulevya.

” Nilimchukua Manji na kumpeleka msalani ili ichukuliwe sampo ya mkojo wake ufanyiwe uchunguzi, ambapo kuna kielelezo cha fomu kuhusu suala hilo na naomba kipokelewe na Mahakama.”

Alieleza kuwa baada ya mtuhumiwa kuchunguzwa alichukua majibu kisha alirejeshwa Polisi na taratibu kufatwa.

Baada ya kuelezwa hayo, Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hadi August 23, 2017.

DPP aamua kuachana na mbunge Lwakatare kuhusu ugaidi

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ameaondoa maombi yake dhidi ya Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare kuhusiana na shtaka la ugaidi dhidi yake.
DPP alikuwa amefungua maombi Mahakama ya Rufani akiomba kibali cha kufungua maombi ya mapitio kuhusiana na uamuzi wa Mahakama Kuu kumfutia Lwakatare mashtaka ya ugaidi.
Maombi hayo ya DPP yalitarajiwa kusikilizwa leo Ijumaa, Agosti 11 na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mussa Kipenka, lakini DPP akaamua kuyaondoa kabla ya usikilizwaji.
Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka ameieleza mahakama kuwa DPP hana nia ya kuendelea na maombi hayo.
Kutokana na nia hiyo ya DPP, wakili wa mjibu maombi, Richard Rweyongeza amesema kuwa hana pingamizi dhidi ya nia ya DPP kuyaondoa maombi hayo na Jaji Kipenka akatoa amri ya kuyaondoa mahakamani maombi hayo.
Kwa uamuzi huo sasa Lwakatare anabaki na shtaka la kula njama ili kutenda kosa, katika kesi ya msingi inayosikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Awali, Lwakatare na mwenzake walikuwa Ludovick Rwezaura walikuwa wakikabiliwa na jumla ya mashtaka manne likiwemo la kula njama za kufanya vitendo vya kigaidi kwa lengo la kumdhuru kwa sumu aliyekuwa Mhariri wa gazeti la Mwananchi, Denis Msacky.
Mashtaka mengine yalikuwa ni ya ugaidi, wakidaiwa kuandaa mikutano ya kupanga makosa ya kigaidi na kufadhili vitendo vya kigaidi.
Hata hivyo, Lwakatare kupitia kwa mawakili wake walifungua maombi Mahakama Kuu wakipinga mashtaka hayo yaliyokuwa yakiangukia katika Sheria ya Ugaidi.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Lawrence Kaduri ilikubaliana nayo na akamfutia Lwakatare mashtaka hayo ya ugaidi na hivyo kubakiwa na shtaka moja tu la kula njama ambalo haliangukii katika sheria hiyo ya ugaidi.
DPP hakukubaliana na uamuzi huo wa Mahakama Kuu, ndipo akafungua maombi ya kibali kufungua maombi nje ya muda, ili kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kumfutia mashtaka hayo ya ugaidi.

Chanzo:  Mwananchi

Serikali kuja na mashahidi 10 kesi ya dawa za kulevya inayomkabili Manji

Serikali imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwamba itafika na mashahidi wasiozidi 10 katika kesi ya kutumia na kujihusisha na dawa za kulevya inayomkabili mfanyabiashara, Yussuf Manji.
Hayo yameelezwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Timony Vitalis mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha baada ya kumsomea Manji maelezo ya awali (Ph) ambapo katika maelezo hayo, Vitalis amedai mshtakiwa ni mkazi wa Sea view DSM, pia ni mfanyabiashara anayetuhumiwa kujihusisha na kutumia dawa za kulevya.
Amedai kuwa alikamatwa February 2, 2017 kisha akapelekwa kituo cha Polisi ambapo alichukuliwa hadi nyumbani kwake na kupekuliwa na baada ya kupekuliwa alipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kuchukuliwa haja ndogo (Mkojo) ambao ulipimwa na kukutwa na dawa za kulevya aina ya Benzodiazepine.
Baada ya kusomewa maelezo hayo, Manji alikubali wasifu wake kwamba ni mfanyabiashara, makazi na jina lake licha ya kudai limekosewa ila usahihi ni Yusuf Manji huku akikana maelezo mengine.
Aidha, wakili Vitalis ameieleza Mahakama kwamba wanaomba kupangiwa tarehe kwa ajili ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa, pia wanatarajia kuwa na mashahidi wasiozidi 10 hivyo Hakimu Mkeha ameahirisha kesi hiyo hadi August 22, 23, na 24, 2017 kwa ajili ya kusililizwa mfululizo.

Bilionea IPTL kutibiwa Amana au Lugalo

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru mshtakiwa Harbinder Singh Sethi anayeumwa atibiwe hapahapa nchini.
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amesema hajawahi kusema atibiwe nje ya nchi, bali atibiwe nchini na kwamba ndani ya siku 14 wanasubiri matokeo kama amefikishwa hospitali kutibiwa ama la.
Amesema hay oleo Alhamisi, Agosti 3 baada ya Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kuomba atibiwe katika Hospitali ya Amana au Lugalo.
Akiwasilisha hoja hiyo leo kwa Hakimu Shaidi, Swai amekiri kuwepo kwa amri ya Mahakama ya mshtakiwa kupatiwa matibabu.
Hata hivyo, amedai hawana ushahidi kuwa siku mshtakiwa alipokamatwa alikuwa anakwenda Afrika Kusini kutibiwa.
Pia, amedai suala la mshtakiwa kupelekwa nje ya nchi kutibiwa si sahihi kwa sababu utaratibu wa mgonjwa kupelekwa nje unafahamika na kwamba haendi kwa sababu ya amri ya Mahakama.
Swai amepinga Sethi kutibiwa nje kwa kuwa madaktari wa hapa nchini hawajakiri kushindwa na hakuna uthibitisho wa madaktari kwamba wameshindwa kumtibu.
Pia, amedai hakuna utaratibu wa mgonjwa kupelekwa Muhimbili moja kwa moja anatakiwa kuanzia Hospitali ya Amana ama Lugalo wao ndiyo watafanya utaratibu wa kumuhamishia Hospitali ya Muhimbili.
Amedai Magereza ambapo Sethi anatibiwa ndiyo wametakiwa kuthibitisha na kufanya utaratibu apeleke Hospitali ya Amana.
Amebainisha kuwa Amana nao hawajasema wameshindwa kumtibu hivyo ameomba aendelee kutibiwa katika Hospitali ya Amana.
Kuhusu ombi la Wakili wa Sethi, Alex Balomi kuomba kesi itajwe ndani ya siku saba kwa ajili ya kuangalia kama amepelekwa hospitali.
Swai aliyeomba siku 14 alidai kutajwa ndani ya siku saba ni kumsumbua mgonjwa na kwamba muda huo autumie kwenda hospitali na siyo mahakamani.
Amebainisha kuwa ndani ya siku 14, atakuwa amefikishwa katika Hospitali ya Amana ama Lugalo kupatiwa matibabu kwa kuwa taratibu za Magereza zimekamilika na wao watasimamia.
Lakini Balomi amedai hadi sasa mteja wake hajapelekwa hospitali na akaomba mahakama isimamie amri yake ya mshtakiwa kupatiwa matibabu.
Hakimu Shaidi katika uamuzi wake amewapa siku 14 Takukuru kama walivyoomba awali, ili kuangalia kama atakuwa amefikishwa katika Hospitali ya Amana ama Lugalo kupatiwa matibabu.

Kesi imeahirishwa hadi Agosti17, 2017.
Awali, Julai 14, 2017, Wakili wa kujitegemea wa Sethi, Alexi Balomi aliifahamisha mahakama kuwa Sethi anaumwa na kwamba hali yake ilikuwa ikiendelea kubadilika kuwa mbaya na alikuwa hawezi kupata usingizi kwa wiki nne.
Wakili Balomi aliiambia mahakama hiyo kuwa Seth anasumbuliwa na uvumbe tumboni kama puto ambao unahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari.
Katika kesi hiyo, Sethi na James Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kighushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha hasara ya Doa za Marekani 22, milioni na Sh309 bilioni.

Maombi ya wabunge waliofukuzwa CUF yasikilizwa

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam hivi sasa inaendelea na usikilizwaji wa maombi ya wabunge waliofukuzwa na Chama cha Wananchi (CUF), ya kutaka kusimamishwa kuapishwa kwa wabunge wapya walioteuliwa juzi kuziba nafasi zao.
Hata hivyo, badala ya kusikiliza maombi ya msingi, mahakama inasikiliza mapingamizj ya awali yaliyowasilishwa na jopo la Mawakili wa Serikali kwa niaba ya wajibu maombi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na Katibu wa Bunge pamoja na pingamizi lililowasilishwa na Bodi ya Wadhamini CUF, na wabunge wateule.
Waombaji katika maombi haya wanawakilishwa na mawakili wawili, Peter Kibatala na Omari Msemo, wakati NEC na Bunge wanawakilishwa na jopo la mawakili nane wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata, wakati Bodi ya Cuf na wabunge wateule wanawakilishwa na Wakili Mashaka Ngole.
Baada ya kumaliza hoja zao za pingamizi, Kibatala na Msemo watajibu hoja hizo na baadaye Jaji Lugano Mwandambo atatoa uamuzi ama leo hii au siku nyingine atakayopanga.

Mkemia: Mkojo wa Masogange umebainika kuwa na heroin

Mkemia kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Elias Mulima, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa sampuli ya mkojo wa msanii Agnes Gerald maarufu kama Deal ama Masogange (28) umebainika kuwa na dawa ya kulevya aina ya heroin.
Akitoa ushahidi leo Jumatano mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, shahidi huyo wa kwanza wa upande wa mashtaka, akiongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula, ameiambia mahakama kuwa mnamo February 15, 2017 askari wawili kutoka Jeshi la Polisi Tanzania, Koplo Sospeter na WP Judith, walimfikisha Masogange ofisini kwake kwa lengo la kumfanyia vipimo vya mjono wake.
Alisema baada ya kuwapokea, alimsajili Masogange na kumpa namba ya mahabara 446 /2017 na kisha kuwakabidhi kifaa maalum kwa ajili ya kuweka sampuli ya mkojo.
Alidai baada ya kupokea sampuli ya mkojo ya Masogange alifanyia uchunguzi kwa kutumia kemikali na kubaini kuwa mkojo wake una chembechembe za dawa za kulevya aina ya heroin ambazo kwa kitaalamu zinajulikana kama Diacety Imophine.
Aidha, alisema uchunguzi zaidi ulibaini chembechembe za dawa nyingine ya kulevya aina ya Oxazepam.
Shahidi huyo alidai baada ya kufanya uchunguzi huo, aliandaa taarifa ya uchunguzi kuhusiana na sampuli hiyo ya mkojo ambapo aliisaini yeye mwenyewe na kuthibitishwa na kaimu mkemia mkuu wa serikali.
Shahidi huyo alimtambua Masogange kwa ndiye aliyepelekwa kuchukuliwa sampuli hiyo ya mkojo ofisini kwake.
Pia alidai anaweza kuitambua taarifa hiyo ya uchunguzi kutokana na kuwepo kwa saini yake, muhuri wa moto wa maabara ya mkemia mkuu wa serikali. Pia ameomba mahakama kupokea vitu hivyo kama kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo.
Hata hivyo, mawakili Nehemiah Nkoko na Reuben Simwanza ambao wanamtetea Masogange wamepinga taarifa hiyo ya uchunguzi wakitaka isipokelewe na mahakama kwa madai haijakidhi vigezo vya sheria.
Nkoko amedai utaratibu wa kisheria haukufatwa kabla ya mtuhumiwa aliyeko chini ya polisi kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu, kwa kuwa ofisa wa polisi alitakiwa kuwasilisha maombi mahakamani ndipo amri ya kupimwa itolewe.
Amesema katika ushahidi wake mkemia huyo hajaeleza kama ofisa wa polisi alipeleka amri ya mahakama kutoka mahakama yoyote ile.
"Ripoti ipo kinyume na sheria, mahakama ina njia moja tu nayo ni kuikataa na sio kuikubali. Sheria ipo wazi, tunaomba mahakama ikubali pingamizi letu na kukataa kupokea taarifa hiyo," alisema.
Naye Wakili Simwanza alidai ripoti hiyo ikitazamwa inataja fomu nyingine ya ombi la Jeshi la Polisi kwenda kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya kufanya vipimo.
Amedai ripoti hiyo ipo yenyewe bila ya kuambatanishwa na fomu maalum inayotumiwa na polisi kupeleka sampuli hivyo haiwezi kupokelewa na kutumika kama kielelezo.
Akijibu hoja hizo, Wakili Kakula alidai mapingamizi hayo hayana mashiko wala miguu ya kusimamia.
Amedai fomu ambayo haijaambatanishwa na ile ya mkemia mkuu ni vitu viwili tofauti na hata uwasilishwaji wake unafanywa na watu wawili tofauti.
Alisema taarifa ya mkemia inawasilishwa na mkemia na ile ya polisi inawasilishwa na polisi.
Kuhusu hoja ya sampuli ya mkojo, Kakula alidai kifungu cha 63 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kimeweka mazingira ambayo ofisa wa polisi atawasilisha maombi mahakamani kuweza kuchukua sampuli.
Alisema iwapo mtuhumiwa anakataa kuchukuliwa sampuli ya mkojo, hivyo atawasilisha ombi mahakamani ili iweze kutolewa amri.
Kakula alisema katika pingamizi lao upande wa utetezi haijaeleza kwamba mshitakiwa alikataa kupima, akalazimishwa. Aliomba mapingamizi hayo yatupiliwe mbali.
Hakimu Mashauri ameahirisha shauri hilo hadi Agosti 28, 2017 kwa ajili ya kutoa uamuzi wa ama kupokelewa kwa taarifa hiyo ama la.
Masogange amefikishwa mahakamani hapo akidaiwa kutumia dawa za kulevya aina ya heroin kati ya Februari 7 na 14, mwaka huu, katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jijini a Dar es Salaam.
Masogange yupo nje kwa dhamana.