HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » JK: HATUTOKI JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI


Rais Jakaya Kikwete akilihutubia Bunge.PICHA|MAKTABA

Dodoma:Rais Jakaya Kikwete amesema Tanzania haitajitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), licha kuwapo kwa vitendo alivyoviita vya ubaguzi vinavyofanywa na wakuu wa nchi za Uganda, Kenya na Rwanda.
Rais Kikwete akilihutubia Bunge jana mjini Dodoma alifichua kwamba sababu kubwa ya viongozi hao kuonekana kama wanaitenga Tanzania ni msimamo wake kuhusu masuala ya Shirikisho la Kisiasa, Uhamiaji, Ardhi na Ajira.
Rais alikuwa akirejea matukio ya hivi karibuni ya marais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Uganda, Yoweri Museveni na Rais wa Rwanda, Paul Kagame kukutana na kujadiliana kuhusu masuala kadhaa yanayohusu EAC bila Tanzania kuwapo.
“Hatuna mpango wa kuondoka, tupo na tunaendelea kuwepo na napenda niwahakikishie kwamba Tanzania haijafanya jambo lolote baya kwa jumuiya yetu au kwa nchi mwanachama mmoja mmoja na tumekuwa waaminifu na watiifu kwa jumuiya wakati wote,”alisema Rais Kikwete.

ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI

 
Aliwashutumu viongozi wao akisema kuwa kauli zao kwamba wanakutana kwa sababu wako tayari ni za kibaguzi kwani katika mikutano yote waliyoifanya Entebbe nchini Uganda, Mombasa – Kenya na Kigali nchini Rwanda hawakuwahi kuialika Tanzania.
“Hali hii haijawahi kuwapo na ni kwa mara ya kwanza tunaanza kuwa na makundi ndani ya jumuiya yetu; huku Kenya, Uganda na Rwanda, kule Tanzania na Burundi,”alisema Kikwete katika hotuba yake iliyochukua saa1:15 na kuongeza:
“Ikiwa itakuja kutokea jumuiya ikadhoofika au ikafa, Mungu apishilie mbali Tanzania isije ikanyooshewa kidole kwamba ndiyo chanzo cha kudhoofika huko au kufa huko”.
Alisema ataendelea kuzungumza na viongozi wa nchi hizo, na kwamba tayari ameanza ili kuhakikisha utekezaji wa mambo yote ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanywa kwa kuzingatia mkataba ulioanzisha jumuiya hiyo.
Rais Kikwete alisema kwa mujibu wa mkataba huo mambo yote yanapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia kalenda ambayo inaweka bayana mambo hayo kuwa ni Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa Sarafu na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Alisema licha ya kuwapo kwa mambo hayo kwenye mkataba ambao umesainiwa na nchi wanachama, Kenya, Uganda na Rwanda wamechukua baadhi ya mambo ambayo kimsingi ni ya jumuiya na kuanza kuyaweka chini ya himaya yao.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni Umoja wa Forodha na Shirikisho la Kisiasa ambayo taarifa zake zilipaswa kuwasilishwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi uliopangwa kufanyika Kampala, Uganda, Novemba 30 mwaka huu.
Kuhusu Umoja wa Forodha, Rais Kikwete alisema walikubaliana kwamba bidhaa zitozwe ushuru pale zinapoingizwa tu na baadaye kuwepo utaratibu wa nchi iliyotoza ushuru husika kwenda katika nchi ambayo bidhaa hizo zinapelekwa, lakini kabla ya utekelezaji waliwaagiza mawaziri kuandaa utaratibu mwafaka.

Kuhusu Shirikisho la Kisiasa, alisema nchi wanachama katika mkutano wa Novemba 30 mwaka jana walikubaliana kwamba lifanyiwe kazi na kwamba taarifa yake pia inapaswa kuwasilishwa katika mkutano wa Kampala.
“Na maagizo yetu katika mkutano wa 15 wa wakuu wa nchi utakaofanyika Novemba 30 mwaka huu mjini Kampala taarifa hiyo itolewe na uamuzi ufanyike, hata hivyo, tunashangaa wenzetu katika mambo waliyokubaliana wanataka kuanza mara moja, wanaanza kwa utaratibu upi?,”alihoji.
Kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki, Rais Kikwete alisema katika mkutano wa 14 wa Novemba 30 mwaka 2012 jijini Nairobi, walipokea taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusiana na kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki.
“Mkutano kujadiliana zaidi kuhusiana na mpango kazi wa kufikia shirikisho la kisiasa na mpango wa kufikia mambo mengine, kukawa na timu ya watalaamu na inategemewa Baraza la Mawaziri litawasilisha mpango huo katika mkutano ujao;
“Kwa kweli unajiuliza hadi unachoka, wenzetu hawa wamekosa imani na jumuiya?
Wanataka kuunda yao ama wanaichukia nchi yetu? Na hivyo wameamua kutufanyia vitimbi tutoke au sijui wanachuki na mimi,”alisema.

Shirikisho la Kisiasa
Rais Kikwete alitumia muda mwingi kufafanua suala la Shirikisho la Kisiasa akisema hatua hiyo kama inavyoonekana kwenye mkataba ni ya mwisho na inapaswa iridhiwe na nchi wanachama kwa kura ya maoni.
“Sisi tuna uzoefu maana tumekuwa na muungano kwa miaka 50, tumewaambia mara nyingi wenzetu kwamba jamani, ili kufikia katika ngazi hiyo lazima kwanza tujenge uchumi wetu maana huo ndio msingi imara wa kuwa na shirikisho,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tunataka shirikisho lijengwe kwenye msingi imara baada ya kuwapo na mtangamano wa kiuchumi, tukifanya hivyo tutakuwa tumefanya kazi nzuri kwa manufaa ya nchi wanachama na wananchi katika katika nchi zetu, msukumo haupaswi kuwa shirikisho la kisiasa”.
Alisema msukumo wa kutaka kuharakishwa kwa hatua hiyo ndani ya EAC haujaanza leo kwani 2001 iliundwa tume ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Amos Wako ambayo iliweka wazi hisia za Watanzania katika masuala ya msingi ndani ya jumuiya hiyo.
Alisema 2006 wakati hoja ya kutaka kuharakishwa kwa shirikisho ilipoibuliwa tena, Tanzania iliunda tume iliyoongozwa na Profesa Samuel Wangwe na matokeo yake yalionyesha kuwa asilimia 74 ya Watanzania walikuwa wakitaka kuwapo shirikisho, lakini kati yao ni asilimia 24 tu waliotaka kuharakishwa kwake.

“Kwa hiyo sisi tunatekeleza matakwa na uamuzi wa Watanzania kwa Serikali yao ambao walitaka tutekeleza mambo haya kwa hatua, msimamo huu uko wazi na tumekuwa tukiusema katika vikao halali na siyo kwa kificho hata kidogo,”alisisitiza.
Kuhusu tuhuma kwamba Tanzania imekuwa kikwazo cha utekelezaji wa mipango ya EAC, Rais Kikwete alikanusha akisema siyo kweli kwani ushiriki wake umewezesha kutekelezwa kwa mipango mingi ikiwamo ya ujenzi wa mtandao wa barabara katika nchi wanachama.
“Tuhuma hizo hazina mashiko maana mtu mwenye akili timamu huwezi kulipa ada ya Dola milioni 12 za Marekani kila mwaka, maana tunalipa halafu tukawa watu wa kukwaza jumuiya, haiwezekani hata kidogo,”alisema Kikwete.

Mambo yasiyo ya EAC
Rais Kikwete alisema Tanzania haikuwa na tatizo na baadhi ya mambo ambayo nchi hizo zimeyafanya na miongoni mwake ni matumizi ya vitambulisho vya Taifa kama hati ya kusafiria na viza ya pamoja ya utalii.
“Tuliamua kwa pamoja nchi wanachama waliokuwa tayari waanze. Waliposema tutumie vitambulisho vya Taifa kama hati ya kusafiria badala ya hati ya kusafiria tukasema sisi Tanzania bado hatunavyo,” alisema.
Alisema Tanzania haijafanya jambo lolote dhidi ya jumuiya au nchi yoyote mwanachama na kwamba kama kuna ushahidi waseme.
“Sisi ni wanachama waaminifu na watiifu kwa jumuiya, tunatimiza ipasavyo kwa jumuiya na kushiriki ipasavyo katika kuijenga,”alisema.
Alisema sababu ya nchi tatu zilizopo katika jumuiya hiyo kufanya mambo peke yao bila kuishirikisha Tanzania hayaeleweki.

MWANANCHI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: