MKUTANO wa Tisa wa Bunge la Muungano
unatarajia kuanza kesho Mjini Dodoma, huku ripoti ya Kamati Ndogo ya
Bunge iliyoundwa kuchunguza tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge
ikisubiriwa kwa hamu kubwa.
Tume hiyo inayoongozwa na Hassan Ngwilizi iliundwa
na Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo
zilizoibuka katika mkutano wa Bunge uliopita. Tuhuma hizo ndizo
zilizomfanya Spika kuivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.
Baada ya kuibuka kwa tuhuma hizo, Agosti mwaka huu, Makinda aliunda tume ya wabunge watano kuchunguza tuhuma hizo.
Ripoti hiyo inatarajiwa kuwa mtihani mkubwa kwa
Spika Makinda hasa ikizingatiwa kwamba ndiye mwenye mamlaka ya
kuwasilisha ripoti hiyo bungeni hasa kutokana na kuibuka kwa maneno ya
chinichini kwamba kumekuwa na jitihada za kuwasafisha wabunge hasa wa
chama tawala.
Hivi karibuni, Naibu Spika, Job Ndugai alikaririwa
akisema kuwa mamlaka ya namna ya kuiwasilisha ripoti hiyo yako mikononi
mwa Spika Makinda.
“Kwa kawaida na kanuni zetu ni kwamba Spika
anaweza kuamua kama ripoti hiyo ijadiliwe au iwasilishwe kwa njia ipi,
wala hawezi kuingiliwa,” alisema Ndugai.
Mbali na ripoti hiyo, Mkutano huo wa Bunge ambao
utadumu kwa wiki mbili, pia unatarajiwa kupokea hoja binafsi kutoka kwa
Mbunge wa Kisarawe (CCM), Suleiman Jaffo kuhusu mifuko ya jamii.
Jaffo aliibua hoja hiyo katika mkutano uliopita
akitaka itungwe sheria ya kufanya marekebisho ili kipengele kinachomtaka
mwanachama wa mfuko kupewa mafao yake pindi anapofikisha umri wa miaka
55 kiondolewe.
Wakati huohuo, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya
ya Umoja wa Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi walianza kuwasili Dodoma jana
tayari kwa mkutano wa uchaguzi unaotarajia kuanza kesho.
Awali, mkutano huo uliokuwa ufanyike Oktoba 27
hadi 28, lakini ulisogezwa mbele ili kupisha waumini wa dini ya Kiislamu
kuungana na wenzao duniani kusherehekea Sikukuu ya Idd El Haj.
Katika uchaguzi huo nafasi ya mwenyekiti inagombewa na Abdallah Bulembo na John Barongo na Martha Mlata.
Tayari Jumuiya nyingine za CCM za Umoja wa Vijana
(UVCCM) na UWT zimeshafanya uchaguzi wa viongozi wake wa juu wa
kuziongoza kwa kipindi cha miaka mitano.Katika chaguzi hizo, UVCCM ilimchagua Khamis Sadifa Juma kuwa mwenyekiti
wake mpya wakati Sofia Simba alichaguliwa tena kuongoza UWT.
No comments:
Post a Comment