WAZIRI
Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, ameeleza kusikitishwa na kauli
za viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la
Umeme nchini (TANESCO) kuhusu hali ya uzalishaji, usafirishaji na
usambazaji wa umeme nchini sanjari na uboreshaji wa utendaji TANESCO.
Amesema
kauli hizo zinatoa matumaini potofu kwa wananchi na kuwasihi kuzipokea
kwa tahadhari kwa kuwa hazielezi ukweli kuhusu tatizo la umeme nchini.
Mnyika
ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, alitoa kauli hiyo jana katika taarifa
yake kwa vyombo vya habari na kusema kulingana na nyaraka alizonazo za
ndani ya wizara hiyo na TANESCO kuanzia Septemba hadi Oktoba mwaka huu,
hali ya uzalishaji na usafirishaji na usambazaji wa umeme imekuwa tete
kwa sababu mbalimbali ikiwemo upungufu wa upatikanaji wa mafuta na gesi
asili kwa ajili ya uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme na kasi ndogo ya
uwekezaji kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa kudumu.
Mnyika pia
alisema amemwandikia barua Spika wa Bunge, Anne Makinda, ili Wizara ya
Nishati na Madini iwajibike kueleza hali halisi katika mikutano ya
kamati za Bunge inayoendelea.
“Katika
barua hiyo nimependekeza pamoja na mambo mengine suala la kupokea na
kujadili taarifa ya utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na
utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa TANESCO
lishughulikiwe na kamati nyingine kwa haraka kwa kuzingatia maelezo na
maelekezo ya Spika aliyoyatoa bungeni wakati wa kuahirisha mkutano wa
nane wa Bunge,” alisema.
Aidha
alisema mapitio ya utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa
shirika hilo yahusishe kamati ya kudumu ya Bunge na itakayoeleza hatua
iliyofikiwa katika uchunguzi wa tuhuma za ufisadi kwa kuzingatia kuwa
siku 60 za uchunguzi zimepita.
Tanzania Daima




No comments:
Post a Comment