Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), tarehe 20 Oktoba, 2012 kuhusu ugonjwa wa Marburg ambao umejitokeza katika nchi jirani ya Uganda. Maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo ni Wilaya ya Kabale, Kanda ya Kusini Magharibi ya nchi, na wilaya hii inapakana na Rwanda. Mpaka tarehe 24 Oktoba 2012, takriban watu 13 wamepata maambukizo na 6 wamepoteza maisha.
Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa
wananchi wote, katika mikoa yote ya Tanzania na hasa wale waliopo katika
mikoa ambayo inapakana na na nchi jirani ya Uganda (Mikoa ya Mara,
Mwanza, Kagera na Kigoma).
Marburg ni ugonjwa wa hatari unaofanana na Ebola na unasababishwa na virusi vijulikanavyo kwa lugha ya kitaalam “Marburg
Virus”. Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yajulikanayo kwa ujumla
kama Homa za Virusi zinazosababisha kutokwa damu mwilini, (Viral
Haemorrhagic Fevers). Chanzo kamili cha virusi vya ugonjwa huu
hakijulikani. Hali inayosababisha mlipuko wake pia haijulikani. Ugonjwa
huu hauna tiba wala chanjo.
Dalili kuu za ugonjwa huu ni
pamoja na Homa kali, inayoambatana na kutokwa damu katika matundu yote
ya mwili yaani pua, njia ya haja kubwa na ndogo, mdomoni, masikioni,
machoni, hali inayopelekea kifo kwa muda mfupi. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati ya siku 3 hadi 9 baada ya kupata maambukizi.
Ugonjwa huu unaenea
kwa urahisi sana na haraka kutoka mtu mmoja hadi mtu mwingine iwapo
mtu atakuwa karibu na mgonjwa na kugusana na mate, damu, mkojo, machozi,
kamasi, maji maji mengine ya mwili, ikiwa ni pamoja na jasho au
kumgusa mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa Marburg.Ugonjwa huu pia unaweza kuenezwa iwapo mtu atagusa nguo au mashuka ya mgonjwa wa Marburg.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu:
- Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya. Aidha taarifa hii pia imejumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa), “Fact sheet” ya ugonjwa, Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli na vipeperushi vinavyoelezea ugonjwa huu.
- Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipaka. Aidha watalaamu hawa wa Afya pia wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huu ili endapo ugonjwa huo utatokea uweze kutolewa taarifa mapema.
- Kupeleka vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya
Wananchi
wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote
aliyeripotiwa nchini. Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo
cha huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote
atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
Kitengo cha mawasiliano ya Serikali
No comments:
Post a Comment