Utangulizi
Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume, Makamu Mwenyekiti
wa CCM na Rais Mstaafu wa Zanzibar;
Ndugu Pius Msekwa, Makamu Mwenykiti wa CCM wa Bara;
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Ndugu Benjamin William Mkapa;
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Waziri Mkuu;
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Wilson Mukama;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM;
Wageni wetu waalikwa kutoka vyama rafiki,
Ndugu zetu wa Vyama vya Siasa Nchini;
Waheshimiwa Mabalozi,
Viongozi wa Dini,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana;
Kama ilivyo ada, naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi
wa rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa Dodoma, siku
ya leo, kwenye Mkutano Mkuu wa Nane wa Chama cha Mapinduzi.
Ndugu Wajumbe;
Karibuni Dodoma. Karibuni Mkutanoni. Nawapeni pole kwa safari.
Tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika salama na tuombe turejee
makwetu salama. Kwa niaba yenu, niruhusuni niwashukuru wenyeji wetu,
yaani wana-CCM na wananchi wote wa Dodoma, wakiongozwa na Alhaji Adam
Kimbisa, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Mkoa Dkt. Rehema
Nchimbi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Tunawashukuru kwa
kutupokea vizuri na kwa ukarimu wao unaotufanya tujisikie tuko nyumbani
katika huu mji ambao ndiyo Makao Makuu ya nchi yetu na Chama chetu.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Halmashauri Kuu
ya Taifa kwa matayarisho mazuri ya Mkutano huu wa Nane wa Taifa wa CCM.
Natoa pongezi maalum kwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa chini
ya uongozi mahiri wa Katibu Mkuu Ndugu Wilson Mukama na Kamati zote za
Maandalizi ya Mkutano kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya ya kuwezesha
Mkutano huu kufanyika. Kwenu nyote nasema hongereni na asanteni sana.
Ndugu Wajumbe;
Karibuni tena Kizota. Nasikitika kwamba matumaini yangu ya kufanya
Mkutano Mkuu katika ukumbi wetu wenyewe hayakutimia. Hii ni kwa sababu
kazi ya matayarisho imechukua muda mrefu kuliko nilivyotazamia.
Tumechelewa kupata kiwanja kilichokidhi mahitaji yetu na matazamio
yetu. Kwanza tulipata kiwanja nyuma ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Lakini tukaona ni mbali mno na walipo wananchi. Tukaja kupata kiwanja
kingine juu ya Kilimani Club ambacho hakikuwa kikubwa cha kutosha.
Mapema mwaka huu ndipo tulipopata kiwanja eneo la Makulu ambacho
kinakidhi sifa za kuwa kikubwa cha kutosha na kuwa karibu na katikati ya
mji wa Dodoma. Tumekiafiki na matayarisho ya kuanza ujenzi
yamekamilika. Leo asubuhi tumeweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa
Ukumbi wa Mkutano (Dodoma Convention Centre). Baadae utafuta ujenzi wa
jengo la Makao Makuu ya CCM na jengo la Hoteli ya Kisasa.
Wageni Karibuni
Ndugu Wajumbe;
Kama mjuavyo Chama cha Mapinduzi kina marafiki wengi Afrika na
kwingineko duniani. Tumekuwa na mazoea ya kualikana katika mikutano
mikuu yetu. Safari hii tumefanya hivyo tena. Kwa niaba yenu niruhusuni
niwashukuru sana wageni wetu wote wa kutoka vyama rafiki Afrika na
duniani kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kujumuika nasi siku ya leo.
Kuwepo kwao ni kielelezo tosha cha udugu na urafiki uliopo baina ya
vyama vyetu na nchi zetu ambao hatuna budi kuudumisha, kuuendeleza na
kuukuza. Hali kadhalika, nawashukuru Mabalozi wa Nchi za Nje na
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa walioweza kuja kushiriki nasi
katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano wetu.
Ndugu Wajumbe;
Tunawakaribisha kwa furaha na upendo mkubwa viongozi na wawakilishi
wa vyama vya siasa vya hapa nchini kwa kukubali mwaliko wetu na kuja
kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM siku ya leo. Tunawashukuru kwa
moyo wao wa uungwana kwani tofauti za vyama si uadui. Wamethibitisha
jinsi demokrasia ya vyama vingi inavyozidi kustawi na kukomaa hapa
nchini.
Nawashukuru sana pia, viongozi wetu wa dini na wananchi mbalimbali
waliojumuika nasi. Kuwepo kwao ni jambo la faraja kubwa. Dua za
viongozi wa dini zitasaidia kuponya na kuupa baraka mkutano wetu uende
salama, uwe wa mafanikio na kuwafanya wale wote wasiokiombea mema Chama
chetu watahayari na kufadhaika.
Karibuni Diaspora
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuwatambua na kuwakaribisha
viongozi na wananchama wa Chama chetu waliopo nje, Marekani, Italia,
India na Uingereza. Ndugu zetu hawa kwa upenzi wao kwa Chama wamesafiri
masafa marefu kuja kushiriki nasi. Hawa wanastahili pongezi maalum kwa
jinsi wanavyopeperusha bendera ya CCM na kueneza sera zake. Naomba
tuwape makofi ya nguvu.
Agenda ya Mkutano
Ndugu Wajumbe;
Agenda ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa Nane wa Chama cha Mapinduzi ina
mambo makuu manne. Kwanza kufanya marekebisho ya Katiba ya Chama cha
Mapinduzi. Mengi ya marekebisho hayo yanatokana na uamuzi wa
Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake cha trehe 11 – 12 Aprili
2011 wa kufanya mageuzi ndani ya Chama. Miongoni mwa matunda ya mageuzi
hayo ni kuundwa kwa Baraza la Ushauri na Wajumbe wa NEC kuchaguliwa
Wilayani badala ya Mikoani.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Halmashauri Kuu ya Taifa ina mamlaka ya
kufanya marekebisho ya Katiba na marekebisho hayo kutumika. Hata hivyo,
marekebisho hayo hayana budi kuletwa katika Mkutano Mkuu wa Taifa ili
yaingizwe rasmi kwenye Katiba.
Ndugu Wajumbe;
Jambo la pili litakuwa ni kwa Serikali zetu mbili kutoa taarifa za
maendeleo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2010 – 2015 tangu baada
ya uchaguzi mkuu hadi sasa. Vile vile, tutapokea Taarifa ya
Halmashauri Kuu ya Chama kuhusu kazi za Chama kwa miaka mitano
iliyopita. Jambo la nne na la mwisho ni kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti,
Makamu wake wawili na Wajumbe wa NEC wa Kundi la Zanzibar na Tanzania
Bara.
Ndugu Wajumbe;
Tofauti na mikutano iliyopita, Halmashauri Kuu ya Taifa inapendekeza kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wajigawe katika makundi matano
kujadili taarifa ya kazi za Chama na zile za utekelezaji wa Ilani.
Kisha kila kikundi kitatoa taarifa ya maoni na mapendekezo yake. NEC
ilifikiria iwe hivyo ili kutoa muda wa kutosha kwa wajumbe kujadili
taarifa hizo muhimu katika utaratibu wa zamani wa mtu mmoja kila mkoa
kuitwa kusoma, wajumbe hawapati fursa ya kutosha ya kuzijadili taarifa
zinazotolewa.
Kuimarisha Chama Kazi Endelevu
Ndugu Wajumbe;
Katika hotuba yangu ya kushukuru baada ya kuchaguliwa kwa mara ya
kwanza kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwenye Mkutano Mkuu wa
Taifa Maalum wa tarehe 25 Juni, 2006, pamoja na kuzungumzia mambo
mengine, nilisisitiza umuhimu wa kuimarisha Chama chetu. Nilitoa maoni
yangu kwa upana kiasi kuhusu mambo ya kuzingatia. Leo tena, katika
ufunguzi wa Mkutano Mkuu huu narudia kusisitiza jambo hili. Nafanya
hivyo kwa sababu hilo ndiyo jukumu la kudumu na jukumu la kwanza na la
msingi kwa kila kiongozi na kila mwanachamawa CCM. Isitoshe, kwa hali
ilivyo sasa, kuimarisha Chama cha Mapinduzi lazima iwe agenda kuu ya
kila mmoja wetu. Ni ukweli ulio wazi kuwa ustawi na uhai wa Chama
unategemea viongozi na wanachama kufanya kazi ya ziada kuimarisha Chama
chao.
Ndugu Wajumbe;
Bahati nzuri, chini ya uongozi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu
Lt. Yusuf Rajab Makamba tarehe 19 Desemba, 2006 ulianzishwa Mradi wa
Kuimarisha Chama. Mradi huo ndiyo uliokuwa dira na mwongozo wetu wa
kufanya kazi za Chama tangu wakati huo mpaka leo. Wajibu wa kila
kiongozi na kila mwanachama na kila kikao cha kila ngazi vimeainishwa
vizuri. Pia, uliwekwa utaratibu mzuri wa kufuatilia utekelezaji wake.
Bila ya shaka mtakumbuka kuwa utaratibu maalum uliwekwa wa kutoa tuzo
kwa Mikoa iliyofanya vizuri katika utekelezaji wa vipengele mbalimbali
vya uimarishaji wa Chama kwa mujibu wa Mradi huo.
Ndugu Wajumbe;
Kazi ya kuimarisha Chama chetu ni jukumu endelevu kwa kila mwanachama
wa CCM, kila kiongozi wa CCM na kila mtumishi wa CCM. Kwa sababu hiyo,
Mradi wa Kuimarisha Chama ni mchakato usiokuwa na ukomo. Ni kazi ya
kudumu na wala siyo tukio lililoanzishwa na Katibu Mkuu Lt. Yusufu
Rajabu Makamba na kukoma siku alipostaafu.
Tuongeze Wanachama
Kazi ya kuingiza wanachama wapya ni ya kudumu katika uhai
wa Chama cha Mapinduzi. Hii siyo kazi ya msimu wa uchaguzi wa ndani ya
Chama au wakati wa kura za maoni na hivyo kugeuzwa kuwa ni kwa ajili ya
kuwapigia debe watu wanaotafuta vyeo. Lazima wakati wote tuwe
tunaingiza wanachama wapya lakini pia lazima tuzingatie utaratibu
ulioelekezwa na Katiba ya CCM. Hatuna budi kuhakikisha kuwa tuna
wanachama walio waumini wa kweli na wapenzi wa dhati wa CCM, itikadi
yake na sera zake na zile za Serikali zake.
Ndugu Wajumbe;
Wanachama ndiyo nguvu kuu ya uhai na ushindi wa CCM. Lazima Chama
chetu kiwe na Jeshi kubwa la wanachama walio tayari kukijenga, kukisemea
na kukipigania. Kuwa na Wanachama wengi ambao ni waumini wa kweli wa
Chama chetu ina maana ya kuwa na kura nyingi za msingi za kuanzia katika
uchaguzi wa dola. Pia wanachama ni nyenzo muhimu ya CCM kupata kuungwa
mkono na wananchi hasa pale ambapo wanachama wataifanya ipasavyo kazi
ya Chama ndani ya umma. Kila mwanachama akifanya kwa mafanikio kazi ya
kushawishi wananchi kupigia kura wagombea wagombea wa CCM tutapata kura
nyingi za uhakika.
Tuwe na Viongozi Wazuri
Ndugu Wajumbe;
Kazi ya kuhakikisha kuwa Chama cha Mapinduzi kina viongozi wazuri ni
ya kudumu na wala siyo ya msimu wa kuchuja majina ya wagombea. Lazima
Chama chetu kiwe na viongozi ambao ni waumini wa dhati wa itikadi yetu
na wanaozijua vyema sera za Chama cha Mapinduzi na Serikali zake. Wao
ndio wanaotarajiwa kuonesha njia kwa kuelimisha wanachama na wananchi.
Viongozi wa CCM lazima wawe hodari wa kufafanua sera na masuala
mbalimbali yahusuyo Chama chetu na Serikali zake. Hawataweza kufanya
hivyo kama wao wenyewe ni maamuma. Kiongozi mzuri wa Chama cha
Mapinduzi ni yule ambaye ni jasiri kukitetea Chama cha Mapinduzi na kama
hapana budi yuko tayari kujitolea muhanga. Kuwa na kiongozi ambaye
haguswi wala kusikitishwa na hali mbaya ndani ya Chama au hujuma dhidi
ya Chama ni sawa na kutokuwa na kiongozi. Bora asiwepo. Na kuwa na
kiongozi ambaye yeye mwenyewe anafanya vitendo viovu dhidi ya CCM na
Serikali zake ni kuwa na nyoka ndani ya nyumba. Ni jambo hatari
lisilokubalika na halistahili kuvumilika. Tukiwajua tuwaseme,
tuwashughulikie, wachague wanapotaka kwenda.
Ndugu Wajumbe;
Kiongozi mzuri wa CCM lazima awe muaminifu na muadilifu na lazima
wanachama na jamii imuone hivyo. Chama chetu kinashindania kushinda
akili na mioyo ya Watanzania na hiyo ndiyo kazi tunayomtarajia kiongozi
wetu afanye katika jamii. Hii ndiyo hasa kazi ya Chama ndani ya umma.
Lakini, ili kiongozi wetu aweze kuifanya kwa mafanikio taswira yake
mbele ya jamii ni kitu muhimu. Awe na taswira nzuri mbele ya wananchi.
Kama jamii inamuona kuwa si mtu muadilifu itakuwa taabu sana kwake
kufanikisha jukumu la msingi la Chama chetu. Hivyo ndugu zangu, lazima
tuhakikishe kuwa viongozi wetu wanakuwa waadilifu ili wasigeuke kuwa
balaa na hasara kwa Chama.
Ndugu Wajumbe;
Baada ya kukamilisha mchakato wa uchaguzi ngazi ya taifa,
tutatengeneza na kutekeleza programu maalum ya kutoa mafunzo kwa
viongozi wa Chama kuanzia ngazi ya Tawi hadi Taifa. Hali kadhalika,
tutaendeleza na kukamilisha kazi ya ukarabati na upanuzi wa Chuo cha
Ihemi ili kiwe kitovu cha kutoa mafunzo ya siasa kwa makada na viongozi
wa Chama na Jumuiya zake kama ilivyokuwa inafanywa katika Chuo cha CCM
cha Kivukoni na vyuo vyake vya kanda.
Ndugu Wajumbe;
Bahati nzuri vyama vya ukombozi vya nchi za Mashariki, Kati na Kusini
mwa Afrika vimekubaliana kuwa Chuo cha Ihemi kiwe Chuo cha Mafunzo ya
siasa kwa makada wa vyama vyao pia. Ni heshima kubwa kwa CCM, lakini
pia inakipa Chama chetu wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa Chuo hicho
kinawekwa katika viwango vya kimataifa. Tuko tayari na tutajipanga
ipasavyo kutimiza wajibu wetu huo wa kihistoria.
Vikao Vifanyike Ipasavyo
Ndugu Wajumbe;
Ni kazi endelevu kwetu sote, wanachama na viongozi, kuhakikisha kuwa
vikao vinafanyika kwa wakati na kwamba mikutano inaendeshwa vizuri na
ina agenda zenye maslahi ya kujenga Chama na kuendesha nchi. Pia, ni
muhimu kuhakikisha kuwa kinachoamuliwa kinatekelezwa ipasavyo. Naamini
kwamba mafunzo tutakayotoa kwa viongozi na watendaji wa Chama kuhusu
wajibu wao na jinsi ya kuutekeleza yatasaidia sana kuimarisha CCM.
Watendaji Mahiri
Ndugu Wajumbe;
Kwa Chama chetu kuwa na watendaji wazuri ni jambo lisilokuwa na
mjadala. Lazima tuwe na watendaji ambao ni makada wazuri na watu mahiri
kwa kazi zao. Wawe ni watu ambao wana uelewa mzuri wa sera za Chama na
kwamba wanaweza kuzifafanua, kuzieneza na kuzitetea. Pia, wawe ni watu
wanaojua vyema kazi yao ya utendaji, kwa mujibu wa shughuli zao
wanazozifanya. Ni vyema kwa kazi za kitaalamu tukapata watu wataalamu
wa kazi hizo. Ni muhimu sana tukayazingatia haya kwani utendaji mzuri
katika Chama ni nguvu muhimu sana ya kukifanya Chama chetu kuwa imara.
Chama chetu kiwe na mipango thabiti ya kuwaendeleza watumishi wake na
kama hapana budi kuwadhamini wakasome. Tufanye hivyo.
Bila ya shaka mtakumbuka kuwa tarehe 3 Novemba, 2007, pale Kizota,
niliahidi kuwa tutaboresha maslahi ya watumishi wa Chama. Tumetimiza
ahadi hiyo. Leo nasema kuwa tutajitahidi kuendelea kuboresha maslahi ya
watumishi wetu kadri uwezo utakavyoruhusu.
Tujitegemee
Ndugu Wajumbe;
Lazima Chama chetu kiwe na uwezo wake chenyewe wa kujisimamia na
kujiendesha. Kiwe na fedha za kutosha na vitendea kazi. Hivi sasa
hatuko hivyo. Hatuna budi kuongeza maarifa na juhudi za kukiwezesha
Chama cha Mapinduzi kujitegemea kifedha bila ya kujali kama kuna ruzuku
au hakuna. Jambo hili sasa liwe ni la kufa na kupona kwetu kuhakikisha
linakuwa. Iwe agenda kuu ya Chama katika ngazi zote. Kila mmoja
afikirie nini cha kufanya na kifanywe. Jambo la kuzingatia ni kufanya
shughuli halali. Fursa zipo tuzitumie. Tusikubali kushindwa kwenye
azma kwani hiyo itakuwa maangamizi wa CCM. Lazima tushinde.
Ndugu Wajumbe;
Mtakumbuka pia kwamba niliahidi
kuimarisha usafiri ndani ya Chama. Ahadi hiyo tumeitimiza. Kila Mkoa
na kila Wilaya imepata gari mpya tena gari nzuri na imara. Gari hizi
tukizitunza vizuri zitatuwezesha katika uchaguzi ujao bila ya taabu.
Kwa Mikoa na Wilaya mpya mipango ya kuwapatia magari iko mbioni. Kila
Jumuiya tuliipatia magari yasiyopungua matatu.
Jumuiya za Chama
Ni wajibu wa kudumu wa Chama chetu kuhakikisha kuwa Jumuiya zake
zinaimarika na kutimiza ipasavyo wajibu wake. Jumuiya ndiyo mkono mrefu
wa Chama cha Mapinduzi kuufikia umma mpana wa Watanzania hasa wale
ambao si wanachama. Jukumu letu ni kuhakikisha kuwa watu hao wanakuwa
wanachama au wapenzi na marafiki wa CCM. Kwa hiyo, kuwepo kwa Jumuiya
ni fursa nzuri kwa Chama cha Mapinduzi kuungwa mkono na watu wengi ili
wakati wa uchaguzi tuweze kupigiwa kura na kupata ushindi. Jumuiya
lazima zihakikishe kuwa zinatimiza ipasavyo wajibu wake ili wasiipotezee
CCM fursa hii adhimu.
Ndugu Wajumbe;
Kwa muhtasari, hayo ndiyo baadhi ya mambo ya msingi ya mradi wa
kuimarisha Chama. Mtakubaliana nami kuwa haya yote ndiyo kazi na wajibu
wa kila mmoja kufanya. Ni kazi endelevu isiyokuwa na ukomo. Tupo kwa
ajili hiyo na rai yangu kwenu ni kuhakikisha kuwa kila mwanachama na
kila kiongozi anatimiza ipasavyo wajibu wake.
Mageuzi Ndani ya Chama
Ndugu Wajumbe;
Kwa dhamira ya kuendelea kukiimarisha zaidi, Chama cha Mapinduzi,
katika mkutano wake wa tarehe 11-12 April, 2011, Halmashauri Kuu ya
Taifa iliamua kuanzisha mchakato na kufanya mageuzi ndani ya Chama.
Lengo kuu la uamuzi huo ni kukiwezesha Chama chetu kuwa na taswira
inayovutia katika mitazamo na hisia za wanachama wake na wananchi.
Kimsingi NEC inataka tukiwezeshe Chama cha Mapinduzi kiendelee
kupendwa na kuaminiwa na wananchi wote wa Tanzania. Tunataka wanawake
na wanaume, wadogo na wakubwa, maskini na matajiri, wanyonge na wenye
nguvu waone kuwa CCM ndiyo kimbilio lao.
Ndugu Wajumbe;
Kwa ajili hiyo mageuzi ya ndani ya Chama yamejengeka juu ya misingi ifuatayo:-
- Kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kuwa na makada na viongozi mahiri, waadilifu na waaminifu kwa Chama chao;
- Kukiwezesha Chama kuwa na sera zinazojali maslahi ya wengi na kusukuma mbele kwa kasi maendeleo ya taifa letu;
- Kukiwezesha Chama kuwa na muundo na mfumo wa uendeshaji ulio nyumbulifu na unaokifanya kuwa karibu na wanachama na wananchi;
- Kukiwezesha Chama kujitegemea kimapato na kiuchumi ili kiweze kuendesha shughuli zake kwa uhakika, uhuru na heshima;
- Kukiwezesha Chama kuwa na watu hodari wa kazi na Makada wazuri ambao wanalipwa vizuri na kuwezeshwa kutekeleza majukumu yao;
- Kukiwezesha Chama kuwasiliana na umma kwa urahisi na kupambana na propaganda chafu za vyama vya siasa; na
- Kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kupambana na maovu ndani ya Chama na katika jamii likiwemo tatizo la rushwa na mengineyo.
Ndugu Wajumbe;
Katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa iliamuliwa kuwa kutokana
na umuhimu wa hoja na haja ya kufanya mageuzi ndani ya Chama utekelezaji
wa mageuzi uanze mara moja. Aidha, pawepo na progamu ya utekelezaji
unayoainisha nini kinafanyika lini na mhusika ni nani! Bila ya shaka
mtakumbuka kuwa katika kikao kile, tuliunda upya Kamati Kuu na kuteua
Sekretarieti mpya. Vile vile iliamuliwa kuwa tufanye marekebisho katika
muundo wa Chama na moja ya matokeo yake ni Wajumbe wa Halmashauri Kuu
ya Taifa kuchaguliwa kutoka wilayani. Nafasi za NEC za mikoa zikafutwa
na zile za taifa zikapunguzwa. Aidha, limeundwa Baraza la Taifa la
Ushauri ambalo wajumbe wake ni viongozi wakuu wa Chama wastaafu.
Wanapata fursa ya kukaa na kutoa ushauri kwa Chama na viongozi wake.
Ndugu Wajumbe;
Tuliamua, pia, kuunganisha chaguzi za Chama na Jumuiya zifanyike
mwaka mmoja. Shabaha ya uamuzi huo ni kutaka kujipa muda wa kutosha wa
kujenga Chama na Jumuiya zake na kujiandaa kwa chaguzi za dola. Uamuzi
huo umeokoa takriban mwaka mzima ambao tulikuwa tunautumia kwa
uchaguzi. Vile vile Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua kwamba mgao wa
fedha unatokana na mapato Chama zinazopelekwa kwenye Matawi na Mashina
uongezwe. Lengo ni kuziwezesha ngazi hizi muhimu za Chama kufanya kazi
vizuri zaidi.
Ndugu Wajumbe;
Suala la nidhamu na maadili ya viongozi na wanachama lilisisitizwa
sana kwa sababu ya umuhimu wake kwa taswira ya Chama chetu mbele ya
jamii na wanachama wake. Pia, kutokana na ukweli kwamba ni kilio cha
wanachama na wananchi cha kutaka tuiondowe taswira mbaya dhidi ya Chama
iliyopo katika jamii kuwa ni Chama kisichokerwa na rushwa. Hicho ni
kilio cha dhati kwa watu wenye nia njema na CCM: Chama chao,
wanachokipenda na kukiamini. Chama ambacho bado hakina badala yake wa
kuiongoza vyema nchi yetu na watu wake.
Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua mambo mawili yafanyike. La kwanza,
mfumo mzima wa kushughulikia masuala ya usalama na maadili katika Chama
utazamwe upya na uimarishwe. Pili, Chama kichukue hatua na lazima
kionekane kinachukua hatua dhidi ya viongozi na wanachama wasiokuwa
waadilifu na waaminifu wanaofanya sura ya Chama ichafuke mbele ya
jamii. NEC iliagiza wenyewe wajipime na kuamua na wasipofanya hivyo
vikao husika katika Chama vichukue hatua.
Ndugu Wajumbe;
Hayo ni baadhi tu ya mambo muhimu yaliyoamuliwa yafanyike katika
kufanya Mageuzi Ndani ya Chama. Utekelezaji wake umeanza. Yapo
yaliyokamilika na yapo yanayoendelea kutekelezwa. Yapo mambo mengi
ambayo ni endelevu kama vile mapambano dhidi ya rushwa. Hatuna budi
kuendelea kulikemea na kusimama kidete kupambana na tatizo hili mpaka
likomeshwe. Ni kwa maslahi na heshima ya Chama chetu kuendesha
mapambano haya bila ya woga mpaka tushinde. Tukishindwa itakuwa hatari
kwa uhai wa Chama chetu.
Umoja ni Ushindi
Ndugu Wajumbe;
Mara ya mwisho tulipokutana tarehe 11 Julai, 2010, tulikuwa
tunajipanga kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Mliniteua mimi
na Dkt. Mohamed Ghalib Billal kupeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya
Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia
tulipitisha Ilani ya Uchaguzi ya 2010-2015. Siku moja kabla ya Mkutano
Mkuu, Halmashari Kuu ya Taifa ilikuwa imemteua Dkt. Ali Mohamed Shein
kupeperusha bendera yetu kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar.
Bahati nzuri tumepata ushindi kwa nafasi zote hizo za juu za uongozi
wa taifa letu. Pia tulifanikiwa kupata Wabunge na Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi wengi zaidi kuliko vyama vya upinzani. Kwa sababu hiyo,
tumeunda Serikali zote mbili za nchi yetu na utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi unaendelea vizuri.
Ndugu Wajumbe;
Kwa upande wa Zanzibar, tuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa na mambo
yanakwenda vizuri. Tuzidi kuunga mkono na kuwatakia heri Rais wa
Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa
Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd.
Tunawapongeza sana kwa mafanikio yaliyopatikana. Zanzibar ina amani na
umoja unaozidi kuimarika. Tunatakiwa tuendelee kuiunga mkono Serikali
ya Umoja wa Kitaifa ili ifanikiwe zaidi.
Ndugu Wajumbe;
Uchaguzi uliopita kwa upande wa Tanzania Bara ulikuwa na changamoto
nyingi ambazo hatukuzizoea wala kujiandaa nazo. Zinaelezea matokeo
tuliyoyapata jambo ambalo linatulazimu kuwa makini zaidi katika uchaguzi
ujao. Tusikubali kushtukizwa tena. Lakini, jambo moja lililo dhahiri
ni kwamba umoja na mshikamano miongoni mwa wana-CCM ndiyo uliotuwezesha
kukabili changamoto hizo na kupata ushindi tulioupata. Bila ya hivyo,
mbinu hasi zilizotumika zingetufanya tushindwe.
Napenda ukweli huu uwepo katika vichwa na mioyo ya wana-CCM na sisi
viongozi wao tuliochaguliwa hivi majuzi na watakaochaguliwa katika
Mkutano huu. Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema: Umoja ni Nguvu, ni kweli kabisa na sisi ni mashahidi. Nami napenda kuongeza kwa kusema kuwa Umoja ni Ushindi.
Ndugu Wajumbe;
Nawaomba wakati wote wa mkutano na baada ya mkutano tukumbuke na
kuzingatia Umoja. Tuishikilie kamba ya Umoja isituponyoke. Tuimbe
Umoja kimoyo moyo na tubainishe wazi wazi kwa kauli na matendo yetu
kuwa: Umoja ni Nguvu Utengano ni Udhaifu! Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi!. Napenda
kuona kuwa tunatoka hapa tukiwa kitu kimoja, tukiwa watu tunaopendana
na tulioshikamana. Nataka tuondoke katika Mkutano sote tukivuta kamba
upande mmoja badala ya kuvutana. Nataka tuazimie kukabiliana na kauli,
matendo au watu wanaopandikiza chuki na kuhatarisha umoja ndani ya Chama
chetu na miongoni mwetu. Nataka kaulimbiu ya ujumbe wa Mkutano huu
uwe Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi! Tukiendelea
kuwa watu tunaovutana na kuhasimiana hatutaweza kukijenga Chama chetu
wala kuwatafutia ushindi wagombea wa Chama chetu. Tutakuwa sawa na ule
msemo wa Kiswahili usemao: “vita vya panzi furaha ya kunguru” Tusijigeuze panzi na wala tusikifikishe Chama chetu kiwe hivyo.
Ndugu Wajumbe;
Mtakubaliana nami kuwa harakati za kutafuta uongozi ndani ya Chama au
uteuzi wa kugombea katika chaguzi za dola imekuwa ndiyo chanzo kikuu
kinacholeta mifarakano na kuvuruga umoja ndani ya Chama chetu. Hili
ndugu zangu siyo sawa hata kidogo. Kugombea uongozi ni haki ya msingi
ya mwanachama na raia wa Tanzania. Kwa nini mtu achukiwe au aonekane
adui kwa kuamua kuitumia haki yake hiyo? Kwa nini afanyiwe vitimbi,
vitendo viovu au njama za kuhujumiwa? Nani mwenye haki zaidi ya
mwanachama ama raia mwenzake? Ni ubabe na jeuri ya pesa isiyokuwa na
msingi. Ni ubinafsi na uchu wa madaraka uliopitiliza mipaka. Watu wa
namna hiyo ni hatari sana kwani wanaweza hata kuua au kukivuruga Chama
chetu kizuri kama tamaa zao zisipokidhiwa.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wale wote wanaochukiana kwa
sababu ya kugombea watakafakari upya misimamo yao. Wafanyayo siyo
sahihi, wanaathiri nguvu na uhai wa Chama chetu. Naomba Kamati za Siasa
za ngazi zote ziwatambue watu hao na kuwaita kuwapatanisha. Naomba
wahusika watoe ushirikiano wao. Hata wale wanaohisi kuwa hawakutendewa
haki katika uchaguzi, walidhulimiwa au hata kushindwa kwa sababu ya
vitendo vya rushwa, wakumbuke kuwa Chama chetu kina utaratibu wa
kushughulikia malalamiko yao. Wautumie utaratibu huo badala ya kufanya
vitendo vinavyokigawa na kukivuruga Chama chetu. Kulalamika katika
vyombo vya habari, kufanya ghasia au kuchochea migawanyiko hakutaleta
ufumbuzi.
Ndugu Wajumbe;
Niruhusuni nitumie nafasi hii kuwasihi wale wote wenye tamaa ya
kugombea uteuzi ndani ya Chama wasituulie Chama chetu. Kuwa na tamaa ya
kugombea Urais, Ubunge na Udiwani si kosa ni haki ya mwanachama na ni
haki ya raia wa nchi hii. Jambo ambalo halikubaliki na gumu kulivumilia
ni kufanya vitendo vya kuwagawa wanachama na Chama chetu.
Kuwalazimisha au kuwashinikiza kujiunga na kundi fulani siyo sawa.
Kumchukia mtu kwa sababu naye anagombea au amekataa kukuunga mkono au
kumuunga mkono umpendae ni jambo baya. Unaifanya demokrasia iwe haina
maana au kichekesho. Na, lililo baya kupita kiasi ni kutumia fedha
kushawishi, kuwarubuni au kuwanunua watu kukuunga mkono au kumuunga
mkono mgombea wako au kujiunga na makundi. Hili ni jambo haramu na ni
utovu wa maadili usiokubalika ambao lazima tuukatae, tuukemee na tuupige
vita kwa nguvu zetu zote. Naomba wote tushirikiane katika mapambano
haya kwa heshima ya Chama chetu.
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
Ndugu Wajumbe;
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 unakwenda vizuri kwa
Serikali zetu zote mbili. Taarifa zitakazotolewa na Waziri Mku,
Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa upande wa Serikali ya Muungano na Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd kwa upande
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, zitathibitisha ukweli huu.
Niruhusuni nichukue muda wenu kidogo nizungumzie baadhi ya mambo
yahusuyo shughuli za Serikali.
Nchi Iko Salama
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuanza kwa kuwahakikishia kuwa Tanzania iko salama pamoja na
kuwepo matukio ya hapa na pale. Mipaka yetu iko salama. Hakuna tishio
lo lote la kiusalama la kutufanya tuhamanike. Hata mpaka wetu na Malawi
uko salama pamoja na kuwepo kwa maneno maneno yahusuyo nchi zetu mbili
kutofautiana wapi ulipo mpaka halali. Hakuna jambo lo lote linalofanywa
upande wa wenzetu ambalo linatufanya tuwe na mashaka ya usalama wa nchi
yetu kuwa hatarini. Kwa sababu hiyo hatujaiona haja ya kusogeza
Majeshi yetu mpakani na anayesema tumefanya hivyo ni muongo. Apuuzwe na
kushushuliwa.
Ndugu Wajumbe;
Tumeendelea na juhudi za kuimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania kwa kuwajengea uwezo, zana na vifaa vya kisasa vya kivita.
Lengo letu ni kukuza nguvu ya kimapigano ya Jeshi letu na kuimarisha
utayari wake kivita. Hali kadhalika, tumeendelea kuboresha maslahi ya
wanajeshi na mazingira yao ya kufanyia kazi na ya kuishi. Kwa upande wa
usalama wa raia, yaani maisha na mali zao, matukio ya uhalifu
yanaendelea kupungua. Hali hii inaashiria kuwa Jeshi la Polisi
linafanya kazi nzuri. Kama tufanyavyo kwa JWTZ, tutaendeleza juhudi za
kuimarisha Jeshi la Polisi kwa watu, zana na vifaa vya kisasa vya
kufanyia kazi. Tutaendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kufanyia
kazi na ya kuishi ya Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama.
Ndugu Wajumbe;
Pamoja na kutokuwepo kwa tishio lililo dhahiri la shambulio la
kigaidi, wakati wote vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko katika
hali ya tahadhari kuepuka kushtukizwa. Kama mnavyokumbuka mwaka 1998
Ubalozi wa Marekani hapa nchini ulishambuliwa na ndugu zetu 11
walipoteza maisha. Hivyo basi, kuchukua tahadhari ni jambo la busara
kufanya. Aidha, tuko katika hali ya tahadhari dhidi ya uharamia wa
kuteka meli katika Bahari Kuu ya Hindi. Takriban mwaka mzima umepita
bila ya matukio ya kutekwa nyara meli katika bahari yetu . Hata hivyo
hatuachi kuchukua tahadhari.
Ndugu Wajumbe;
Matukio ya hivi karibuni ya vurugu zenye mwelekeo wa kidini
yanasikitisha na kusononesha. Ni mambo ambayo hayafanani na sifa ya
nchi yetu ya kuheshimiana na kuvumiliana pamoja na kuwepo tofauti zetu
za dini, kabila rangi au maeneo tutokako. Vitendo hivyo havikubaliki na
Serikali haitawavumilia au kuwaonea muhali wale wote wanaohusika na
kuchochea vurugu hizo. Tumechukua hatua na tutaendelea kuchukua hatua
bila ya ajizi. Ombi langu na wito wangu kwa viongozi na wafuasi wa dini
nchini kuhubiri dini zao huku wakitambua na kuzingatia umuhimu wa
kuheshimu imani za wengine na kuvumiliana. Tusipofanya hivyo nchi yetu
tutaingiza kwenye matatizo yasiyostahili kuwepo.
Ndugu Wajumbe;
Inatia moyo kuona kuwa watu wenye nia njema na nchi yao ni wengi.
Kwa sababu hiyo pamoja na jitihada za baadhi ya watu wasiyoitakia mema
nchi yetu hawajafanikiwa kuwagawa na kuwafarakanisha Watanzania.
Nawaomba Watanzania wenzangu tuwe na moyo huo huo na sisi katika
Serikali tutaendelea kumchukulia hatua mtu ye yote anayetaka kutuvurugia
amani na utulivu wa nchi yetu na watu wake.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali haitamuonea mtu ye yote
asiyehusika. Tutaendelea kuidumisha sifa yetu ya kuendeleza utawala
bora, kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia utawala wa sheria.
Kadhalika tutaendelea kuheshimu mgawano wa madaraka miongoni mwa
mihimili mikuu ya dola. Nafurahi kwamba mpaka sasa mambo yanakwenda
vizuri.
Muungano Imara
Ndugu Wajumbe;
Muungano wetu ni imara pamoja na kuwepo vitendo vyenye lengo la
kuudhoofisha vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa siasa na wa dini
hasa kule Zanzibar. Jambo linalosikitisha ni watu hao kutumia njia za
vitisho na ghasia ili kuwalazimisha watu kuwaunga mkono. Njia hizo
hazikubaliki na wala hazitavumiliwa.
Inastaajabisha mambo hayo kufanyika hivi sasa wakati kuna Tume ya
Katiba. Kama mtu ana maoni yo yote kuhusu Muungano ayafikishe tu,
yatapokelewa na kupimwa. Vile vile Kamati ya Pamoja ya Serikali zote
mbili inayowakutanisha Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
imekuwa inafanya kazi nzuri kutatua kero za Muungano. Kama mtu analo
jambo analotaka lipatiwe jawabu awasilishe kwa wahusika
litashughulikiwa.
Hali ya Uchumi
Ndugu Wajumbe;
Katika Mkutano Mkuu Maalum wa Julai, 2010 hapa Kizota, nilielezea
mafanikio tuliyoyapata na changamoto tulizokumbana nazo katika kukuza
uchumi wa nchi yetu na kupunguza umasikini. Nilieleza pia nia yetu ya
kuendelea kupambana na changamoto zilizokuwa mbele yetu pamoja na ugumu
unaotokana na hali ya kuyumba kwa uchumi wa dunia ambamo na sisi pia
tumo. Kwa ajili hiyo mwaka 2011 tulizindua Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano(2011/12 – 2015/16).
Mpango huu ni wa kwanza kati ya mitatu katika safari yetu ya
kutekeleza Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025. Kwa mujibu wa Dira yetu
hiyo, tunatarajia ifikapo mwaka 2025 nchi yetu itaondoka katika kundi la
nchi maskini sana duniani na kuwa nchi ya uchumi wa kati. Yaani
tunataka pato la wastani la Watanzania litoke kwenye dola za Kimarekani 545 za sasa hadi kufikia dola za Kimarekani 3,000.
Lengo hilo ni kubwa linalohitaji mipango thabiti na uwekezaji makini wa
Serikali na sekta binafsi. Pia inahitaji kuwepo kwa nidhamu ya dhati
ya viongozi na wananchi wa Tanzania.
Ndugu Wajumbe;
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo umekwishaanza. Lengo la jumla katika Mpango wa kwanza ni Kufungulia fursa kwa ukuaji wa uchumi; wa pili ni Ujenzi wa mazingira ya maendeleo ya viwanda; na wa tatu ni Kuimarisha ubunifu na ushindani kimataifa.
Tayari miradi ya kimkakati imekwishaainishwa na inapewa kipaumbele
katika bajeti ya Serikali na ubia baina ya sekta binafsi na sekta ya
umma. Katika kila hatua suala la kukuza ajira limepewa umuhimu mkubwa
kwani lengo letu ni kuwa na ukuaji wa uchumi unaojumuisha maisha ya
watu. Vijana ni walengwa wakubwa.
Mwelekeo wa uchumi wetu ni mzuri. Kasi ya ukuaji wa uchumi iliyokuwa
asilimia 6.4 mwaka wa jana inatarajiwa kufikia asilimia 7 mwaka huu.
Mauzo yetu ya nje yanazidi kukua na kuongezeka. Kwa mfano mwaka 2005
ilikuwa dola za Kimarekani milioni 2,945.5 na sasa ni milioni 7,461.2. Akiba yetu ya fedha ya kigeni nayo ni nzuri. Hivi sasa ni dola za Kimarekani bilioni 4.1 inatuwezesha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa miezi 3.8.
Ndugu Wajumbe;
Changamoto kubwa katika uchumi ni mfumuko wa bei. Ni kweli umepungua
kutoka asilimia 19.8 Desemba, 2011 hadi asilimia 13.5 Septemba, 2012,
hata hivyo kupungua huko ni kidogo mno. Tunaendelea kuchukua hatua za
kudhibiti na kupunguza zaidi mfumuko wa bei. Kwa vile moja ya sababu ni
kupanda kwa bei za mafuta. Tumeipa dhamana EWURA kusimamia kwa karibu
uagizaji na upangaji wa bei ya mafuta.
Kwa kuwa bei za vyakula hasa mchele na sukari navyo huchangia kupanda
kwa mfumuko wa bei na kuongeza gharama ya maisha mamlaka husika
zimeagizwa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanawezeshwa kuagiza bidhaa
hizo kwa wingi kutoka kwa nje kwa kuwapatia nafuu ya baadhi ya kodi.
Pamoja na hayo jawabu la kudumu lipo katika kuendeleza mageuzi ya kilimo
ili nchi yetu ijitosheleze kwa chakula na kupata ziada kubwa ya kuuza
nje. Hayo ndiyo malengo na hatua zinazochukuliwa katika ASDP, Kilimo
Kwanza na SAGCOT. Ndiyo maana tutaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo kwa
wakulima, kuimarisha masoko na miundombinu vijijini.
Mapato na Matumizi ya Serikali
Ndugu Wajumbe,
Tunazidi kupata mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa ukusanyaji wa
mapato ya Serikali. Makusanyo ya mapato ya kodi Mwezi Agosti 2012, kwa
mfano, yalifikia shilingi bilioni 554.8 ikilinganishwa
na makusanyo ya shilingi bilioni 147 mwezi Desemba 2005. Mafanikio haya
yametokana na juhudi za dhati za Serikali katika kusimamia mabadiliko
ya sera na kuimarisha mifumo na taasisi za ukusanyaji wa mapato ya kodi
na mengineyo.
Kwa sababu ya kuongezeka huko kwa mapato, bajeti ya Serikali nayo imeongezeka kutoka shilingi trilioni 4.13 mwaka 2005/06 hadi shilingi trilioni 15.12 mwaka huu. Jambo linaloleta faraja ni kuwa mchango wa Serikali kutokana na bajeti hiyo nao umeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.1 mwaka 2005 hadi trilioni 8.8 mwaka huu. Utegemezi wa wahisani nao unaendelea kupungua kutoka asilimia 44 mwaka 2005/6 hadi 21.
Ndugu Wajumbe;
Sambamba na kuongeza mapato, nidhamu, udhibiti wa matumizi ya fedha
na mali za umma vinazidi kuimarika. Hii ni kutokana na kuimarika kwa
mifumo na kada ya uhasibu katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Pia
ni matokeo ya kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma.
Hati Chafu katika idara za Serikali zinaendelea kupungua katika taarifa
ya ukaguzi kila mwaka. Hivi sasa tunaelekeza nguvu zetu katika kuhakiki
thamani ya fedha zilizotumika na kazi iliyofanyika au huduma
iliyotolewa.
Uwekezaji
Ndugu Wajumbe,
Serikali imechukua hatua kadhaa kuboresha mazingira ya uwekezaji na
ya kufanya biashara hapa nchini. Lengo letu ni kuvutia wawekezaji wa
ndani na nje kuongeza vitega uchumi nchini na kupanua biashara ndani ya
nchi na kati ya nchi yetu na nchi nyingine duniani. Tunafanya hayo kwa
kutambua ukweli kwamba uchumi unakua na kuongezeka pale ambapo uwekezaji
unaongezeka. Takwimu zinaonyesha kwamba uwekezaji umekuwa ukiongezeka
mwaka hadi mwaka katika sekta ya utalii, viwanda, kilimo, madini, fedha,
ujenzi na sasa kwenye utafutaji wa gesi na mafuta. Tumepata
mafanikio makubwa katika utafutaji wa gesi na nchi yetu itakuwa moja ya
mzalishaji mkubwa wa gesi. Mwaka 2011, kwa mfano, kulikuwa na jumla ya
miradi 826 yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 7,177 itakayozalisha ajira ya watu 79,000. Haya ni mafanikio madogo lakini tunaweza kufanya vizuri zaidi.
Tutaendelea kutumia fursa ya kijiografia ya nchi yetu kuvutia
uwekezaji na kuifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara na
usafirishaji kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati. Ili kufanikisha
hayo, tutaendelea kuboresha miundombinu ya barabara, reli, bandari,
viwanja vya ndege na teknohama.
Miundombinu
Ndugu wajumbe;
Moja ya vipaumbele vya juu vya Serikali ya CCM ninayoiongoza ni
kuboresha miundombinu ya usafiri wa ardhini, majini na angani nchini.
Tumethibitisha hayo kwa mgao wa fedha za bajeti ya Serikali ambapo
miundombinu ni ya pili baada ya elimu. Mwaka huu ni shilingi trilioni 2.4, ambayo ni asilimia 16 ya bajeti ya Serikali ukilinganisha na elimu yenye trilioni 3.6 ambayo ni sawa na asilimia 24, na afya yenye shilingi trilioni 1.5 sawa na asilimia 10
ya bajeti ya Serikali. Tunafanya hivyo kwa kutambua mchango muhimu wa
sekta ya usafiri kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Usafiri
unapokuwa bora na wa uhakika, gharama za usafirishaji zinapungua,
shughuli za uzalishaji viwandani na kilimo zinaimarika. Ni kichocheo
kikubwa cha kuibuka kwa fursa mbalimbali za uchumi na kuongeza kasi ya
maendeleo na kukuza kipato cha Watanzania waliopo mijini na vijijini.
Ndugu Wajumbe;
Tunafanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa barabara kuliko wakati
mwingine wo wote katika historia ya nchi yetu. Hivi sasa barabara
zenye urefu wa kilometa 11,154 zinajengwa kwa kiwango
cha lami katika sehemu mbalimbali nchini. Tulijipa lengo la kuunganisha
mikoa yote kwa barabara za lami na barabara zote kuu ziwe za lami.
Nafurahi kusema kuwa utekelezaji wake unakwenda vizuri. Tumeanza
kufanikiwa kuifikia ile mikoa ambayo kwa muda mrefu ilikuwa haifikiki
kwa urahisi kwa kukosa barabara za lami. Katika hotuba yangu ya tarehe
25 Juni, 2006 niliwaambia Wajumbe wa Mikoa ya Ruvuma, Rukwa, Mtwara,
Kigoma na Tabora kuwa kilio chao tumekisikia. Niliahidi kuwa ujenzi wa
barabara katika Mikoa hiyo tutaipa kipaumbele. Tumetimiza ahadi hiyo na
kazi inaendelea kwa kasi na hata wenyewe ni mashahidi. Karibu
tunafikia ndoto yetu ya kwamba hakuna mkoa utakaoachwa nyuma.
Ndugu Wajumbe;
Inafurahisha zaidi kuona kuwa zaidi ya asilimia 60
ya gharama za ujenzi wa barabara tunazojenga nchini ni fedha zetu
wenyewe. Aidha, uwezo wa Mfuko wa Barabara (Road Fund) nao
umeongezeka sana kutoka shilingi bilioni 58 mwaka 2005 hadi shillingi bilioni 430.
Hali hiyo imeongeza uwezo wetu wa kujenga na kukarabati barabara
mbalimbali nchini. Kwa ajili hiyo tumeongeza bajeti ya barabara kwenye
Halmashauri zote nchini.
Ndugu Wajumbe;
Pamoja na barabara, tunaendelea kuimarisha viwanja vya ndege, bandari
na usafiri wa reli. Changamoto mbalimbali zinajitokeza katika
utekelezaji wa lengo letu na kubwa zaidi ikiwa ni ile ya gharama za
ujenzi na ukarabati wa miundombinu kuwa kubwa mno ikilinganishwa na
uwezo wetu. Tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuzikabili changamoto
hizo hatua kwa hatua na tunazipunguza.
Elimu
Ndugu wajumbe;
Tumefanikiwa kupanua sana fursa za kuwapatia elimu vijana wetu katika
ngazi zote. Kuna watoto wengi katika elimu ya awali, na kwa elimu ya
msingi asilimia 97 ya watoto wenye umri wa kwenda shule wamejiandikisha. Kwa kiwango hicho, tuko mahali pazuri kufikia asilimia 100
ifikapo mwaka 2015 kama ilvyoagiwa katika Malengo ya Milenia ya Umoja
wa Mataifa. Kuhusu elimu ya Sekondari, wananchi na wadau wengine
wameitikia wito wa Serikali wa kila Kata kuwa na shule ya sekondari. Kwa
sababu hiyo idadi ya shule 3,165 zimejengwa kati ya 2005 na hivi sasa na idadi ya wanafunzi katika shule za sekondari imeongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,884,272 mwaka huu.
Tumepanua sana mafunzo ya ufundi na elimu ya juu. Hivi sasa nchi yetu ina vyuo vikuu 27 na wanafunzi waliopo vyuoni humo ni zaidi ya 166,484 ikilinganishwa na 40,719
wa mwaka 2005. Ili kutoa fursa sawa kwa wanafunzi wote tumeongeza sana
uwezo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili iwape wanafunzi wengi
mikopo ya elimu. Bajeti ya Bodi hiyo imeongezeka kutoka shilingi
bilioni 56.1 mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 306.0 mwaka huu. Wanafunzi wanaopata mikopo wapo 93,176 ukilinganisha na 16,345 mwaka 2005. Tutaendelea kuongeza fedha ili tuwafikie wanafunzi wengi kadri inavyowezekana.
Ndugu Wajumbe;
Upanuzi mkubwa wa elimu katika ngazi zote nchini umezua changamoto
mbalimbali kuhusu ubora wa elimu. Tunazitambua changamoto hizo kuwa ni
pamoja na zile za upungufu wa walimu, hususan wa sayansi; upungufu wa
vifaa vya maabara, vitabu na nyumba za walimu hasa kwenye maeneo ya
vijijini. Tumejipanga vyema kuzitafutia ufumbuzi na tumeanza kufanya
hivyo. Tumeongeza vyuo vinavyotoa mafunzo ya ualimu ili kuongeza idadi
ya waalimu. Bajeti ya elimu ni kubwa kuliko zote ili kusaidia kutatua
tatizo la upungufu wa vitabu, maabara, vifaa vya kufundishia na nyumba
za walimu na mahitaji mengineyo. Hivi karibuni nilipokuwa Mkoani
Singida nimewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kuhakikisha
kuwa shule zote za sekondari katika maeneo yao zinakuwa na maabara ya
sayansi katika miaka miwili ijayo.
Afya
Ndugu wajumbe;
Suala la afya ya Watanzania tunalipa umuhimu mkubwa sana. Tumeongeza bajeti ya afya kutoka shilingi bilioni 271 mwaka 2005 hadi shilingi trilioni 1.5
mwaka huu. Nyongeza hii ndiyo iliyotuwezesha kutekeleza Sera mpya ya
Afya (2007) na Mpango wa Miaka Kumi wa Maendeleo ya Afya ya Msingi
(MMAM) wa kuitekeleza vyema Sera hiyo. Lengo kuu la sera na MMAM ni
kuwapatia Watanzania huduma ya afya iliyo bora katika umbali usiozidi
kilometa tano. Vile vile, ni kuimarisha huduma zinazotolewa katika
hospitali za Wilaya, Mikoa, Kanda na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katika mpango huu pia tumeazimia kukabili tatizo la upungufu wa
madaktari, wauguzi na wataalamu wengi. Tunaendelea kupanua mafunzo ya
wataalamu hao katika vyuo vyetu hapa nchini na hata nje ya nchi.
Tumejenga na tutaendelea kujenga vyuo vipya, wakati huo huo tukipanua
vilivyopo. Tumeendelea kujenga uwezo wa kupambana na maradhi makubwa
yanayoua watu wengi. Tumeelekeza nguvu zetu kwenye maradhi
yanayoambukiza kama vile malaria, UKIMWI na kifua kikuu na yale
yasiyoambukiza kama vile saratani, moyo, shinikizo la damu na vifo vya
kina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Ndugu Wajumbe;
Kwa maradhi yote mafanikio ya dhahiri yanaendelea kupatikana. Maambukizi ya virusi vya UKIMWI yanapungua kutoka asilimia 8 hadi asilimia 5.7, vifo kutokana na malaria vimepungua kwa asilimia 40
kwa Tanzania Bara na kwa Zanzibar tunakaribia kutangaza kufutika kwa
maradhi hayo. Tumepanua uwezo wa kutibu maradhi ya moyo ikiwa ni pamoja
na kufanya upasuaji wa moyo. Tumepanua uwezo wa kuchunguza na kutibu
maradhi ya kansa. Tunaendelea kujenga uwezo wa ndani kwa maradhi
tunayopeleka wagonjwa wengi nje na mafanikio yanaaza kuonekana. Safari
ni hatua, naamini tutafika kwani mwelekeo wetu ni mzuri.
Umeme na Maji
Ndugu wajumbe;
Tunaendelea kupanua uwezo wetu wa kuzalisha na kusambaza umeme
nchini. Tumeanza safari ya uhakika ya kupunguza kutegemea mno umeme wa
nguvu ya maji. Tunapanua umeme utokanao na vyanzo vingine hasa gesi
asilia na makaa ya mawe. Mipango ya kutumia upepo na mionzi ya jua nayo
iko mbioni. Pamoja na hayo tunayo mikakati ya kupunguza umeme
unaozalishwa kwa kutumia mafuta kwa kubadili mitambo hiyo iweze kutumia
gesi asilia.
Hivi majuzi tu nilizindua ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi
Dar es Salaam. Litakapokamilika nchi yetu itakuwa na uwezo wa kuzalisha
megawati 3,000 na kuung’oa mzizi wa fitina wa mgao na
upungufu wa umeme nchini. Tumeendelea kuwekeza katika usambazaji wa
umeme nchini jambo ambalo limetuwezesha kuwapatia umeme kwa asilimia 18.4 Watanzania kutoka asilimia 10 mwaka 2005. Kwa kasi hii naamini tutafikia lengo la asilimia 30 ifikapo 2015.
Kwa upande wa maji, jitihada za kuwapatia wananchi maji safi na
salama zinaendelea vizuri. Eneo hili lina changamoto kuu mbili. Kwanza
ni ule ukweli kwamba kuna baadhi ya maeneo ya nchi yetu hayana vyanzo
vya maji karibu au hayapati mvua za kutosha au yana ukame. Katika maeneo
ya aina hii upatikanaji wa maji huwa wa shida sana na hivyo
kutulazimisha kujenga miradi ya maji ya bomba kutoka masafa marefu.
Changamoto yetu ya pili ni ule uwezo mdogo wa kifedha kwa miradi mingi
inayohitaji pesa nyingi. Mwaka 2006 tulianzisha Programu ya Maendeleo
ya Sekta ya Maji. Kufuatia utekelezaji ulio makini wa programu ya sekta ya maji, asilimia 60 ya watu wa vijijini na asilimia 86 ya watu wa mijini wanaopata maji safi na salama. Ni matumaini yangu kuwa tutafikia lengo letu la asilimia 65 la upatikanaji maji kwa vijijini na asilimia 90
kwa mijini ifikapo 2015. Bahati nzuri tunayo miradi ya maji
inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini na
itapokamilika tutafikia lengo letu au hata kulivuka.
Pongezi kwa Kuchaguliwa
Ndugu Wajumbe;
Katika Mkutano huu, Ndugu Amani Abeid Karume, Makamu Mwenyekiti wa
Zanzibar na Ndugu Pius Msekwa, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa
Tanzania Bara watastaafu. Ndiyo maana NEC imeamua kuwapendekeza kwenu
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi na Ndugu Philip Mangula kuchukua nafasi zao. Napenda kuchukua
nafasi hii kwashukuru kwa dhati Rais Amani Abeid Karume na Mzee Msekwa
kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya kunisaidia kuongoza Chama chetu.
Wamekifanyia Chama chetu mambo mengi mazuri ambayo hatuna budi
kuwapongeza na kuwashukuru. Waliendelea kuwa walimu wangu na washauri
wangu kwa mambo mengi ya Chama na nchi. Nawashukuru sana. Sote
tuwatakie afya njema na maisha marefu. Na tumuombe Mzee Msekwa asichoke
kuandika vitabu ili hazina yake kubwa ya uzoefu na maarifa iwanufaishe
wengi kwa miaka mingi ijayo.
Kwa viongozi wa Mikoa, Wilaya na Jumuiya pamoja na Wajumbe, nirudie
kuwapongeza nyote kwa kuchaguliwa kwenu. Poleni kwa magumu ya uchaguzi
mliyokumbana nayo. Sasa uchaguzi umeisha, fanyeni kazi ya kujenga
Chama. Tibuni majeraha ya uchaguzi na hasa fanyeni kila muwezalo kuziba
nyufa za uchaguzi na migawanyiko miongoni mwa wanachama na viongozi.
Kumbukeni wosia wa Baba wa Taifa “Umoja ni Nguvu” Kumbukeni kaulimbiu ya Mkutano wetu huu ya Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi! Kajengeni umoja katika maeneo yenu ya uongozi kwa maslahi ya Chama chetu na nchi yetu.
Hitimisho
Ndugu Wana-CCM;
Kwa kuhitimisha naomba nirudie kusema kuwa tumepata mafanikio ya
kutia moyo katika ujenzi wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
CCM ya mwaka 2010 – 2015. Bado kazi kubwa iko mbele yetu kwa mambo
yote hayo mawili. Tunaitambua na tunayo mipango thabiti ya kutekeleza
majukumu yetu. Nina imani tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kufikia
malengo yetu. Tukiendelea kushirikiana tutafika. Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi!
Baada ya hotuba yangu naomba sasa nitamke kuwa Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM umefunguliwa rasmi.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Kidumu Chama cha Mapinduzi
Asanteni sana kwa Kunisikiliza
No comments:
Post a Comment