HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » MKURUGENZI MTENDAJI WA TANESCO MHANDISI WILLIAM MHANDO AFUKUZWA KAZI RASMI

Taarifa kwa Umma iliyotolewa 30/10/2012

 
 TAARIFA YA KUACHISHWA KAZI MKURUGENZI MTENDAJI WA TANESCO KWA KINA ZAIDI
  Mhandisi, William Geofrey Mhando

BODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), imemwachisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Mhandisi William Mhando. Taarifa ya kuachishwa kazi kiongozi huyo, imetolewa jana kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Jenerali Robert Mboma.

“Kutokana na tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa taratibu za shirika, ikiwamo matumizi mabaya ya mamlaka, mnamo tarehe 16 Julai 2012, Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, iliamua kumsimamisha kazi pamoja na maofisa wengine waandamizi, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, William Mhando kwa nia ya kupisha uchunguzi huru na wa haki, ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo.

“Baada ya hapo, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, ilifanya uchunguzi, ili kubaini ukweli juu ya tuhuma zilizokuwa zinamkabili Mhandisi William Mhando.

“Baada ya uchunguzi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, aligundua kuwepo kwa ushahidi dhahiri wa ukiukwaji wa taratibu za shirika na matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi William Mhando.

“Aidha, baada ya kupokea taarifa hiyo, bodi iliteua jopo la watu watatu, kusikiliza utetezi wa Mhandisi William Mhando, dhidi ya tuhuma zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

“Baada ya kumsikiliza, jopo hilo lilimkuta Mhandisi William Mhando na hatia dhidi ya makosa yanayohusiana na ukiukwaji wa taratibu za shirika, ikiwamo mgongano wa kimaslahi.

“Pamoja na yote yaliyoelekezwa hapo juu, Oktoba 29 mwaka huu, bodi ilikutana na kujiridhisha kuwa, Mhandisi William Mhando, alifanya makosa yanayohusiana na kuingia kwenye mikataba yenye mgongano wa kimaslahi kinyume na taratibu za shirika.

“Hivyo basi, kufuatia makosa hayo, Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, iliamua kumwachisha kazi Mhandisi William Mhando, kuanzia Oktoba 29 mwaka huu,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Pamoja na Bodi ya TANESCO kuchukua hatua hiyo, wakati wa Bunge la Bajeti lililomalizika Agosti mwaka huu, Bunge lilirindima wakati lilipokuwa likijadili mwenendo wa shirika hilo.

Katika michango ya wabunge mbalimbali, walionyesha kutoridhishwa na mwenendo wa shirika hilo, kwa kile walichoeleza kuwa, Mhando alikuwa akitumia madaraka yake vibaya katika kuliendesha shirika hilo.

Miongoni mwa tuhuma zilizoelekezwa kwake, ni jinsi alivyofanikiwa kujipatia mamilioni ya fedha, kupitia kampuni yake aliyoianzisha yeye na mkewe na kuanza kuliuzia shirika vifaa vya ofisini, huku akijua kuwa anakiuka sheria za utumishi wa umma.

Vile vile, wakati wa utawala wa mkurugenzi huyo, kuna boksi la misumari liliagizwa kutoka nchini Uingereza na kuingizwa nchini, kisha likalipiwa mamilioni ya shilingi kinyume cha sheria.

Pamoja na hayo, wakati Mhando akiliongoza shirika hilo, nguzo za umeme zilizokuwa zikikatwa katika misitu iliyoko Iringa, ilikuwa ikinunuliwa na TANESCO kwa gharama kubwa, kwa madai kuwa ilikuwa ikiagizwa kutoka nje ya nchi.

Katika kutekeleza ulaji huo, nguzo hizo baada ya kukatwa katika misitu ya hapa nchini, ilikuwa ikigongwa mihuri ikionyesha kuwa, ilikuwa ikiagizwa kutoka nchini Afrika Kusini, kupitia Mombasa nchini Kenya.

Julai 14, mwaka huu Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO ilimsimaisha kazi Mhando kwa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Mbali na Mhando, wengine waliosimamishwa kazi ni pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga, na Meneja Mwandamizi Ununuzi, Harun Mattambo.

Taarifa hiyo ilisema Bodi ya Wakurugenzi ya TANECSO ilikutana katika kikao cha dharula Julai 13, mwaka huu, kujadili masuala mbalimbali ikiwamo tuhuma zinazoelekezwa dhidi ya menejimenti ya shirika hilo.

Kikao hicho cha Julai 13, mwaka huu ilikutana kwa dharula na kuweza kujadili masuala mbalimbali ikiwamo tuhuma zinazoelekezwa dhidi ya Menejimenti ya TANESCO.

Tuhuma hizo ni pamoja na ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka, ambapo katika majadiliano marefu bodo hiyo ya TANESCO iliona ni nzito na kuamua kuzifanyia kazi kwa kufanya uchunguzi wa haraka.

Pamoja na hayo bodi iliazimia kufanyika kwa uchunguzi wa tuhuma hizo kuanza mara moja kwa kutumia mchunguzi huru sambamba na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi William Mhando ili kupisha uchunguzi huo na kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kazi nchini.

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: