HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » Noti za zamani zachanganya wananchi

 
MATUMIZI ya noti mpya na za zamani katika mzunguko kwa karibu miaka miwili sasa, yanatajwa kuwa kashfa nyingine kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), baada ya ile ya wizi uliofanyika katika Akaunti ya Madeni ya Nje, (EPA).

Baada ya BoT kuzindua noti mpya za Sh1,000, 2,000, 5,000 na 10,000 Januari 2011, Gavana Benno Ndullu alitangaza kuwa noti za zamani zenye thamani sawa na hizo, zingeondolewa kwenye mzunguko ndani ya kipindi cha miezi sita, ahadi ambayo mpaka sasa haijatekelezwa.

Akizungumzia hali hiyo mwanzoni mwa wiki, Gavana Ndullu alisema, hawezi kusema lini noti za zamani zitakwisha matumizi yake kwa kuwa hili litategemea kumalizika kwa noti hizo kwenye mzunguko.

Tangu noti mpya zilipoingia katika mzunguko, taifa limekuwa likitumia noti za aina mbili kwa pamoja, kitendo ambacho kimezua mjadala, huku baadhi ya watu wakieleza kuwa kinahatarisha uchumi wa taifa.

Watu wa kada mbalimbali waliozungumza na gazeti hili wameitupia lawama BoT, wakisema imeshindwa kuweka usimamizi mzuri wa fedha ama kwa makusudi au uzembe, hivyo kutoa fursa kwa watu wasio waaminifu kuingiza fedha chafu kwenye mzunguko.

“Biashara ya noti bandia inaonekana kama halali…, wanasema ukipeleka Sh100,000 unauziwa noti bandia za Sh200,000 namna ya kuzibadilisha utajua mwenyewe,” alieleza meneja wa benki moja mjini Moshi, ambaye hakutaka atajwe gazetini.

Kwa nyakati tofauti maofisa wengine wa benki kutoka mikoa ya Dare es Salaam, Mbeya, Arusha, Mwanza na Kilimanjaro, walidokeza kuwa noti za zamani ni bora ikilinganishwa na noti mpya.

Mbali na kuchakaa haraka, maofisa hao wamesema noti mpya ni rahisi kughushiwa na maeneo salama ya kuzipeleka fedha hizo ni vijijini.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema kimsingi hakuna athari zozote kiuchumi kama nchi itaendelea kutumia noti mbili zenye thamani moja, lakini hii inatoa mwanya wa kusambaa noti bandia kwenye mzunguko wa fedha.
“Kama moja ya noti hizo zinaghushika kirahisi, watu wataghushi na kuziingiza kwenye mzunguko. Huu ni udhaifu wa Benki Kuu katika kusimamia suala hilo. Fedha hizo zinatakiwa zifike benki na zikienda huko, zisitolewe tena kwa wananchi,” alisema.
“Kuna uwezekano noti hizo kutokubalika kwenye baadhi ya maeneo,” alisema.
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi katika Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Moris Oyuke pamoja na kusema kuwa kutumika kwa noti tofauti zenye thamani moja hakuna madhara kiuchumi, alisisitiza kuwa hali hiyo inapaswa kudhibitiwa.

“Kama BoT inapata Sh10,000 iliyochakaa na kuiharibu, kisha kutoa Sh10,000 mpya, hapo hakuna madhara. Tatizo linakuja kama BoT itaharibu kiasi kidogo cha fedha na kuingiza katika mzunguko fedha nyingi zaidi, hii italeta mfumko wa bei,” alisema.

Mkuu wa Idara ya Fedha katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Esther Ishengoma alisema kuwa kuwepo kwa noti mbili katika mzunguko kunaleta mkanganyiko katika jamii.

Dk Ishengoma alibainisha kuwa noti za zamani ni ubora zaidi ya noti mpya na inawezekana Serikali imeliona hilo ndiyo maana inashindwa kuziondoa katika mzunguko.

“Noti za zamani zinaonekana kuwa na ubora wa juu kuliko zile mpya hii inaweza kuwa sababu ya Serikali kushindwa kuziondoa kwenye mzunguko,” alifafanua Dk Ishengoma.
Kwa upande wake, Dk Ulingeta Mbamba ambaye ni Mkuu wa Shule ya Biashara katika chuo hicho, alisema licha ya ubora hafifu, noti mpya zinatambulika kwa urahisi zaidi katika mashine za kuhesabia fedha.


“Ninachoweza kusema ni kuwa mashine za kuhesabia fedha hutambua kwa urahisi noti bandia za noti mpya kuliko zile za noti za zamani, hii inasaidia kupunguza noti bandia ambazo huathiri uchumi wa nchi,” alieleza Dk Mbamba.

Mhadhiri mwingine katika idara ya Uchumi chuoni hapo, Jehovaness Aikael alisema kuwa hakuna athari zozote katika uchumi kwa sababu zote zina thamani.

“Serikali inafanya kila kitu kwa lengo la kuwapa wananchi kile kilicho bora. Sasa suala hili tutalishughulikia ili kuondoa usumbufu ambao umejitokeza,”alisema waziri huyo.
Hata hivyo, Gavana Ndullu alibainisha kuwa noti za zamani zinazoonekana kuwa mpya sasa hazitolewi na benki, ziko kwa wananchi.

“Hizi mnazoziona mpya ni wananchi walikuwa nazo na hatuwezi kwenda kuwaambia wazee huko vijijini leteni noti zenu tuwape mpya. Kinachofanyika zikishafika Benki Kuu hatuzirudshi tena kwenye mzunguko,” alisema Profesa Ndullu.
Habari hii imeandikwa na Godfrey Kahango, Mbeya, Daniel Mjema, Moshi, Raymond Kaminyoge.

CHANZO: MWANANCHI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: