Vurugu kubwa zimeibuka katika Jiji la Mwanza kati ya wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu wamachinga na mgambo wa jiji hilo na kusababisha mtu mmoja kupoteza maisha kwa kupigwa risasi.
Aidha, Polisi jijini Mwanza wameua watu watatu wanaodaiwa kuwa ni majambazi katika tukio la kurushiana risasi.
Mtu huyo aliyeuwawa kwa kupigwa risasi amefanya jumla ya idadi ya watu waliuwawa mkoani hapa katika matukio tofauti kufikia wanne.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza, Lily Matola, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema katika tukio la vurugu za mgambo na wamachinga, mbali na kifo hicho watu wawili wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi.
Alisema katika tukio hilo ambalo lilitokea jana, aliyeuawa ni mpigadebe mmoja ambaye jina lake wala makazi yake havijatambuliwa.
Kamanda Matola alisema katika vurugu hizo, wamachinga wawili walijeruhiwa kwa kupigwa risasi na wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Alisema vurugu hizo ziliibuka jana kati ya saa 5 :00 asubuhi na 6:00 mchana muda mfupi baada ya mgambo wa mgambo hao walipokwenda eneo hilo kwa ajili ya kuendesha operesheni ya kuwaondoa wamachinga katika maeneo yasiyoruhusiwa kufanyabiashara na ndipo kukazuka mapigano.
Kamanda Matola alisema mgambo hao wakiwa eneo hilo wamachinga walianza kuwarushia mawe na katika kujiokoa, mgambo hao walianza kupiga risasi hewani na risasi moja ilimpata mpigadebe ambaye alifariki papo hapo.
Aliongeza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Kamanda Matola alisema kufuatia vurugu hizo, polisi wanawashikilia mgambo watatu huku wenzao wawili wakiwa wamejeruhiwa vibaya na wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Katika tukio lingine, watu watatu wanaosadikiwa kuwa majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Big Bite lililopo Kilimahewa, Wilaya ya Ilemela jijini hapa.
Kwa mujibu wa Kamanda Matola, watuhumiwa hao ambao hadi sasa bado majina yao hayajatambuliwa, waliuawa kwa kupigwa risasi, kati ya majira ya saa 4:00 na saa 5:00 juzi usiku.
Kamanda Matola alisema polisi waliokuwa katika doria, ghafla baada ya kuwashtuakia, kulizuka mapambano ya kurushia risasi kati ya majambazi hao na polisi.
Alisema majambazi hao walikuwa na bunduki aina ya SMG yenye namba za usajili T1964TB8799 ikiwa na risasi 43.
Kamanda Matola alisema wakati wa mapambano hayo, hakuna askari aliyejeruhiwa.
Alisema miili ya majambazi hayo imehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo.



No comments:
Post a Comment