HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » Rais Jakaya Kikwete: Uhuru wa Dini Siyo Hati ya Kufanya Fujo

 
Rais Jakaya Kikwete














RAIS Jakaya Kikwete, amesema uhuru wa kisiasa na wa kuabudu unaotolewa na Katiba na kujengeka chini ya uongozi wake, siyo uhuru wa kuvunja amani. Pia Rais Kikwete ametangaza kwamba, Serikali yake inajenga kiasi cha nyumba 10,000, kwa ajili ya wanajeshi ili kuwezesha kuishi katika nyumba nzuri na za kisasa.
Rais Kikwete ameyasema hayo juzi wakati alipozungumza na wapiganaji na maofisa wa Chuo cha Jeshi cha Monduli, wakati wa ziara yake ya siku mbili kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Arusha.

Katika moja ya miradi hiyo, Rais Kikwete alizindua Shule ya Msingi ya Sokoine, ambayo ni kwa ajili ya watoto wa wapiganaji na maofisa wa chuo hicho, shule ambayo aliiahidi mwenyewe wakati alipozindua nyumba za kisasa za askari wa chuo hicho, Januari mwaka 2010.

Akizungumza na wapiganaji na maofisa hao baada ya kufungua shule hiyo, Rais Kikwete alizungumzia mambo mbalimbali, ikiwamo fujo ambazo zimekuwa zikifanyika nchini kwa kisingizio cha siasa na hivi karibuni kwa kisingizio cha udini.

Rais Kikwete aliwaambia askari hao kwamba, Katiba inatoa uhuru wa kuabudu na uongozi wake unalea uhuru huo pamoja na uhuru wa kisiasa.

“Lakini uhuru huo siyo uhuru wa kuvunja amani wala utulivu wa nchi. Hatuwezi kuvumilia uvunjifu wa amani kwa kisingizio chochote. Hakuna mtu ataruhusiwa kuhujumu ama kuvuja utulivu na amani ya nchi. Kamwe hatutaliruhusu jambo hili, kwa kisingizio chochote,” alisema Rais Kikwete.

Rais pia aliwaambia askari hao, kwamba Serikali yake hivi karibuni, itaanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 10,000 za wanajeshi katika maeneo mbalimbali nchini.

“Ili kuwawezesha wanajeshi wetu kuishi katika nyumba nzuri, hatuwezi kuendelea kuwaweka askari na maofisa wetu katika zile nyumba alizoacha Douglas pale Lugalo.

“Tutajenga nyumba nzuri na za kisasa, ili muweze kuishi katika nyumba bora na za kisasa,” alisema.

Pia alizungumzia kwa kifupi kuhusu utekelezaji wa mpango wa miaka 15 wa kuboresha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ikiwamo upatikanaji wa vifaa vipya na vya kisasa zaidi.

“Katika miaka mitatu ijayo, tutakuwa na jeshi lenye sura mpya kabisa na huo ndio utakuwa mchango wangu kwenu, kwa kadri ninavyojiandaa kuondoka madarakani,” alisema Rais Kikwete.


Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye ukarabati mkubwa wa Barabara ya Minjigu-Arusha, yenye urefu wa kilomita 98, Rais Kikwete alirudia wito wake kuhusu umuhimu wa utulivu wa kidini nchini.

“Kwa kweli yanayotokea nchini kwa sasa kuhusu fujo za kisiasa na kidini, ni mambo yasiyonipa raha kabisa.

“Tusiwape nafasi wanaopandikiza chuki za kisiasa na chuki za kidini. Tuendelee kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu na siri ya kudumisha tunu hizo ni utii wa sheria na utii wa hiari wa sheria.

“Tukianza kubaguana kwa misingi ya dini, siasa na rangi za miili yetu hatufiki popote, tafadhali tuyaache haya,” alisema Rais Kikwete 

CHANZO: MTANZANIA

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: