WAKATI Watanzania wakisubiri kwa hamu hatima ya rufaa ya
aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mahakama ya Rufani
nchini, imetoa amri ya kuiondoa rufaa iliyokuwa imekatwa na aliyekuwa
mgombea ubunge wa Jimbo la Ubungo, Hawa Ng’umbi (CCM) dhidi ya Mbunge wa
jimbo hilo, John Mnyika (CHADEMA) baada ya kuridhia maombi ya pande
zote mbili zilizoomba mahakama hiyo kuiondoa mahakamani.
Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani; Natalia Kimaro, Salum Massati na
Catherine Oriyo waliketi jana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya rufaa
hiyo iliyokuwa ikipinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar
es Salaam, katika kesi ya kupinga ubunge wa Mnyika iliyofunguliwa na
Ng’umbi.
Jaji wa Mahakama Kuu Upendo Msuya mwaka huu, katika hukumu yake
alitupilia mbali kesi hiyo ya Ng’umbi kwa madai kuwa alishindwa kuleta
ushahidi thabiti ambao unaonyesha taratibu na sheria za uchaguzi
zilikiukwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambao ulimtangaza Mnyika
kuwa ni mbunge halali wa jimbo hilo.
Jana, Jaji Kimaro alisema anaiondoa rufaa hiyo iliyokuwa ikipinga
hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
“Kwa kuwa mwomba rufaa (Ng’umbi) na mjibu rufaa (Mnyika) kabla ya leo
kuja hapa mahakamani walikutana nje ya mahakama na kufikia uamuzi wa
kuiondoa bila gharama rufaa hii ambayo leo ilikuja kwa ajili ya kuanza
kusikilizwa, na leo mawakili wao wamewasilisha ombi hilo mbele ya
mahakama hii, basi mahakama hii inakubali ombi lao hilo na inatoa amri
ya kuiondoa rufaa hii chini ya 102(3) na (4) cha Kanuni za Mahakama ya
Rufani nchini,” alisema Jaji Kimaro.
Awali kabla ya kutolewa kwa amri hiyo ya mahakama, wakili aliyekuwa
akiwawakilisha wajibu rufaa wengine ambao ni Msimamizi wa Uchaguzi wa
Jimbo la Ubungo, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao walikuwa
wakitetewa na wakili wa serikali, Obadia Kameya wakati mjibu rufaa wa
kwanza alikuwa akitetewa na Edson Mbogoro, walianza kwa kuikumbusha
mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa rufaa na
kwamba wapo tayari kwa ajili ya kuendelea.
Lakini wakili wa Ng’umbi alisimama na kujitambulisha, na kisha
akaeleza kuwa siku mbili zilizopita mteja wake alikutana na Mnyika
kufanya mazungumzo ambayo yalihitimishwa kwa kukubaliana kuwa rufaa hiyo
waiondoe mahakamani, na kwamba amemwelekeza awasilishe ombi hilo la
kuomba rufaa hiyo iondolewe mahakamani bila gharama.
Baada ya kuwasilisha ombi hilo, mawakili Kameya na Mbogoro walieleza
kuwa hawana pingamizi na ombi hilo na kwamba wanaiachia mahakama iamue.
Baada ya Jaji Kimaro kumaliza kutoa amri hiyo, Mnyika ambaye jana
alikuwepo mahakamani hapo huku Ng’umbi akishindwa kufika, aliwaeleza
waandishi wa habari nje ya mahakama kuwa amefurahishwa na uamuzi huo.
“Ni wakili wa Ng’umbi ndiye alimpigia simu wakili wangu Mbogoro
wakutane ili wazungumzie ombi la Ng’umbi la kutaka kuiondoa rufaa yake
aliyoikata dhidi yangu, na kisha mawakili wetu wakaja kunikutanisha mimi
na Ng’umbi tukazungumzia ombi hilo na tukakubaliana na ombi lake
lililotaka aiondoe rufaa yake,” alisema Mnyika huku akiwa amezingirwa na
umati wa wafuasi wake.
Aidha, wafuasi wa Mnyika, wengine wakiwa wamebeba bandera za CHADEMA,
waliondoka katika eneo la Mahakama ya Rufaa kwa maandamano, huku
wakiimba nyimbo za kupongeza uamuzi huo na kumsifia mbunge huyo ambaye
kwa sasa atakuwa hakabiliwi tena na kesi ya kupinga ubunge wake katika
mahakama yoyote hapa nchini.
Mnyika kulipua mafisadi leo
Wakati huo huo, Mnyika alisema kuwa leo atawalipua na kutangaza
waziwazi majina ya vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao alidai
walishiriki kuhujumu mali za viwanda vya nguo vilivyoko katika jimbo
lake.
Mnyika alisema atafanya hivyo, atakapokuwa katika ziara ya siku mbili
katika jimbo hilo inayoanza leo, huku akiweka wazi kutofumbia macho tena
kuhusiana na hujuma ya baadhi ya watendaji wa Serikali ya CCM.
“Kesho (leo Jumamosi) nitaanza ziara katika Kata ya Manzese kukagua
viwanda vilivyouawa na serikali ya CCM, na nitataja majina ya vigogo wa
CCM waliofanya ufisadi hadi kuua viwanda na kusababisha vijana kukosa
ajira,” alisema.
Mnyika alisema Mwalimu Nyerere katika utawala wake alikazania na
kuanzisha viwanda kwa ajili ya kuokoa na kusaidia ajira kwa vijana,
lakini baadhi ya viongozi mafisadi wa CCM walikula njama na kuvifilisi.
Aliongeza kuwa, kesho, akiwa katika Kata ya Ubungo, atalipua ukweli
wote wa hujuma kubwa zilizofanywa na watendaji wa serikali katika
Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO).
Alisema kuwa amesikia Jumatatu wiki ijayo, TANESCO watafanya mkutano
wa kutaka kupandisha bei ya umeme, na akawataka wakazi wa Ubungo
kushiriki na kupinga jitihada zozote za kuongeza bei ya nishati hiyo.
“Bei ya sasa ni balaa kwa Watanzania wanyonge, lakini bado tena
wanataka kuongeza mzigo kwa wananchi jambo ambalo hatuwezi kulikubali,”
alisema Mnyika.
CHANZO: TANZANIA DAIMA



No comments:
Post a Comment