Shekhe Ponda Issa Ponda
KADHI Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Habibu
(49) amekana kumfahamu Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
Tanzania, Shekhe Ponda Issa Ponda na wafuasi wake katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Habibu alikana kumfahamu Ponda na wafuasi wake
jana Mbele ya Hakimu Mkazi, Ritha Tarimo mara baada ya kutakiwa na
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka awatazame kina Ponda na
aelezee iwapo kuna mmoja aliwahi kuingia kwenye Baraza la Maulamaa wa
Bakwata.
Baada ya kuambiwa hivyo, Habibu alidai kuwa hakuna
hata mmoja anayefamfahamu katika utendaji wa kazi za Uislamu kama
kiongozi kwenye baraza lakini akawatambua kimavazi kuwa ni waumini wa
Kiislamu. “Ila kwa kuona, muungwana ishalaa inamuonyesha kuwa kuna
baibui, kanzu na kofia (baraghashia) inaonekana kuna Waislamu na wasio
Waislamu.”
Akiendelea kutoa ushahidi wake, Kadhi huyo
aliiambia mahakama ; “Nathibitisha kuwa Kampuni ya Agritanza Ltd
inamiliki lile eneo kwa Uhalali na kwamba haikupita uchochoroni ikaruka
ukuta ikaingia ndani ya hilo eneo, ilifuata utaratibu na kupokea hati
zote na haki yake,” alisema Habibu.
Alifafanua kuwa Baraza la Maulamaa ni chombo
kinachotoa uamuzi ya mwisho na kutoa miongozo mbalimbali kwa Waislamu na
kwamba Bakwata inawakilisha Waislamu wote Tanzania.
Alidai kuwa Baraza hilo la Maulamaa linaundwa na
wajumbe 10 kutoka mikoa mbalimbali na kwamba mjumbe huteuliwa kutokana
na kuwa na kiwango cha elimu kilichopevuka na uadilifu.
“Baraza hili linamiliki mali zinazohamishika na
zisizohamishika na sisi ndiyo tunachukua uhimizwaji wa kuulizwa na
kudodoswa kila kilichopo ndani ya Bakwata kwa kuwa ni lazima tuhusishwe
hususan katika masuala ya elimu,” alisema Habibu.
Kwa mujibu wa maelezo ya Katiba, vikao hufanyika
mara mbili kwa mwaka chini ya Mwenyekiti wa Baraza la Maulamaa pamoja na
vikao vya dharura. “ Januari 3, 2011, tulifanya kikao cha kawaida
ambacho kilikuwa na agenda tatu ikiwemo ya umuhimu wa kujenga chuo Kikuu
cha Kiislamu ambapo wajumbe walipendekeza kijengwe katika maeneo ya
Dodoma, Tanga ama Chang’ombe.”
“Kutokana na mapendekezo hayo, tuliafikiana
kijengwe Chang’ombe lakini ikaonekana kuwa Chuo Kikuu cha Kiislamu
kinahitaji sehemu kubwa na pale kuna Ekari 4 hapatoshi,” alisema shahidi
huyo wa pili wa upande wa mashtaka.
Hivyo walimtaka Katibu Mkuu wa Baraza la Maulamaa
na timu yake wafanye mchakato wa kutafuta eneo maalumu kubwa ambalo
wataweza kujenga chuo hicho Kikuu cha Kiislamu na kwamba baada ya siku
nne au tano walipigiwa simu na kuwa wanahitajiwa Makao Makuu (Bakwata).
Shahidi huyo alidai kuwa walipofika waliambiwa kuwa kuna kikao cha dharura na kupatiwa taarifa na Katibu Mkuu wao juu ya mchakato huo wa kutafuta eneo kuwa kampuni ya Agritanza Ltd ilijitokeza na kutaka tuwape zile ekari nne na wao watupe ekari 40 huko Kisarawe Pwani.
Shahidi huyo alidai kuwa walipofika waliambiwa kuwa kuna kikao cha dharura na kupatiwa taarifa na Katibu Mkuu wao juu ya mchakato huo wa kutafuta eneo kuwa kampuni ya Agritanza Ltd ilijitokeza na kutaka tuwape zile ekari nne na wao watupe ekari 40 huko Kisarawe Pwani.
“Sisi tuliona ekari 40 kwa ekari 4 ni kama ardhi
na mbingu na Mungu alisikia kilio chetu akawaleta hao na tukaona kabla
ya mazungumzo twende tukaone, tulipofika Manshalaa eneo lilikuwa sehemu
nzuri, linapendeza, linavutia na mimi nilikuwa wa kwanza kuwashawishi
wenzangu tukubaliane na mabadilishano na mchakato ukafanyika,” aliongeza
shahidi huyo mahakamani hapo.
Hivyo Baraza la Maulamaa liliridhia kutoa maamuzi kwa Baraza la Wadhamini kufanyika kwa mchakato na makubaliano wa maeneo hayo.
Baada ya kutolewa kwa ushahidi huo, mmoja wa Wakurugenzi wa
Kampuni ya Agritanza Ltd, Seleman Mohamed (48) akitoa ushahidi wake
aliiambia mahakama hiyo kuwa yeye ni mfanyabiashara na kwamba ni kweli
wao waliingia mkataba na Bakwata wa kubadilishana ardhi ekari nne kwa
ekari 40.
Kesi itakuja kwa ajili ya kutajwa Desemba 18, mwaka huu na itaendelea kusikilizwa Desemba 31, mwaka huu.
Ponda, Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
Tanzania, Shekhe Mukadam Abdallah Swalehe (45) na wafuasi wao
wanakabiliwa na mashtaka matano yakiwemo ya uchochezi, kula njama na
wizi wa mali yenye thamani ya Sh59.6 milioni.
Katika shtaka la uchochezi, Shekhe Ponda na Shekhe
Mukadam wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu katika eneo
la Chang’ombe Malkazi,akiwa kama Kiongozi wa Baraza na Jumuiya ya
Kiislamu Tanzania aliwashawishi wafuasi wake kutenda makosa hayo.
MWANANCHI



No comments:
Post a Comment