Malasusa aikomalia Serikali

 Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa

ATAKATA ICHUKUE HATUA MADHUBUTI DHIDI VYA VIKUNDI  VYOTE CHOCHEZI

WAKATI baadhi ya vinara wa vurugu zinazohusishwa na masuala ya kidini wakiwa Mahakamani jijini Dar es Salaam na Zanzibar, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa ameidai kuwa Serikali ina kigugumizi katika kusema ukweli kuhusiana na vurugu hizo na zingine zinazotokana na imani za kidini nchini.
Akihutubia wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa 31 wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani unaofanyika mjini Bagamoyo jana, Askofu Malasusa alisema kuwa,  Serikali ilipaswa si tu kuwakamata, bali pia kufuta usajili wa vikundi vyote vinavyosababisha vurugu nchini.
Askofu Malasusa alisema kuwa, kitendo cha  Serikali kukaa kimya bila kuchukulia hatua vikundi vilivyosajiliwa na kuwa na mlengo tofauti na madhumuni yake ama inapendezwa, kuvutiwa na hata kushawishiwa na yale ambayo yanazungumzwa na vikundi hivyo japo wanaweza wasikubaliane na vitendo vyao.
Kuanzia katikati ya Oktoba mwaka huu, kulizuka ghasia katika mji wa Zanzibar na vitongoji vyake zinazodaiwa kufanywa na wafuasi wa Kikundi cha Uamsho vilivyokwenda sambamba na kuchoma makanisa.
Katika mfululizo wa matukio hayo, makanisa takriban saba yalichomwa moto jijini Dar es Salaam baada ya kuzuka ghasia maeneo ya Mbagala, wilayani Temeke, zilizotokana na imani za kidini na watu 49 walikamatwa na baadaye kuachiwa huru.
Hata hivyo, kesi bado ziko mahakamani kwa viongozi wa wafuasi hao ambao kwa Zanzibar ni Farid Hadi Ahmed na Dar es Salaam, Sheikh Ponda Issa Ponda.
“Naomba serikali ipige marufuku vikundi hivi, hatutaki viendelee wala kupewa nafasi kushamiri hata kama ni ndani ya kanisa ninaloliongoza kwani yaliyotokea Rwanda na Burundi na hata Kenya. hatutaki yatokee hapa kwetu” alisema Askofu Malasusa.
Mkuu huyo wa Kanisa alisema katika hotuba yake ya ufunguzi kuwa, pamoja Wakristo wamejifunza kupitia maandiko Matakatifu kuwa: ‘Kushindana kwetu sio kwa juu ya damu na nyama bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, majeshi, pepo wabaya katika ulimwengu wa roho’, hana uhakika kama wote wana uvumilivu wa kutosha.
“Sina hakika mtu akija na silaha kushambulia na  wewe upo ndani na silaha na biblia kama utatoka na biblia, au silaha,” alisema Mkuu huyo wa KKKT na kusisitiza kuwa, jambo ambalo halitakiwi litokee nchini.
Askofu Malasusa alitoa wito kwa serikali kushirikiana na taasisi za dini kikamilifu kudumisha umoja, amani na mshikamano wa kindugu miongoni mwa Watanzania.
“Tumeshuhudia uchomaji wa makanisa huko Zanzibar, Mwanza, Mdaula, Mto wa Mbu, Tunduru, Rufiji, Kigoma na hapa Dar es Salaam, vitendo ambavyo si utamaduni wa Watanzania ambako kwa asili ni wamoja, wanapendana sana wanashirikiana bila kujali tofauti ya dini zao,” alisema Malasusa na kuongeza;
“Watanzania wengi wanasikitishwa sana vikundi vinavyochochea chuki na uhasama baina yao, hivyo Serikali inatakiwa kuchukua hatua zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi vinginevyo amani ya nchi yetu itakuwa mashakani.”
Malasusa ambaye alisema kuwa, ingawa Tanzania inatajwa kuwa kisiwa cha amani, matukio yaliyotokea hivi karibuni yanatia shaka.
Alisema kitendo cha kuchomwa moto makanisa na watu wanaodaiwa kuwa ni Waislamu wenye msimamo mkali  kilimuogopesha sana kwani lingeweza kutokea lolote kama upande wa pili wangeamua kulipiza kisasi.
“”Ukweli, hakuna taifa ambalo linaweza kuruhusu vita vya dini kisha likabaki salama... Dini siku zote zina uwezo wa kulifanya jambo la kawaida kuwa la kufa na kupona kwa sababu, dini zinatamka na kushikilia hatma ya maisha ya mtu  baada ya ulimwengu wa sasa,” alisema.
Malasusa alisema kuwa, dini zinamhakikishia mtu maisha ya milele ambayo kila mtu anapenda kuhakikishiwa awapo duniani, hivyo anaamini kuwa wanaoeneza Uislamu kwa njia ya kujenga chuki na uhasama dhidi ya dini nyingine hao si Waislamu na hali kadhalika kwa Wakristo kama wapo.
Alisema; "Ninasema hivyo ili Taifa lipone japokuwa anayesema kweli anakuwa adui wa wengi na kuonekana hafai katika jamii.
"Lakini nasema, kwangu ni heri kuzuia kuliko kuponya au kutibu."
Mbali na hayo, aliwataka waumini wa kanisa hili kuchangamkia utoaji wa maoni ya katiba ili waweze kuwa na mapendekezo yao katika katiba ijayo.
“Ushiriki wa Wakristo katika utoaji wa maoni ni mdogo sana, nasisitiza kuwa ni  vema tushiriki mambo yote yanayohusu jamii kwa kuwa kanisa ni sehemu ya jamii,” Askofu Malasusa aliangaliza.

Akemea ushoga
Malasusa pia alikemea utandawazi katika kanisa, likiwemo suala la ushoga na utoaji wa mimba kubainisha kuwa vitendo hivyo havina nafasi katika Kanisa la KKKT kwani hakuna haki za jamii ambazo zinapingana na maandiko matakatifu.
Kauli mbiu ya mkutano huo inatoka katika kitabu cha Wafilipi 3:  12 - 14 ambayo inasema: ‘Sijidhanii kwamba nimefika, bali nakaza mwendo.”


CHANZO: MWANANCHI

No comments

Powered by Blogger.