ALIYEKUWA
Mbunge wa Igunga, Dk. Dalaly Kafumu (CCM), ambaye alivuliwa ubunge na
Mahamaa Kuu Kanda ya Tabora Agosti mwaka jana, amekata rufaa kupinga
hukumu hiyo.
Akisoma
hukumu hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu, Mary Shangali, alitaja vipengele sita
alivyotumia kutengua matokeo ya ubunge wa Dk. Kafumu.
Alisema
vipengele hivyo vilikuwa ni pamoja na matukio yaliyojitokeza wakati wa
kampeni za uchaguzi huo ambapo ni kutolewa kwa ahadi ya kutojengwa
daraja kama hatachaguliwa Kafumu.
Hata hivyo,
katika rufaa yake hiyo aliyoiwasilisha mahakamani juzi, Dk. Kafumu
alisema anaamini atashinda kutokana na sababu zilizotolewa na Jaji wa
Mahakama Kuu kuwa dhaifu na zisizomhusu yeye.
Akizungumza
na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Dk. Kafumu alisema kuwa
atawakilishwa na mawakili watatu ambao aliwataja kuwa ni pamoja na Dk.
Masumbuko Lamwai, Kayaga na Kanyama.
Dk. Kafumu
alisema sababu za kutaka rufaa mbali na kwamba ni haki yake Kikatiba
lakini pia anaamini kuwa mahakama kuu ilikosea kumhusisha na vurugu
zilizosababisha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Igunga, Fatuma Kimario,
kuvuliwa Hijab na wafuasi wa CHADEMA.
Alisema
kitendo cha Magufuli kutoa ahadi ya daraja ilikuwa ni sehemu ya
utekelezaji wa Ilani ya CCM na yeye binafsi hakuhusika kutoa ahadi hiyo.
Katika
mahojiano hayo, Dk. Kafumu alilalamika kuwa baadhi ya waandishi wa
habari walimlisha maneno kuhusu uamuzi wake huo wa kukata rufaa na hivyo
kufafanua upya kile alichokisema baada ya hukumu.
“Nilisema
nimetoka mahakamani, bado mapema nawasiliana na chama changu, lakini
hata kama nikipoteza ubunge na ukamishna wa madini, mimi bado ni
mtaalamu nitafanya kazi nyingine, sikusema sitakata rufaa,” alisisitiza.
Katika kesi hiyo mlalamikaji alikuwa Joseph Kashindye, aliyekuwa mgombea ubunge kupitia CHADEMA.
Katika hukumu yake Jaji Shangali alisema ahadi hiyo ilikiuka mwenendo wa kampeni za uchaguzi.
Aidha Jaji
alisema pia kitendo kilichofanywa na upande wa walalamikiwa cha kwenda
kutembelea hospitali na kutoa misaada mbalimbali kilikiuka taratibu na
hivyo kuathiri zoezi zima la uchaguzi huo.
Kipengele
kingine alichokitaja kukiuka taratibu za uchaguzi ni pamoja na kitendo
cha ugawaji mahindi ya msaada siku chache kabla ya upigaji kura katika
jimbo hilo na hivyo kuwafanya wananchi kupiga kura kutokana na ushawishi
wa misaada hiyo.
Pia kupanda
katika majukwaa ya kampeni kwa Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, Ismail
Aden Rage (CCM), akiwa amening’iniza silaha kiunoni nako kuliathiri
mwenendo mzima wa uchaguzi huo.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment