Msafiri Jeremia akiwa na mkewe Monica Daniel.
NDOA ya Msafiri Jeremia na Monica Daniel, wakazi wa Kijiji cha
Munisagale,Wilaya ya Kilosa mkoani hapa imekuwa ya mateso baada ya mume
kupata ajali na kupoteza mkono na mguu.
Hayo ni maneno ya baadhi ya wanakijiji wa Munisagale waliyoyatoa kwa
nyakati tofauti mbele ya mwandishi wetu huku wakiwa na majonzi wakidai
kwamba tangu mwaka 2000, Jeremia alipopata ajali ya treni na kukatwa
mguu na mkono, familia hiyo imekuwa ikiishi maisha ya dhiki huku Monica
akibeba jukumu la kuilisha.
Jeremia alipohojiwa na gazeti hili alisema akiwa kwenye hekaheka za
kutafuta riziki ndipo alipopata ajali iliyomtia kilema cha maisha.
“Ajali ya treni iliyotokea mwaka 2000 katika Kijiji cha Msagali mkoani
Dodoma, mimi nilikuwemo ambapo nilikatwa mguu na mkono na tangu kipindi
hicho maisha yangu ni ya tabu kwani jukumu la kulea familia limekuwa la
mke wangu ambaye hufanya vibarua vya kulima, akikosa tunalala na njaa na
watoto wetu wawili,” alisema Jeremia.
Mke wake alikuwa na haya ya kusema: “Namshukuru Mungu kwa kumnusuru mume
wangu na kifo kwenye ajali hiyo kwani wengi walikufa lakini baba
watoto wangu alinusurika na kukatika mguu na mkono, hayo ni mapenzi ya
Mungu.
“Naamini hapa duniani kila mtu ni mlemavu mtarajiwa na kama walivyosema
wahenga kwamba kabla hujafa haujaumbika, haya yaliyomkuta mume wangu
yanaweza kumkuta yeyote hata mimi.
“Familia yetu tuna watoto watatu, Simon (20), Thomas (17) na Magreth
(13) hawa wawili wamemaliza shule huyu wa mwisho kutokana na gharama
kubwa za shule tumeshindwa kumsomesha kwa sababu ya ukata,” alisema
Monica.
Mwandishi wetu aliamua kumpiga picha bure na akaziambatanisha katika
waraka wake wa kwenda kwa waziri mkuu kitengo cha maafa ambapo kwa sasa
wanasubiri majibu ya barua hiyo.
Mtu aliyeguswa na habari hii anaweza kumsaidia Jeremia kwa kuwasiliana naye kwa
NAMBA +255715 289 073.
1 comment:
NAWAPA POLE SANA BILA SHAKA MUNGU ATAWASAIDIA WAPATE MSAADA KUTOKA KWA WAZIRI MAANA HATA YEYE HALI ATAIONA. NAKUSHUKURU KWA KUWAPA MSAADA WA PICHA BURE
Post a Comment