RUFANI kumi
zimewasilishwa mbele ya Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya
TFF kuhusiana na uchaguzi utakaofanyika Februari 22 na 24 mwaka huu.
Wakati
uchaguzi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) utafanyika Februari
22 mwaka huu, ule wa TFF wenyewe utafanyika Februari 24 mwaka huu.
Waliowasilisha
rufani mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Idd Mtiginjola ni pamoja na
waombaji uongozi saba walioenguliwa katika kinyang’anyiro hicho.
Warufani hao ni Omari Mussa Nkwarulo na Michael Richard Wambura
walioomba kugombea urais na umakamu wa rais.
Wengine ambao
waliomba ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda mbalimbali ni
Farid Nahdi (Morogoro na Pwani), Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu),
Omari Isack Abdulkadir (Dar es Salaam), Eliud Peter Mvella (Iringa na
Mbeya) na Shaffih Kajuna Dauda (Dar es Salaam).
Warufani
wengine ni wadau ambao waliweka pingamizi dhidi ya baadhi ya waombaji
uongozi katika TPL Board na TFF, pingamizi ambazo zilitupwa mbele ya
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa sababu za kiufundi.
Wadau hao
waliokata rufani ni Agape Fue dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga
kumpitisha Jamal Malinzi kugombea urais, Medard Justinian dhidi ya
Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga kumpitisha Athuman Nyamlani kugombea
urais, na Frank Mchaki dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga
kumpitisha Hamad Yahya kugombea uenyekiti wa TPL Board.
Kamati ya
Rufani ya Uchaguzi ya TFF imetoa siku ya kesho (Februari 9 mwaka huu)
kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 8 mchana kwa wote wenye maslahi na rufani
hizo (interested parties) kupitia rufani hizo na kuwasilisha hoja zao
kwa maandishi.
Kwa
watakaoshindwa kufanya hivyo watapata fursa ya kuwasilisha hoja zao kwa
mdomo, ambapo wanaweza kuwa wenyewe au wanasheria wao siku ya
usikilizwaji wa rufani hizo. Rufani zitasikilizwa Jumapili (Februari 10
mwaka huu) kuanzia saa 2 asubuhi.
OLJORO MWENYEJI WA SIMBA VPL 2012/2013
Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa 2012/2013
inaingia raundi ya 16 kesho (Februari 9 mwaka huu) kwa mechi nne ambapo
Oljoro JKT itaikaribisha Simba jijini Arusha.
Mechi hiyo
namba 129 itafanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid
huku Simba ikiingia na kumbukumbu ya sare katika mechi yake iliyopita
dhidi ya JKT Ruvu wakati wenyeji wao wakiwa wameshinda 2-0 dhidi ya
Kagera Sugar.
Uwanja wa
Kaitaba mjini Bukoba wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 3,000 tu
utatumika kwa mechi kati ya wenyeji Kagera Sugar na Mgambo Shooting.
Mwamuzi wa mechi hiyo atakuwa Amon Paul kutoka Musoma mkoani Mara.
Toto Africans
baada ya kufanya vibaya katika mechi tatu zilizopita ugenini imerejea
nyumbaji jijini Mwanza itakapoumana na Coastal Union ya Tanga katika
mchezo utaochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.
Mwamuzi Simon
Mberwa kutoka mkoani Pwani ndiye atakayechezesha mechi kati ya wenyeji
Tanzania Prisons na African Lyon ambayo imepata huduma za kocha mpya
Salum Bausi kutoka Zanzibar. Hiyo itakuwa mechi ya kwanza kwa Bausi
kuiongoza timu katika VPL.
Maofisa
wengine wa mechi hiyo ni mwamuzi msaidizi namba moja Abdallah Rashid,
mwamuzi msaidizi namba mbili Abdallah Mkomwa wote kutoka Pwani wakati
mwamuzi wa mezani ni John Kanyenye wa Mbeya. Kamishna wa mechi hiyo ni
Rashid Rwena kutoka Ruvuma.
Mechi kati ya
Mtibwa Sugar na Azam iliyokuwa ichezwe kesho imesogezwa mbele kwa siku
moja ambapo sasa itafanyika Jumapili (Februari 10 mwaka huu) katika
Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro.
FDL KUENDELEA KUTIMUA VUMBI WIKIENDI
Ligi Daraja la
Kwanza (FDL) kuwania tiketi za kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu
ujao inaendelea kutimua vumbi wikiendi hii kwa mechi kumi na moja
zitakazopigwa kwenye viwanja mbalimbali.
Kundi A
keshokutwa (Februari 10 mwaka huu) Mbeya City itacheza na Polisi Iringa
katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, Mkamba Rangers
itaumana na Burkina Faso (Uwanja wa CCM Mkamba) wakati JKT Mlale itakuwa
mwenyeji wa Kurugenzi kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Green Warriors
na Ndanda zitacheza kesho (Februari 9 mwaka huu) kwenye Uwanja wa
Karume, Dar es Salaam katika moja ya mechi za kundi B. Mechi nyingine
kundi hilo kesho ni kati ya Tessema na Villa Squad kwenye Uwanja wa
Mabatini mjini Mlandizi.
Keshokutwa
(Februari 10 mwaka huu) Transit Camp itacheza na Ashanti United kwenye
Uwanja wa Karume, Dar es Salaam wakati Polisi Dar es Salaam na Moro
United zitavaana Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.
Kundi
C kesho (Februari 9 mwaka huu) ni Polisi Dodoma vs Polisi Tabora
(Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Polisi Mara vs Mwadui (Uwanja wa Karume,
Musoma), Morani vs Kanembwa JKT (Uwanja wa Kiteto, Manyara) na Rhino
Rangers vs Pamba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF
No comments:
Post a Comment