Stori:Hamida Hassan na Gladness Mallya
MKAZI wa Mbezi Kwa Msuguri jijini Dar, Sultan Rashid hivi karibuni alizua tafrani nyumbani kwao baada ya kudhaniwa kuwa amefariki dunia pale alipopiga hodi na kuingia sebuleni.
Kwa mujibu wa baba wa Rashid, mzee Sultan Rashid, Ijumaa iliyopita alipokea taarifa ya msiba wa mtoto wake huyo na kuambiwa kwamba kifo chake kimetokana na ajali mjini Morogoro.
Mzee Sultan alikwenda Morogoro na alipofika hospitali ya mkoa aliambiwa kuwa mtoto wake alishazikwa na manispaa kutokana na kukosa ndugu.
“Baada ya kurudi nyumbani tukafanya taratibu zote za msiba kwani jitihada zetu za kwenda kwenye vituo vya polisi pale Morogoro hazikuzaa matunda,” alisema.
Siku nne baada ya kusomwa kwa hitima, saa nne usiku, kijana Rashid alirudi Dar na kuingia nyumbani kwao huku akiwashuhudia ndugu zake wakiendelea kulala matanga kutokana na msiba wake.
Ndugu na majirani walimshangaa na wengine kumkimbia kutokana na kuamini kuwa kijana huyo alishafariki dunia hadi pale walipotulizwa na binamu wa kijana huyo.
Rashid alisema kwamba alipata ajali na kupoteza fahamu kwa siku nne na alilazwa katika Hospitali ya Sabasaba mjini Morogoro.
“Nilipozinduka nilijikuta nikihudumiwa na Waislamu wa madhehebu ya Sunni, nilipopata nafuu walinipa nauli na kunitaka nirudi nyumbani,” alisema.
Mzee Sultan alisema anawashukuru wote waliomsaidia katika tatizo hilo na kuongeza kwamba ataandaa dua kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na kurejea kwa mwanaye.
CHANZO: GPL



No comments:
Post a Comment