Taarifa za kimichezo kutoka shirikisho la leo mpira wa miguu TFF
Kiingilio cha chini katika mechi ya mchujo
ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of
the Atlas) itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.
Viti vya kijani katika uwanja huo
wenye uwezo wa kumeza watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa viti
vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045 ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti
vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio vya daraja la juu ni
kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni sh. 15,000 wakati sh.
20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A yenye watazamaji 748
kiingilio chake ni sh. 30,000.
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo
itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza kuuzwa siku mbili ya mchezo
(Ijumaa na Jumamosi) katika vituo vifuatavyo; Shule ya Sekondari
Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa
Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni na Dar Live
Mbagala.
Katika vituo hivyo tiketi
zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya mauzo ya
tiketi uwanjani siku ya mechi. Vilevile tunapenda kuwakumbusha
watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika maeneo
yasiyohusika ili kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya
kushuhudia mechi hiyo.
SAMATA, ULIMWENGU WARIPOTI STARS
Washambuliaji wa Taifa Stars,
Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wamewasili nchini jana usiku na
kwenda moja kwa moja kambini.
Ujio wa washambuliaji hao
unafanya idadi ya wachezaji walioripoti kambini kufikia 20 kati ya 23
walioitwaa baada ya mshambuliaji Khamis Mcha aliyekuwa na kikosi cha
timu yake ya Azam nchini Liberia naye kuripoti kambini leo asubuhi.
Wachezaji John Bocco na makipa
Mwadini Ally na Aishi Manula ambao pia nao walikuwa Liberia na timu yao
ya Azam wataripoti kambini leo alasiri. Wachezaji hao ni sehemu ya
msafara wa timu ya Azam ambao utakuja na ndege ya mchana kutokea Nairobi
kwa vile ile ya asubuhi waliyotangulia nayo wenzao kuwa imejaa.
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha Kim Poulsen leo
inaendelea na mazoezi Uwanja wa Taifa. Mazoezi hayo yataanza saa 9
alasiri.
TIMU TATU ZASHUKA DARAJA FDL
Timu tatu zimeshuka daraja kutoka
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kurudi Ligi ya Mkoa msimu ujao wa 2013/2014
baada ya kushika nafasi za mwisho katika ligi hiyo msimu huu 2012/2013
iliyomalizika wikiendi iliyopita.
Small Kids ya Rukwa imeporomoka
kutoka kundi A baada ya kuondolewa kwenye michuano hiyo mapema kwa
kushindwa kufika uwanjani kwenye moja ya mechi zake. Kwa mujibu wa
kanuni matokeo yote ya mechi ilizocheza yalifutwa.
Moro United ya Dar es Salaam
ndiyo iliyoaga FDL kutoka kundi B baada ya kumaliza mechi zake ikiwa na
pointi tatu. Wakati kutoka kundi C timu iliyoshuka ni Morani ya Manyara
iliyomaliza ligi ikiwa na pointi kumi na moja.
Timu zilizopanda daraja kucheza
Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2013/2014 ni Mbeya City ya Mbeya
iliyoongoza kundi A ikiwa na pointi 31, vinara wa kundi B timu ya
Ashanti United ya Dar es Salaam yenye pointi 29 wakati Rhino Rangers ya
Tabora imepanda kutoka kundi C ikiwa na pointi 32.
LIUNDA KUTATHIMINI WAAMUZI KOMBE LA DUNIA
Mwamuzi Msaidizi wa zamani wa
kimataifa wa Tanzania, Leslie Liunda ameteuliwa kuwa mtathimini wa
waamuzi (referee assessor) kwenye moja ya mechi za mchujo za Kombe la
Dunia.
Shirikisho la Kimataifa la Mpira
wa Miguu (FIFA) limemteua Liunda kutathimini waamuzi kwenye mechi kati
ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Libya itakayochezwa Jumapili
(Machi 24 mwaka huu).
Mechi hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Martyrs jijini Kinshasa kuanzia saa 9.30 alasiri kwa saa za Afrika ya Kati (CAT).
Waamuzi watakaochezea mechi
hiyo William Selorm Agbovi atakayekuwa mwamuzi wa kati, Malik Alidu
Salifu (mwamuzi msaidizi namba moja), David Laryea (mwamuzi msaidizi
namba mbili) na mwamuzi wa mezani (fourth official) Cecil Amatey
Fleischer. Waamuzi wote hao wanatoka Ghana.
Post a Comment