Mkuu Mstaafu, John Malecela ameonya
Watanzania kuhusu mpasuko wa kidini akibainisha kuwa utaigawa nchi
vipande vipande, Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi ametoa wito maalumu
akiwataka waumini wa dini tofauti kuvumiliana.
Malecela na Mwinyi walitoa kauli hizo mjini Dodoma
na Kibaha, Pwani jana kwa nyakati tofauti, wote wakiwa na nia ya
kusisitiza ulinzi wa amani ya nchi inayoanza kutetereka.
Kauli ya Malecela
Malecela alisema kwa namna ilivyo sasa, Tanzania
imekuwa ni tofauti na ile aliyoanza kuiona yeye katika kipindi cha uhuru
kwenye miaka ya 1960 wakati huo nchi ikiwa moja na watu wake wakiwa ni
wamoja.
“Msipokuwa makini na amani yenu, nchi hii mtaigawa
vipande vipande na kamwe amani ya kweli haiwezi kupatikana kwa mambo ya
kusingiziana, badala yake tusaidiane sisi kwa sisi, na sisi na
viongozi,” alisema.
Onyo la Malecela limekuja kutokana na mfululizo wa matukio ya uvunjifu wa amani na mpasuko wa kidini unaoanza kujitokeza nchini.
Malecela alieleza wasiwasi wake juu ya tofauti za
kidini katika ibada maalumu ya kuombea amani iliyofanyika katika Kanisa
Anglikana Chiwondo lililoko kijiji cha Hombolo katika Manispaa ya
Dodoma.
Anafuata nyayo za viongozi wa kitaifa walioonya
masuala ya udini kama Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Marais wastaafu, Mwinyi na
Benjamin Mkapa pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na
Frederick Sumaye.
Alisema waliovamia na kupiga bomu kanisani Arusha
ambapo Balozi wa Vatican nchini, Francisco Montecillo Padilla
alinusurika kuuawa, si wajinga na wanaweza kufanya mambo kama hayo eneo
lolote nchini.
“Kujenga nchi ni kazi ngumu sana lakini kuibomoa
ni kitendo cha muda mfupi ambacho kinaweza kufanyika kwa kutumia sekunde
chache ni lazima kuisaidia serikali katika kuitafuta amani,” aliongeza
Malecela.
Malecela ameonya baadhi ya watu kutochukua
sheria mikononi kuhusu yale yanayowapata na badala yake waiachie
Serikali yao kufanya uamuzi wa nini kifanyike ili amani ibaki.
Nasaha za Mwinyi
Kwa upande wake Rais Mstaafu Mwinyi alisisitiza amani idumishwe
na kuwataka Waislamu na Wakristo kupendana na kuvumiliana ili jamii
iweze kuishi bila hofu.
“Haiwezekani dini moja kuitaka dini nyingine
isiwepo,” alisisitiza Mwinyi. Mwinyi alitoa msisitizo huo jana mjini
Kibaha wakati akitoa mawaidha yaliyolenga kusisitiza amani nchini
kufuatia matukio kadhaa yaliyoripotiwa kutokea nchini na kudaiwa
yanahusiana na masuala ya kidini.
Alisema si ajabu kukuta hata sasa baadhi ya watu
wameingiwa na hofu na waumini wakisikia kitu hata kama ni paka
wanakimbia na kuacha maubiri.
“Hakuna sababu ya kutufikisha hapo jamani, mbona
dini hazijaanza leo? Tangu enzi watu wanaabudu kila mtu kwa imani yake,
watu wanaoana, wanakula pamoja, wapo ofisi moja, magari wanapanda pamoja
sasa iweje hii itokee leo hii?” alihoji Mwinyi.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment