HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » MOTO WA BAJETI WAKOLEA, JK KUTETA NA WABUNGE

Rais Jakaya Kikwete.
Wakati Rais Jakaya Kikwete akifikia nusu ya kipindi chake cha pili cha utawala cha miaka mitano na mawaziri wake wakiwasilisha bajeti zao bungeni Dodoma, mwishoni mwa wiki hii atakutana na wabunge wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na mambo mengine kujadili utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya chama hicho kwa kipindi cha 2010-2015.

Mkutano huo utakaofanyika Jumamosi na Jumapili wiki hii, unaitishwa wakati baadhi ya wabunge wa chama hicho wakiwa wanahoji kasi ya utekelezaji wa ilani hiyo, hasa kwa

miradi mikubwa ya miundombinu ambayo ama fedha zimekwisha kutengwa au bado.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jijini Dar es Saalam jana kuwa, Rais Kikwete atakutana na wabunge hao mjini Dodoma wiki hii.


Huu utakuwa ni mkutano wa kwanza wa Rais na wabunge hao tangu aanze utawala wake ngwe ya mwisho baada ya uchaguzi mkuu wa 2010.


Hadi sasa serikali ya awamu nne imebakiwa na bajeti mbili na nusu, yaani ya mwaka 2013/14 ambayo inaendelea kujadiliwa Dodoma kwa sasa, lakini pia kutakuwa na ya mwaka 2014/15 na ile ya 2015/16 ambayo itatekelezwa kwa miezi sita tu na awamu ya nne kabla ya kumaliza muda wake wa utawala Oktoba 2015 baada ya uchaguzi mkuu wa rais na wabunge.


Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM anatarajia kukutana na wabunge wa chama hicho pamoja na mawaziri kujadili utekelezaji wa ilani hiyo.


Nape aliwaambia waandishi wa habari kuwa mkutano huo utawapa wabunge fursa ya kujadili utekezaji wa ilani hiyo ambayo ilikiweka madarakani chama chao katika uchaguzi wa mwaka 2010.


Nape aliongeza kuwa mkutano huo pia utatumika kujadili hali ya kisiasa katika majimbo wanayotoka wabunge wa chama hicho tawala.


“Mwenyekiti kukutana na wabunge siyo mara ya kwanza, awali vikao hivi  vilikuwa vikifanyika kwa siku moja, lakini kikao hicho kitakuwa cha muda mrefu ili kutoa fursa kwa wabunge kutoa  maoni yao kwa viongozi wa chama chao,” alisema.


Nape alisema na kusisitiza kuwa kikao hicho hakitakuwa na uhusiano wowote na kuwadhibiti baadhi ya wabunge wa CCM, ingawa lolote linaweza kujitokeza kwenye kikao nje ya ajenda iliyokusudiwa.


Alisema viongozi wa CCM wanafahamu kuwa hawajakutana na wabunge kwa muda mrefu, hivyo watakuwa na mambo mengi ya kuzungumza na kukishauri chama hicho kutokana na uwakilishi wa majimbo yao.


“Wabunge ni wawakilishi wa wananchi na wanakutana nao mara kwa mara kutambua changamoto zinawakabili ili kuwawakilisha bungeni na muda wa kikao hicho utatosha kutambua utekelezaji wa ilani yetu,” alisema Nape.


Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Rais Kikwete akitoa ahadi nyingi kwa wananchi ambazo hadi sasa hazijatekelezwa.


Miongoni mwa ahadi hizo ni ununuzi wa meli mpya katika maziwa ya Tanganyika, Victoaria na Nyasa.


Ahadi nyingine ni kujenga viwanja vipya vya ndege katika maeneo kadhaa nchini, ujenzi wa hospitali mpya na kuzipandisha nyingine hadhi, ujenzi wa barabara za lami na kupeleka huduma za maji na umeme katika maeneo mengi ya vijijini.


Pia ahadi hizo zilihusu kuifumua na kuijenga upya reli ya kati pamoja na kutekeleza miradi mipya ya kuzalisha umeme.


Miongoni mwa miradi mipya ya nishati ya umeme ambayo CCM kiliahidi kuitekeleza ni uzalishaji wa umeme wa megawati 250 katika mto Rusumo ambao ungetekelezwa kwa pamoja kati ya Tanzania na Rwanda.


Baadhi ya wabunge wamekuwa wakieleza kutoridhiwa na utekelezaji wa ahadi za CCM zilizotolewa kwa wananchi katika kampeni za mwaka 2010 kwamba unasuasua na hali hiyo inaweza kukiathiri chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.


Kwa mfano, Mbunge wa Mwibara, Kangi, Lugola, wakati wa mkutano wa bajeti unaoendelea alisema kuwa utekelezaji wa kusuasua wa ahadi hizo utasababisha wabunge wengi kushindwa kurejea bungeni katika uchaguzi mkuu ujao.
CHANZO: NIPASHE

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: