� Madai ya kuua, kubaka na kupora mali za watu yaongozeka
� Polisi aliyechomewa nyumba aangua kilio mbele ya Nchimbi
Familia ya Mariam Abdllah,Mkazi wa mtaa wa
Mtawike,kata ya Magomeni Mtwara,ikiwa chini ya baada ya nyumba yao
kuteketezwa kwa moto na watu wasiojulikana katika ghasia zilizozuka
ambapo baadhi ya wanachi wanapinga kusafirishwa kwa gesi asilia kutoka
Mtwara kwenda Dar es salaam.
Mkuu wa mkoa huo, Kanali mstaafu Joseph Simbakalia, amethibitisha
kutokea kifo cha mjamzito, Fatuma Mohamed, huku asijue chanzo chake, na
kwamba hana taarifa za vifo vingine.
Naye Kamanda wa Polisi mkoani humo, Linus Sinzumwa, aliwaambia
waandishi wa habari kuwa, watu wawili wamepoteza maisha katika ghasia
hizo. Aliwataja kuwa pamoja na Fatuma, yumo pia Karim Shaibu (22), mkazi wa Chikongola, aliyefariki Mei 22, mwaka huu.
“Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, nina
taarifa ya kifo cha mtu mmoja, mjamzito, mazingira ya kifo chake siwezi
kuyaeleza,” alisema Simbakalia alipotakiwa kufafanua utata huo.
Lakini Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula,
Mohamed Kodi, alisema hadi sasa amepokea maiti mbili, na majeruhi 18
ambao hali zao zinaendelea vizuri.
MADAI YA MAUAJI
Hata hivyo, wananchi wamepinga vikali taarifa za serikali kwa madai
kuwa zimepotosha ukweli, kwa kuwa wananchi waliojeruhiwa na kupoteza
maisha ni wengi na wengine wameshazikwa. Katika kata ya Mikindani, wananchi wamemtaja Mussa Mohamed mkazi
wa mtaa wa Jangwani, kuwa ameuwawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati
wakiendesha doria ya nyumba kwa nyumba.
Said Kajuba, alisema aliyefariki ni ndugu yake na wakati anapigwa risasi, aliona na wametoa taarifa polisi pasipo kupata msaada. Katika eneo la Magomeni-Likombe karibu na kiwanda cha Olamu,
wananchi wamedai kuna watu (hawakutaja idadi) waliouawa, ingawa
hawakuwatambua kwa majina.
BIBI KIZEE ALILIA NYUMBA, WATOTO WAKE
Mkazi wa mtaa wa Mtawike, kata ya Magomeni, Mariam Abdalah, amedai
kuchomewa nyumba na askari waliofika eneo hilo kwa ajili ya kuwakamata
wahalifu.
Mariam alisema wanawe wawili walikimbia na hadi sasa hajui walipo.
“Kama mnavyoona sina pa kuishi, nyumba imechomwa moto, ninalala nje,
nilinunua chakula cha akiba kimeungua chote, wanangu wawili sijui
walipo, nimewaona askari wa kike akiwasha kiberiti kuchoma nyumba yangu
ya nyasi,” alidai.
NYUMBA KUCHOMWA MOTO
Mkazi wa mtaa wa Magomeni Tulivu, Magomba Abdalah, alidai nyumba
sita za wananchi zimechomwa moto na kwamba hasira zao (wananchi)
zilizidi baada ya polisi kufanya hujuma badala ya kuwalinda na kutuliza
ghasia.
“Askari waliofanya vitendo hivi si wa Mtwara mjini wala hatuwajui, ni wageni wameletwa kukabiliana nasi.” “Tunatarajia askari wawe walinzi wa raia ila wamechoma nyumba,
wameiba mali, wametupiga sana, kwa hali hii ni ngumu kuona kuwa ni watu
wema kwetu,” alisema
Aidha, alisema kwa sasa kuna uhasama mkubwa kati ya polisi na
wananchi kwa kuwa sehemu za biashara zinazodaiwa kuchomwa moto na askari
wa jeshi hilo, zilikuwa kitega uchumi cha vijana wasiojua hatima yao
“Serikali inatupeleka wapi, kwenye mtaa wetu askari kachomewa
nyumba, hakuwa na tatizo na mtu, ila hasira za wananchi zimetokana na
polisi wageni kuchoma vibanda na maduka yao, hali si nyepesi kama inavyoonekana, askari wageni wataondoka hawa tunaobaki nao itakuwaje,” alihoji Magomba.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, ametembelea
maeneo yalioathiriwa na vurugu hizo, ikiwamo ofisi za Chama Cha
Mapinduzi (CCM), mahakama ya mwanzo Mikindani na nyumba za
askari polisi watatu.
DIWANI WA CCM AIUMBUA POLISI
Katika eneo la Mikindani, diwani wa kata ya Magengeni, Omary
Nawatuwangu, alisema askari polisi wamehusika kuchoma nyumba za wananchi
na kuharibu mali.
Kutokana na kauli hiyo, Nchimbi, `alimbana’ diwani huyo kwa
maswali, akihoji uhakika wa kuwa polisi wamehusika na kwanini wananchi
walifanya uharibifu wa mazingira ikiwamo kutaka kubomoa daraja.
Diwani huyo kupitia CCM, alisema akiwa nyumbani kwake, walifika
polisi wakimuomba asaidiane nao kutoa magogo yaliyokuwa yamepagwa
barabarani.
Alisema, baada ya hapo aliwaona wakiwasha moto kwenye vibada vya
biashara eneo la kituo cha mabasi cha Mikindani na kuchoma nyumba ya
bibi mmoja anayeishi peke yake.
Nawatuwangu, alisema hadi kufikia jana, baadhi ya watu waliendelea
kukaa misituni kutokana na hofu ya kupigwa ama kuuwawa kwa risasi, kwa
kuwa polisi wanavunja
milango na kukamata wananchi waliopo majumbani.
MSIMAMO KUHUSU GESI
Baadhi ya wananchi wa tarafa ya Mikindani, Mawazo Mtonya, Mzee Issa
Salum Nambanga, Fatuma Mfaume, Said Kajuba, walielezea ukosefu wa ajira
kuwa miongoni mwa vyanzo vilivyochochea vurugu kwenye eneo hilo.
“Kuna Bahari ila haturuhusiwi kuvua hadi uwe na nyavu kubwa,
hatuna shughuli za kibiashara, kupatikana kwa gesi tuliona ni neema
kwetu ila serikali inaleta siasa kwenye hili, hatutakubali tunataka gesi
itunufaishe,” alisema Said Kajuba.
Alisema madai yao kwa serikali ni kuanza ujenzi wa viwanda mkoani
humo, ili wananchi wapate ajira na kipato cha familia na si kusafirissa
gesi hiyo kwenda Dar es Salaam kabla ya kuanza kwa ujenzi husika
“Tunachokiona serikali inataka kutufanyia kiini macho, wanataka
kujenga bomba la gesi kabla ya viwanda na uwekezaji wowote hapa kwetu,
endapo gesi itasafirishwa kwa bomba uwekezaji mkubwa utakuwa Dar es
Salaam nasi tutaendelea kuwa masikini,” alisema Nambanga.
Abidi Salum mkazi wa Mikindani, alisema hawana pingamizi na gesi
hiyo kunufaisha Watanzania wote, lakini viwanda vya kuchakata gesi ni
muhimu vikajengwa Mtwara na gesi safi isambazwe.
“Kama sisi tukihitaji gesi ya kutumia inafuatwa Dar es Salaam,
kwanini wasije kuchukua huku, hatutaki isafirishwe kwa bomba, itakwenda
nyingi,
wakishindwa watumie magari, nyaya au meli,” alisema Salum.
POLISI WANENA, MMOJA ABUBUJIKWA MACHOZI
Baadhi ya askari waliochomewa nyumba na mali kuharibiwa, walisema
hali hiyo imewashtua na wamewatambua baadhi ya raia waliofanya vitendo
hivyo. Mmoja wao, Koplo Philemon, alibubujisha machozi mbele ya Nchimbi,
wakati akielezea tukio la kuharibiwa na kuibiwa mali kwenye nyumba yake.
Hata hivyo, Nchimbi, alimtaka kuwa jasiri kwa kuwa askari anatakiwa kuwa jasiri muda wote. Katika nyumba wa Mwandishi wa TBC, Kassim Mikongolo, ambaye mke
wake ni askari polisi, PC Fatuma Mohamed, ilielzwa kuwa wahusika wa
uhalifu huo walifanya hivyo mara mbili na wametangaza kwa yeyote
atakayemsaidia, watamdhuru kwa kumchomea nyumba.
“Nyumba yangu imechomwa mara mbili, awali tuliokoa baadhi ya vitu,
tumeviweka nje, polisi walipoondoka, wahalifu wakarudi na kuiba kuku
wote, nina baadhi ya vitu vya kuhamishia kwa ndugu lakini wanaogopa,
wahalifu walitahadharisha watakaotusaidia, nyumba zao zitachomwa
moto,”alisema.
SIMBAKALIA NAYE
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Simbakalia,
alisema iwapo itabainika askari polisi wamehusika na vitendo vya
kikatili vinavyolalamikiwa, watachukuliwa hatua.
“Zipo njia nyingi za ofisi za wakuu wa wilaya na mkoa kupokea
taarifa za malalamiko, wanawake au wasichana waliobakwa waje kutupa
taarifa, ikibainia hakuna askari atakayeachiwa kwani vitendo hivyo ni
kinyume na maadili ya kazi zao,” alisema.
Alisema kwa sasa hali ya usalama imerejea na wanawahamasisha wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji.
WAANDISHI WA HABARI WANUSURIKA KIPIGO
Waandishi wa habari walinusurika kupigwa katika eneo la Mkanaledi,
ambako kulikuwa na kundi la vijana waliodai (waandishi) hawaandiki
ukweli na wanaipendelea serikali.
Kutokana na hali hiyo, waandishi hao walilazimika kukimbia, kila mtu akielekea upande wake na wengine kupoteana.
MCT YASISITIZA USALAMA WA WAANDISHI
Mapema katika mkutano na waandishi wa habari, Mkuu wa mkoa wa
Mtwara alipouliza juu ya uwezekano wa kuwapatia ulinzi waandishi ,
alisema Katiba inasema ulinzi ni wajibu wa raia wote, hivyo wajilinde na
kwamba jeshi la polisi halina polisi wa kulinda kila mtu nyumbani
kwake.
Wakati kiongozi huyu akitamka hivyo, tayari Baraza la Habari
Tanzania(MCT) limeshatoa taarifa kwa vyombo vya habari likisisitiza
pamoja na mambo mengine ombi kwa serikali ifanye kila linalowezekana kwa
ajili ya kuhakikisha usalama wa waandishi na raia wengine wote wa mkoa
wa Mtwara.
Pia MCT limetoa rai kwa wamiliki wa vyombo vya habari na
menejimenti zake kuchukua kila hatua za dharura kuhakikisha usalama wa
waandishi wao huko Mtwara.
Lakini pia waepuke kufanya maamuzi ya aina yoyote yanayoweza
kuhatarisha maisha ya waandishi wao walioko huko. Aidha waandishi wawe
waangalifu kuhakikisha hawajiweki katika mazingira hatarishi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment