HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » WARIOBA: IKULU KUGAWANYWA


Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba 


Dar es Salaam: Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema iwapo Mfumo wa Serikali Tatu utaridhiwa na wananchi ni lazima mambo yaliyo ndani ya Muungano yatagawanywa ikiwa ni pamoja na Ikulu ya Rais.
Amesema kuwa kutokana na taifa kufanya mabadiliko ya Katiba ni lazima kuwepo mpangilio wa kugawana mambo mbalimbali yaliyokuwa chini ya Muungano ikiwamo majengo, wafanyakazi, Ikulu, hata vitendea kazi na kwamba utaratibu huo ni kama ule uliotumika wakati Tanganyika na Zanzibar zilipoungana.
Kauli ya hiyo ya Jaji Warioba imekuja siku tatu tangu Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kueleza kuwa Tanzania Bara itaanza mchakato wa kutunga Katiba yake Aprili mwaka 2014 na kumalizika Desemba mwaka huohuo.
Jaji Warioba aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na waandishi waandamizi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwananchi Jumamosi, Mwananchi Jumapili, Mwanaspoti, The Citizen na The Citizen on Sunday, Tido Mhando ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa MCL na Theophil Makunga, Meneja wa Uendeshaji na Biashara MCL.
Swali: Makao Makuu ya Serikali ya Muungano yatakuwa wapi?
Warioba: Ukibadili Katiba wakati wowote ni lazima kuwe na makubaliano fulani.
Unajua Serikali ya Muungano na Tanganyika ilikuwa pamoja, sasa ukianzisha Serikali ya Tanganyika, lazima kwenye mpangilio muanze kugawana hata wafanyakazi kwa kuwa wafanyakazi hao walikuwa ni wa Muungano. Hapo ndiyo mtaamua wafanyakazi gani watakwenda katika Serikali ya Tanganyika, watakaobaki katika Muungano na wale watakaokwenda Zanzibar.
Hata katika majengo hali inakuwa hivyo hivyo, lazima kutakuwa na majengo yaliyokuwa yakitumiwa na wizara mbalimbali na hata Ikulu. Hapo pia lazima myagawanye na kukubaliana viongozi wa Tanganyika watakuwa wapi na wale wa Muungano watakuwa wapi. Lakini, hata vifaa vya kutendea kazi navyo inatakiwa mgawane kulingana na makubaliano yenu.
Suala hili linategemea zaidi mazungumzo ya pande zote mbili, baada ya kukamilika kwa mchakato huu kwa sababu hii iliyopatikana sasa ni rasimu tu, ambayo itajadiliwa na wananchi kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba na baadaye kuwepo kwa kura ya maoni. Wapo watakaokuwa wakihoji kuhusu vyeo, katika hili itakuwa kama tulivyokuwa tukiungana Tanganyika na Zanzibar, wakati huo wapo ambao walikuwa wakuu wa mikoa na wakajikuta wameingia katika Muungano huku wakiwa na vyeo hivyo. Kilichofanyika ni kuendelea tu na nafasi hizo mpaka utakapofanyika utaratibu mwingine kwa njia ya mazungumzo.
Unajua jambo hili siyo jukumu la tume hii, tunaliacha kwa sasa na hatujui litakuwaje kwa sababu ni suala la mazungumzo.
Swali: Majukumu ya Rais yatakuwaje?
Warioba: Rasimu imeeleza majukumu (roles) ya Rais kama mkuu wa nchi, ambaye anakuwa kama taasisi na sisi tulichokifanya ni kujenga taasisi hizo, kwamba ijulikane akifanya chochote awe ameshauriwa, isiwe yeye peke yake.

Kama ni kuteua mawaziri kwanza atashauriwa, hata wakiteua basi apeleke majina aliyoyateua kwenye Bunge, kama ni mtumishi wa umma analazimishwa kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Utumishi wa Umma na hawezi kuteua kutoka nje.
Katika vyombo vya usalama, tumeshauri kianzishwe chombo cha Baraza la Ulinzi na Usalama na hao ndiyo watakaomshauri rais.
Swali: Kwa mantiki hiyo huoni kama bado kutakuwa na mianya ya kupitisha watu kulingana na umaarufu wao au nguvu yao katika jamii?
Warioba: Kama angekuwa anawateua mwenyewe sawa, lakini wateule hao wamepitia katika hatua fulani na aliyeteuliwa atatazamwa sifa zake.
Mfano ni Tume ya Uchaguzi (NEC), tulipokea mapendekezo mengi juu ya nini kifanyike ili iwe huru, lakini tulizingatia suala la sifa za mwombaji kwanza, si jambo rahisi watu kukaa kikao na kupanga nani ashike nafasi hiyo.
Wanaotaka nafasi NEC wataomba na watachunjwa kulingana na sifa zao, baadaye majina yao yatapendekezwa, hivyo Rais hawezi kwenda nje ya jambo hilo. Katika jambo hilo viongozi wengi walipendekeza wanasiasa ndiyo waingie katika Tume ya Uchaguzi. Sisi tuliangalia jambo hili kwa umakini sana sambamba na kuangalia uzoefu wa nchi nyingine, tuliona kwamba mahali popote pale ambapo Tume ya Uchaguzi ina wawakilishi wa vyama vya siasa, kumekuwa na matatizo na siku zote wamekuwa hawakubaliani.
Ndiyo maana tukaweka sifa katika Katiba na kuwa na utaratibu ambapo Rais atateua na orodha atakayopelekewa ndiyo ataitumia kuteua nani awe mwenyekiti, makamu na wajumbe wa tume hiyo, katika hilo sidhani kama vyama vitahusika.
Hata Rais wa Marekani anateua watu wengi, hata kama Bunge lina wabunge wengi wa chama chake anajua wazi kuwa asipopeleka watu wenye sifa wabunge watamkatalia.
Ndiyo maana tunakazania maadili, tunasema Rais ndiyo kiongozi pekee wa nchi aliyechaguliwa na watu wote, lakini kwa sababu ya upungufu wa maadili, hatujawahi kuona ni mtu gani tunaweza kumchagua na tumwamini kuwa atasimamia maadili ya nchi.


MWANANCHI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: