MAGUFULI:WALIOLIPWA FIDIA WAONDOKE


WAZIRI wa Ujenzi Dk. John Magufuli amewataka wananchi waliolipwa fidia katika maeneo inayopita miradi ya ujenzi ya barabara kuondoka haraka kabla hawajaondolewa kwa nguvu.
Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa barabara za jijini Dar es Salaam jana.
Alisema wapo wananchi ambao wamelipwa fidia, lakini kwa kiburi hawataki kuondoka kwa madai kuwa fedha walizolipwa haziwatoshi.
“Serikali hakuna fedha za mchezo, kama kuna mtu anajifanya kuwa yeye ni jeuri basi wajue kuwa serikali ni jeuri kuliko wao,” alisema.
Dk. Magufuli aliwaagiza makandarasi hao kuhakikisha wanaendelea na ujenzi katika maeneo hayo huku akisisitiza kuwa kwa wale waliofungua kesi mahakamani iwapo watashindwa kesi hizo watalazimika kugharamia.

Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini

Alisema makandarasi hao hawawezi kusubiri kesi hizo kwa kuwa hatua ya kuchelewa kukamilisha miradi hiyo inaweza kuchangia kuwepo kwa mgogoro wa kifedha.
Dk. Magufuli akiwa eneo la Mwenge alimueleza Diwani wa Kata ya Magomeni, Julian Bujugo kuwa maendeleo hayaangalii chama bali utekelezaji wa miradi hiyo unaendeshwa kisheria.
“Nakushukuru kwa kuwa wewe ni mwanachama wa CCM na umebomoa mwenyewe, nakushukuru sana,” alisema Dk. Magufuli.
Bujugo alikuwa akidai kuwa hadi hivi karibuni alikuwa hajalipwa fedha zake za fidia, wakati sio kweli.
Akizungumzia mradi wa magari yaendayo haraka (DART), Dk. Magufuli alimtaka mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili mradi huo uweze kukamilika ifikapo mwaka 2015 kama mkataba wao unavyoonyesha.

TANZANIA DAIMA

No comments

Powered by Blogger.