Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesimamia msimamo wake, kutaka serikali mbili, kikipinga mfumo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Hatua hiyo imefikiwa mjini Dodoma katika Baraza la Katiba la chama hicho linalowashirikisha wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Vyanzo vya NIPASHE kutoka ndani ya baraza hilo, vilieleza kuwa sehemu kubwa ya wajumbe waliochangia eneo la muundo wa serikali ya Muungano, walitaka kuendelea na mfumo wa serikali mbili.
“Msimamo wetu (CCM) ni serikali mbili, lakini hizi tatu zilizoletwa tunaziona ni gharama kubwa kuziendesha,” alieleza mjumbe mmoja ambaye pia ni Mbunge kutoka mikoa ya kaskazini.
Tangu kuzinduliwa kwa rasimu ya Katiba Mpya, CCM imekuwa ikisimamia muundo wa serikali mbili ambao hata hivyo, umekuwa ukipingwa na baadhi ya wanachama wake, akiwamo Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mansour Yussuf Himid.
Taarifa zinaeleza kuwa Himid, aliyevuliwa uanachama wake na Kamati Maalumu ya CCM-Zanzibar, amewagawa wajumbe wa Nec kutokana na kuwapo wanaopinga kufukuzwa kwake, wengine wakiunga mkono.
Mmoja wa wajumbe hao kutoka mkoa wa Mjini Magharibi kisiwani Unguja, alisema Himid ana nguvu na ushawishi wa kisiasa visiwani humo, hivyo kumfukuza uanachama itakuwa pigo kwa CCM.
Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini
Pia mjumbe huyo alisema Himid ataendelea kuwa Mwakilishi wa jimbo hilo, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar inayoeleza kuwa ukomo wa Mwakilishi unatokana na mambo kadhaa ikiwamo kujiondoa katika chama cha siasa.
“Huyu mmemfukuza, lakini kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ataendelea kuwa Mwakilishi, hivyo atayasema mambo yenu mengi sana huko,” alisema.
“Huyu anastahili kufukuzwa tu, kwa maana anaenda kinyume cha msimamo wa chama ambao unajulikana kuwa ni serikali mbili,” kilieleza chanzo hicho.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema jana kuwa, sakata la Himid litajadiliwa katika kikao cha Nec, kuwa vile ndicho chenye mamlaka ya kuwathibitisha wagombea wa nafasi hiyo.
Rais Kikwete akiwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, aliongoza kikao cha CC jana asubuhi, ambapo Mwenyekiti na Katibu wa chama hicho mkoani Kagera, Costansia Buhiye na Aveline Mushi walihojiwa kuhusu mgogoro huo.
Wakati viongozi hao wakihojiwa, Mwenyekiti na Katibu wa CCM wilaya ya Bukoba Mjini, Yusuph Ngaiza na Katibu wake Janeth Kayanda pamoja na Meya Amani, hawakuwapo mjini humo, hivyo wakawekwa ‘viporo’.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusitishwa CC kupisha kikao cha Nec, Nnauye, alisema viongozi hao walichelewa kutokana na gari lao kuharibika wakiwa njiani kuja Dodoma.
Hata hivyo, NIPASHE lilimshuhudia Amani akiwasili kwenye ofisi za Makao Makuu ya CCM mjini hapa na kuingia ndani ya ukumbi wa White House palipofanyika kikao cha CC.
Lakini, Amani aliingia ukumbini humo na kutoka nje baada ya takribani dakika tano. Kisha aliondoka.
Akizungumzia hali hiyo, Nape alisema baada ya kuchelewa kwao, Amani, Buhiye, Mushi, Ngaiza, Kayanda na Balozi Kagesheki, wangehojiwa wakati wa mapumziko ya chakula cha mchana.
Hata hivyo, hadi wajumbe wa Nec walipotoka kwa mapumziko hayo saa 10 jioni, hapakuwa na kikao cha CC kilichoketi kuwahoji viongozi hao kama ilivyotangazwa na Nape.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment