Wakati suala la ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) likiendelea kujadiliwa namna ya utekelezaji wa mambo mbalimbali ikiwamo sarafu moja na suala la kisiasa, Baraza la Elimu ya Vyuo Vikuu kwa ukanda huu(IUCEA) linataka taasisi zake zitoe elimu inayofanana.
Msukumo wa kutoa kiwango cha elimu kinachofanana,
unatokana na hali iliyopo sasa kwa wahitimu wa vyuo vikuu katika nchi za
EAC kushindwa kumudu ushindani wa soko la ajira duniani.
Katibu Mtendaji wa IUCEA, Profesa Mayunga Nkunya
anasema mfumo huo utasaidia wahitimu wa jumuiya hiyo kupata taaluma
itakayokuza mahitaji katika soko la ajira duniani.
Akizungumzia mfumo wa elimu wa Tanzania, Profesa
Nkunya anasema ni wa kizamani ambao haimsaidii mwanafunzi anapohitimu
masomo yake.
“Kwetu sisi mtihani ndiyo kigezo pekee cha kumpima
mwanafunzi, kufanya hivyo ni kosa kwa sababu kunawengine wanafeli
lakini wanauwezo mzuri tu kwenye masuala mengine. Tunataka kuwa na mfumo
katika Afrika Mashariki unaoangalia uwezo wa kila mtu” anasema.
Anasema kama nchi hizo zitaendelea na mfumo wa
sasa wa kuchukulia mtihani kuwa kipimo pekee cha kupima uelewa wa
mwanafunzi, zitazidi kupoteza nafasi nyingi za watu wenye uwezo.
Profesa huyo anasema katika nchi za EAC ni Rwanda
pekee ndiyo imebadili mfumo wake wa elimu ambao unatoa fursa kwa kila
mtu kupata elimu bila kuhukumiwa na kigezo cha kufaulu au kutokufaulu
kwenye mitihani.
Anaongeza kuwa nchi zilizoendelea duniani
zimefanikiwa kutoa elimu kwa watu wake kwa sababu kwao mitihani siyo
kigezo cha kupima uwezo wa mtu.
Akizungumzia mpango huo wa IUCEA Msemaji wa Tume
ya Vyuo Vikuu hapa nchini (TCU), Edward Mkaku anasema haoni ubaya wowote
wa mpango huo lakini IUCEA haina mamlaka katika vyuo vikuu vya Afrika
Mashariki kwani kila nchi ina sheria zake katika suala la elimu.
Mkaku anasema ili hatua hiyo ifikiwe, inabidi kila nchi mwanachama wa EAC iafiki kujiunga na mpango.
Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Biashara la
Afrika Mashariki (EABC), Andrew Kaggwa anasema anasema wahitimu wa elimu
ya vyuo vikuu katika nchi za EAC, wana ujuzi mdogo ambao hauwezi
kufanya vizuri kwenye soko la ushindani.
Kaggwa anasema mfumo huo wa elimu utasaidia EAC
kutatua changamoto ya ajira kwa wahitimu wa elimu ya juu kutokana na
kile alichoeleza kwamba wataweza kutengeneza bidhaa zao wenyewe badala
ya kutegemea bidhaa kutoka nje.
Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini
Mkurugenzi huyo anasema wataalamu kutoka Asia, China na Amerika
ndiyo wamejaa katika nchi za EAC kwa sababu watu wa jumuiya hii wamekosa
ujuzi unaowasaidia kumudu kuendesha viwanda na biashara katika nchi
zao.
“Sisi tunawafanyia kazi wenzetu kwa kuwauzia malighafi ambazo wanazileta huku kama bidhaa na kutuuzia tena” anasema Kaggwa.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine
(SUA) mkoani Morogoro, Eliaza Mkuna ambaye anasomea Shahada ya Uzamili
wa Sayansi katika Kilimo na Uchumi, anasema licha ya mpango huo kuwa
mzuri, tatizo lipo kwenye elimu ya chini.
“Jinsi tunavyomuandaa mwanafunzi kuanzia ngazi ya
chini tunatofautina katika nchi hizi tano, ukizingatia Tanzania
tumekumbwa na anguko la elimu kwa siku za hivi karibuni” anasema msomi
huyo.
Anasema kuwa maandalizi ya kutosha yanahitajika
kabla ya mpango huo kuanza kazi. Anasema maono ya kielimu katika nchi
hizi yanatofautiana kutokana na kila moja kuwa na vipaumbele vyake.
“Tanzania tuna ‘Big Result Now’ je tunajua nchi nyingine zina dira gani? Je zinashabihiana?” anahoji Mkuna.
Anasema elimu inategemea vitu vingi ambavyo
vinatofautiana kati ya nchi moja na nyingine ambapo anatolea mfano wa
vitabu vinavyotumika kufundishia katika shule za Kenya ni tofauti na
vile vinavyotumika nchini Tanzania.
Jarida la IUCEA la mwaka jana lilimnukuu Rais wa
Rwanda, Paul Kagame akisema bado nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki
hazijafikia lengo la Umoja wa Mataifa(UN) la kuwa na angalau asilimia 10
ya watu wenye elimu ya kiwango cha chuo kikuu.
Rais Kagame anasema kiwango kilichopo sasa cha asilimia tano hadi saba ni kidogo ukilinganisha na lengo la UN.
Kagame anawataka viongozi wa IUCEA kutekeleza
mipango yao ya maendeleo na kuhakikisha kuwa vyuo vikuu vya EAC,
vinashirikiana katika rasilimali walizonazo ili kufanikiwa kitaaluma na
kitafiti.
Kagame aliongeza kuwa nchi yake na wanachama
wengine wa EAC wanatarajia mipango yenye mashiko inayoakisi mafanikio ya
kuwa na jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika kuhakikisha mchakato huo unatimia Kaggwa
anasema, baraza hilo ambalo baadhi ya vipaumbele vyake ni pamoja na
masuala ya weledi, uwajibikaji, usawa na ubunifu limeandaa kongamano
litakolishirikisha wafanyabiashara, wataalamu na taasisi mbalimbali
litakalofanyika jijini Nairobi mwezi Oktoba mwaka huu.
Lengo la kongamano hilo litakuwa ni kukutanisha sekta za umma na
binafsi ili kujadili namna ya kuboresha sekta ya elimu katika nchi za
EAC.
Baraza hilo linalenga kuunda mtandao wa vyuo vikuu
kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na vya nje ya jumuiya
hiyo. Pia linalengo la kuunda jukwaa litakalokuwa linajadili masuala ya
kitaaluma na mambo mengine yanayohusiana na elimu ya juu.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment