MATUKIO ya uporaji na utoroshaji madini yanazidi kushika kasi
ambapo wafanyabishara wawili wa madini ya Tanzanite jijini Arusha
wamejeruhiwa kwa risasi na kuporwa kiasi kikubwa cha madini yenye
thamani ya zaidi ya sh mil. 60 fedha taslimu huku Ofisa Usalama wa
Uwanja wa ndege mkoani Kigoma naye akitiwa mbaroni kwa kutaka kutorosha
madini.
Matukio hayo mawili yalitokea juzi na jana zikiwa ni siku chache tangu
kuuawa kwa mfanyabiashara bilionea wa jijini Arusha Erasto Msuya
aliyepigwa risasi zaidi ya 20 wilayani Hai mkoani Kilimanajaro.
Wakati hali ikiwa hivyo, wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA)
umetangaza kukamata shehena ya madini yenye thamani ya zaidi ya sh
bilioni 13 katika kipindi cha miezi 10 yaliyokuwa yakitoroshwa nchini
kinyume cha utaratibu.
Katika tukio la jijini Arusha lililotokea jana saa 9:30 alasiri eneo
la Pangani, wafanyabiashara Steven Alex na Abel Mutta walipigwa risasi
na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wakati wakiwa kwenye gari kando ya
barabara walikokuwa wamekuja kununua madini hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alikiri kutokea kwa
tukio hilo lakini akadai asingeweza kulizungumzia kwa vile hakuwa na
taarifa kamili.
Hata hivyo mashuhuda wa tukio hilo, walidai kuwa wafanyabiashara hao
walikuwa ndani ya gari aina ya Range rangi ya Silva ambapo Alex alikuwa
upande wa dereva na Abel alikuwa upande wa pili wakiwa na mtu mwingine
nyuma ambaye hakufahamika jina lake mara moja.
Wakati wafanyabiashara hao wakiwa wameegesha gari kando ya barabara
kusubiri kuwalipa watu waliowauzia madini, zilikuja pikipiki tatu
zikasimama kando ya gari lile na vijana watatu walishuka na bastola
kisha kumsogelea Alex wakimtaka afungue mlango.
“Vijana hao walikuwa wakidai afungue awape hela zao lakini hakufanya
hivyo, ndipo wakampiga risasi tumboni na kwenye paja huku Mutta akipigwa
ya mguuni na kisha walifungua mlango wa gari baada ya kuwajeruhi
wakachukua madini na fedha,” alisema shuhuda mmoja.
Aliongeza kuwa baada ya kufanikisha mpango wao, vijana hao waliondoka
na pikipiki zao ambazo zilifichwa sehemu ya namba za usajili huku kila
mmoja akielekea barabara yake.
Ofisa Kigoma
Mkoani Kigoma, mmoja wa maofisa usalama wa uwanja wa ndege, Clephace
Lukindo, alikamatwa na maofisa wenzake uwanjani hapo akitaka kuvusha
madini ya dhahabu yenye uzito wa kilogramu tisa sawa na thamani ya sh
milioni 400.
Hata hivyo tukio hilo limekuwa likifichwa na uongozi wa uwanja pamoja
na jeshi la polisi mkoani humo kwa kile kinachodaiwa kuwa ofisa huyo
amekuwa akitoa vitisho kwa wafanyakazi wenzake.
Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, ofisa huyo ambaye anadaiwa
kuwekewa mtego na maofisa wenzake wawili baada ya kubaini mpango wake
huo wa kutaka kuvusha mzigo huo kwa kutumia leseni ya kusafirishia
madini ya mtu mwingine.
Taarifa zilidokeza kuwa ofisa huyo licha ya kuwa na leseni hiyo
isiyokuwa ya kwake, hakuwa na nyaraka zingine za kuonyesha alikopata
mzigo, anaupeleka wapi na kiasi chake.
Chanzo hicho kilidai kuwa baada ya kufika eneo la ukaguzi, ofisa
mwenzake, Yusuf Mpame, na polisi Koplo Theophil walimtaka aonyeshe
vibali na nyaraka hizo ili wathibitishe kuwa mzigo huo unasafirishwa
kihalali.
Hata hivyo Lukindo baada ya kuona wenzake wamemshtukia na kutaka
kumkamata alitumia nguvu kumkaba ofisa mwenzake Mpame ambaye alimnyonga
shingo na kisha kung’ata lakini akanusuriwa na wenzake Koplo Theophil na
Jeremiah.
Meneja wa uwanja huo aliyefahamika kwa jina moja la Tesha,
alipotafutwa na gazeti hili alipokea simu lakini alipoulizwa juu ya
sakata hilo alikatika ghafla hewani na alipopigiwa tena hakupokea.
Mmoja wa wafanyakazi wa uwanja huo alilidokeza gazeti hili kuwa
Lukindo alikuwa ayasafirishe madini hayo kwenda jijini Dar es Salaam kwa
ndege ya Shirika la ndege la Tanzania lakini baada ya sakata hilo
alikamatwa na kupelekwa polisi alikoshikiliwa hadi jana.
Majeruhi aliyeumizwa na mtuhumiwa huyo alifikishwa hospitali na
kupatiwa matibabu ya shingo ingawa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma,
Frasser Kashai, licha ya kupigiwa simu mara mbili alikwepa kulizungumzi
tukio hilo akisema anaendelea kulifuatilia.
“Sina taarifa kuhusu tukio hilo unaloliuliza hadi sasa,” alijibu
kamanda lakini alipobanwa aeleze hali ya ofisa aliyejeruhiwa
inaendeleaje alisema hilo bado walikuwa bado wanalichunguza na
likikamilika watalitolea taarifa.
Wakati tunakwenda mitamboni, taarifa zilizotufikia zilisema kuwa ofisa huyo alipewa dhamana na jeshi hilo.
TMAA na utoroshaji
Madini hayo yalikamatwa kwenye viwanja mbalimbali vya ndege nchini
ambapo wakaguzi wa TMAA walishirikiana na Idara ya Uhamiaji, Usalama wa
Taifa, watumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Jeshi la Polisi na
wafanyakazi wa viwanja vya ndege (TAA).
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za wakala huyo jijini
Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TMAA, Bruno Mteta,
alisema madini hayo yalikamatwa kati ya Septemba mwaka 2012 na Julai
mwaka huu katika matukio 23 tofauti.
Alisema kwa mwezi huu tayari wakala huyo amewakamata raia wawili wa
kigeni wakiwa na shehena ya madini wakitaka kutoroka nayo huku
akisisitiza kwamba watapandishwa kizimbani wakati wowote.
“Agosti 20, mwaka huu, tumewakamata raia wawili wa kigeni mmoja
aliyekuwa anasafiri amekamatiwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere (JNIA) akiwa na madini ya vito yenye thamani ya sh milioni
25.32.
“Wa pili amekamatwa akiwa kwenye makazi yake Jangwani Beach hapa
jijini kwa kweli thamani ya madini ya mtuhumiwa huyu haijafahamika,”
alisema na kuongeza kuwa serikali imeyataifisha madini hayo.
Kwa mujibu wa Mteta wafanyabiashara wa kigeni na wazawa wanaruhusiwa
kusafirisha madini hayo kwa kuzingatia utaratibu ili serikali ipate mgao
wake.
Awali, mkurugenzi huyo alisema tangu mwaka 2009 hadi mwishoni mwa
mwaka jana, serikali ilipokea sh bilioni 317.74 ambazo ni mrabaha
uliolipwa na kampuni 10 kubwa za madini hapa nchni.
Alisema hivi sasa wizi wa madini kwenye migodi mikubwa haupo kutokana
na uwepo wa watumishi wa TMAA wanaotoa ripoti ya uzalishaji kila siku na
kwamba wafanyabiashara wa madini wanaoongoza kwa kukwepa kodi ni
wazawa.
Mteta alieleza changamoto zinazowakabili kuwa ni kushindwa kuifikia
mipaka yote inayounganisha nchi jirani (njia za panya) ambazo hutumiwa
na wafanyabiashara wengi kutorosha madini hayo.
Alisema watoroshaji wengi wa madini hayo ni wageni kutoka nchi
mbalimbali ambao wanauziwa madini na Watanzania na kufafanua kwamba kati
ya matukio 23 Watanzania ni wawili.
Alisema tayari kesi tatu kati ya 23 zimesikilizwa na kutolewa hukumu
na kutoa mfano wa kesi ya mgeni aliyekamatwa na madini yenye thamani ya
zaidi ya dola 6,200 za Marekani kwamba alitozwa faini ya sh milioni 1.5
na madini yake kutaifishwa na serikali.
TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment