KAMATI Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inaanza vikao vyake
mjini hapa huku macho na masikio ya Watanzania yakitaka kujua hatima ya
Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani, ambaye anakabiliwa na tuhuma
za ufisadi zilizosababisha mgogoro baina yake na madiwani wanane.
Ajenda ya mgogoro wa umeya mjini Bukoba imelazimika kuingizwa katika
vikao hivyo vya juu baada ya chama makao makuu kusitisha uamuzi wa
Halmashauri Kuu mkoa wa Kagera wa kuwavua uanachama madiwani wanane
wakidaiwa kukisaliti chama kwa kuungana na wenzao wa upinzani wakitaka
kumng’oa meya Amani.
Meya Amani anatuhumiwa na madiwani hao kuwa ameiingiza halmashauri kwenye mikataba mitatu ya kifisadi.
Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh
bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT) haukufuata
taratibu, na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha
malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata
utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani.
Vilevile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh.
milioni 297 zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa
mapato na matumizi ya mradi ya kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa
kituo cha mabasi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Katibu wa NEC,
Itakadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kwa sasa sekretarieti ya chama
hicho tayari inaendelea na vikao ambapo leo mchana Kamati Kuu itakaa
chini ya mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini
Alizitaja ajenda nyingine za vikao hivyo mbali na mgogoro wa umeya
Bukoba kuwa kujadili maoni yaliyokusanywa na chama kuhusu rasimu ya
Katiba mpya na hali ya kisiasa nchini.
Nape alisema kuwa Agosti 24 na 25 mwaka huu, NEC Taifa itaendelea na
vikao vyake ambapo itatoa uamuzi mbalimbali wa mambo ambayo hayakupatiwa
ufumbuzi na Kamati Kuu.
Alisema kuwa Agosti 24, asubuhi, chama hicho kitazindua baraza la
wazee kitaifa ambalo wajumbe wake ni viongozi wakuu wastaafu ambao ni
marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Dk. Salmin Amour,
Amani Abeid Karume na Samuel Malecela na Pius Msekwa ambao walipata kuwa
wenyeviti na makamu wa chama hicho.
Faida na hasara
Vyanzo vyetu vya ndani ya CCM vimedokeza kuwa endapo chama hicho
kitabariki uamuzi wa NEC Kagera na kuwatimua madiwani hao wanane huenda
kikajichimbia kaburi la kisiasa mjini Bukoba kwani kutokana na nguvu ya
CHADEMA itakuwa vigumu kurejesha kata zote.
Hata hivyo baadhi ya madiwani hao wameonyesha wazi kuhamia CHADEMA
endapo watavuliwa uanachama wa CCM kwani hata Mwenyekiti wa CHADEMA,
Freeman Mbowe, amewakaribisha rasmi kuwa watapokelewa kutokana na
ushujaa wao wa kupambana na ufisadi.
Pia uamuzi wa kuwafukuza madiwani hao, unaweza kukifanya chama hicho
kumpoteza mbunge wake wa Bukoba mjini, Balozi Khamis Kagasheki, ambaye
anawaunga mkono. Duru za kisiasa zinadai kuwa madiwani hao
wamemshinikiza ajiuzulu ubunge ikiwa wao wataondolewa.
Lakini uamuzi wa kumtosa meya Amani unaweza kukijengea heshima chama
hicho mbele ya umma kikaonekana kupambana na ufisadi kwa vitendo ingawa
utaleta mpasuko kwa viongozi wake wa wilaya na mkoa.
Hadi tunakwenda mitamboni jana, kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM
ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu alilihakikishia gazeti hili
kuwa meya Amani lazima ang’olewe ili kukinusuru chama.
“Unajua hata tukifumba macho tukamlinda meya na kuwatosa madiwani
ambao kimsingi mimi sioni kosa lao, bado wanaweza kwenda mahakamani
kupinga uamuzi wetu na ndani ya muda huo wa kungoja uamuzi wa mahakama
wakapiga kura na kumwondo meya,” alisema kiongozi huyo aliyeomba
kuhifadhiwa jina lake kwa vile si msemaji wa chama.
CCM Taifa iliagiza madiwani hao wanane waendelee na kazi zao za udiwani kama kawaida, huku wakisubiri uamuzi wa Kamati Kuu.
Nape alifafanua kuwa utaratibu wa kutoa adhabu kwa viongozi wa CCM
walio kwenye vyombo vya dola hasa wabunge na madiwani, uamuzi wa
halmashauri ya mkoa si wa mwisho, kwani unapaswa kupata baraka za Kamati
Kuu ndipo utekelezwe.
Hivi karibuni akiwa mjini Bukoba, Rais Jakaya Kikwete alijaribu
kuingilia kati mgogoro huo kwa kuwataka meya Amani na mbunge wa Bukoba
mjini, Balozi Khamis Kagasheki, kumaliza tofauti zao ili miradi hiyo
iendelee kutekelezwa.
Hata hivyo, ushauri wake ulipuuzwa na madiwani hao pamoja na wenzao wa
CHADEMA na CUF wakisema tatizo si ugomvi kati ya wawili hao bali
wanapinga ufisadi wa meya wao kuingia mikataba ya miradi bila
kuwashirikisha.
Madiwani 15 walisaini hati ya tuhuma za ufisadi dhidi ya meya na
kuiwasilisha kwa Mkurugenzi wa Manispaa, wakimtaka aitishe kikao ili
wapige kura ya kumng’oa tangu mwishoni mwa mwaka jana.
Kati yao wa CCM na kata zao kwenye mabano ni Richard Gaspar
(Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye
pia ni naibu meya (Buhembe), Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa
CCM wa wilaya (Kashai), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi
(Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo) na Dauda Kalumuna
(Ijuganyondo).
Wapinzani waliokuwa wameungana nao ni Dismas Rutagwelela (Rwamisenyi),
Israel Mlaki (Kibeta), Winfrida Mukono (viti maalumu), Conchester
Rwamlaza ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu CHADEMA pamoja na Ibrahim
Mabruk (Bilele), Felician Bigambo (Bakoba) na Rabia Badru (viti maalumu -
CUF).
TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment