HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » WANAFUNZI WALIPISHWA ADA YA KUINGIA DARASANI


Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kibweheri iliyopo Kibamba nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam wamedai kuchangishwa Sh. 300 kila siku mmoja kwa ajili mwalimu kuingia darasani.


Mbali na michango hiyo wanafunzi hao wanakosa huduma ya choo na kujisaidia kwenye mapori huku walimu wao wakiomba msaada wa choo katika shule ya jirani.

NIPASHE Jumamosi ilizungumza na baadhi ya wanafunzi shule hiyo ambao walidai kuwa hulazimishwa kutoa mchango wa Sh. 300 kwa ajili ya kuwalipa walimu wa muda waliletwa shuleni hapo baada ya kukosekana kwa walimu wa masomo ya Sayansi.

Mmoja wa wanafunzi hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema kuwa wanasoma katika mazingira magumu licha ya wazazi wao kuwalipia ada.


Alisema wanapokosa mchango huo wa Sh. 300 huchapwa viboko na walimu hawaingii darasani kwa wakati.

Alisema masomo ambayo walimu huingia mara kwa mara darasani ni ya Kiswahili, English na Historia.
"Kwa sisi wa kidato cha nne kama wametususa vile kiukweli mwalimu wa English, Historia na Civics wana moyo wa kutufundisha," alisema.


Alisema mafunzo kwa vitendo hufundishwa siku za Jumamosi na hulipia Sh 300 wakati siku za kawaida  hawafundishwi mara kwa mara licha ya kukaribia kumaliza kidato cha nne.

Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini

Tatizo lingine ni kukosekana kwa choo, tangu mwezi Aprili mwaka huu na kuwafanya waendelee kuishi katika mazingira magumu huku wakilazimika kujisaidia kwenye mapori na wakati mwingine kwenda kuomba msaada kwenye shule nyingine ya sekondari ya Kibwegeri.

Alisema awali wanafunzi walilazimika kukaa nyumbani kwa wiki mbili kwa ajili ya kusubiri ujenzi wa choo ambacho kilititia kutokana na mvua na mpaka sasa hawajajengewa choo kingine.

Aidha, alisema wanafunzi waliochelewa kulipa ada ya mitihani ya taifa ya kidato cha nne wametakiwa kulipia Sh. 70,000 ambazo hukatwa Sh. 5000 kwa ajili ya nauli ya mwalimu kupeleka fedha hiyo wizarani.

Mmoja wa mzazi wa wanafunzi hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazeti  alikiri kuwepo kwa michango hiyo shuleni hapo.


Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Teddy Lungino, alisema suala la michango hiyo halifahamu.

Alikiri kuwepo kwa tatizo la choo na kwamba hata walimu hulazimika kwenda kujisaidia katika shule jingine.

Lungino alisema inawalazimu kuwarudisha wanafunzi nyumbani kutokana na ukosefu wa ada ya shule kwani hata Afisa Elimu Kinondoni amewajulisha kufanya hivyo.

Mkuu wa shule hiyo, Kaobwe Shumbana, alipoongea na NIPASHE kwa njia ya simu, alikanusha kuwepo kwa michango hiyo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kassimu Majaliwa, alisema utaratibu wa kulipishwa fedha mwanafunzi haupo na kwamba suala hilo halijawahi kutokea.

Alisema mwanafunzi haruhusiwi kurudishwa nyumbani kutokana na kutolipia michango ya shule na serikali imeshawakataza suala hilo na walimu wakuu wanalitambua.

"Aulizwe Afisa Elimu ni kwanini ameruhusu jambo hilo wakati kwenye mkutano mkuu wa mwaka jana uliofanyika Kibaha suala hilo lilikuwa ni ajenda na mimi nilikuwepo tulikubaliana wanafunzi kutorudishwa nyumbani kwa kukosa michango," alisema Majaliwa


Alisema anatambua tatizo la upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na kwamba mazingira hayo hayasababishi mwanafunzi kulipia Sh 300.
CHANZO: NIPASHE

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: