JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
SOMO MUHIMU KWA WADAU
ASIYE RAIA WA
TANZANIA NI NANI?
Maswali mengi yanaulizwa kuhusu uraia, hasa wakati
huu ambapo zoezi la kuwabaini wageni wanaoishi nchini kinyume cha sheria
linaendelea katika maeneo mbalimbali nchini, yakitaka kujua nani hasa ni raia
wa Tanzania.
Kimsingi, masuala ya
uraia duniani kote yanaongozwa na falsafa kuu mbili ambazo ni Haki za Kidamu (Jus
Sanguinis - The rights of blood),
ambapo mtu hupata uraia kutokana na uhusiano wa kidamu na wazazi
wenye uraia wa nchi husika. Hii ina maana kwamba, pamoja na mtu kuzaliwa katika
nchi husika anatakiwa pia kuwa na mzazi ambaye ni raia wa nchi hiyo. Falsafa
hii ndiyo inayofuatwa na nchi ya Tanzania.
Kwa maana nyingine
kuzaliwa pekee nchini Tanzania hakumpi mtu haki ya moja kwa moja ya kuwa raia wa Tanzania, bali mtu atakuwa raia
ikiwa amezaliwa Tanzania na wakati wa kuzaliwa kwake mzazi wake mmoja sharti
awe ni raia wa Tanzania.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFY HAPA CHINI
Falsafa nyingine ni (Jus
Soli - The right of Soil), ambayo mtu
hupata Uraia kutokana na kuzaliwa kwake katika ardhi ya nchi fulani.
Kufuatana na Falsafa hii, mtu hupata uraia kutokana na kuzaliwa katika nchi
husika bila kujali uraia wa wazazi wake.
URAIA WA TANZANIA
Masuala ya uraia nchini
Tanzania yanasimamiwa na Sheria ya Uraia ya Tanzania ya mwaka 1995 Sura 357
kama ilivyorejewa mwaka 2002, pamoja na kanuni zake za mwaka 1997. Sheria
hii imeanisha aina tatu za uraia wa Tanzania ambazo ni;
1.
Uraia wa Tanzania kwa kuzaliwa
2.
Uraia wa Tanzania kwa kurithi
3.
Uraia wa Tanzania kwa Tajnisi, au kujiandikisha.
Uraia
wa Tanzania wa kuzaliwa:
Utambuzi wa nani ni raia wa Tanzania
unazingatia vipindi mbalimbali vya historia ya Tanzania, yaani kabla na baada
ya uhuru wa Tanganyika, kabla na baada ya Mapinduzi ya Zanzibar na baada ya
Muungano wa Tanzania. Pia, mahali
alipozaliwa na alizaliwa na nani kama inavyoainishwa hapa
chini:
Aliyezaliwa Tanganyika kabla ya Uhuru
Mtu aliyezaliwa Tanganyika
kabla ya Uhuru alitambulika kuwa ni raia wa Tanganyika wa kuzaliwa, ikiwa mmoja
wa wazazi wake alizaliwa Tanganyika na anatokana na Raia wa Uingereza, makoloni yake au nchi zilizokuwa chini ya udhamini wa
Uingereza
Aliyezaliwa Tanganyika baada ya Uhuru
Mtu aliyezaliwa Tanganyika baada
ya Uhuru alitambulika kuwa ni raia wa Tanganyika wa
kuzaliwa, ikiwa mmoja wa wazazi wake alikuwa raia wa Tanganyika.
Aliyezaliwa Zanzibar kabla na Baada ya Mapinduzi
Mtu aliyezaliwa Zanzibar kabla na
baada ya Mapinduzi alitambulika kuwa ni raia wa Zanzibar wa kuzaliwa.
Ila, mtu huyo hakutambulika kuwa
ni raia wa zanzibar ikiwa wazazi wake walitokana
na mataifa yafuatayo; Australia, Ubeligiji, Kanada, Ceylon (Sri Lanka),
Ufaransa, Italia, New Zealand, Ureno, Jamhuri ya Ireland, Afrika
Kusini na Marekani.
Aliyezaliwa Tanzania siku na baada ya Muungano wa Tanzania
Mtu aliyezaliwa katika Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania siku na baada ya Muungano, atatambulika kuwa ni raia wa
Tanzania wa kuzaliwa ikiwa mmoja wa wazazi wake ni raia wa Tanzania.
Mtu hawezi kuwa raia wa Tanzania kwa kuzaliwa kama wakati
wa kuzaliwa kwake hapa nchini, wazazi wake wote hawakuwa raia wa Tanzania; au Baba
yake ni Balozi wa nchi ya kigeni na ana kinga ya kibalozi; au mmoja wa mzazi
wake alikuwa ni adui wa nchi ya Tanzania (enemy) na mtoto huyo alizaliwa katika
eneo lililokuwa likikaliwa na adui.
Sheria ya Uraia ya Tanzania Sura 357 ya mwaka
1995 (R.E, 2002) ndiyo sheria pekee inayotambua sheria zote za nyuma,
zilizokuwa zinasimamia masuala yote ya uraia katika vipindi mbalimbali vya
historia ya Tanzania.
Kwa mantiki hiyo mtu yeyote ambaye alikuwa
raia wa Zanzibar au Tanganyika kwa kuzaliwa, kabla ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar tarehe 25/04/1964, ataendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuzaliwa, mara baada
Muungano.
Aidha, mtu yeyote kama hakutambulika kuwa raia
wa Zanzibar au Tanganyika kabla ya Muungano, hatatambulika kuwa ni raia wa
Tanzania mara baada ya muungano.
URAIA WA TANZANIA KWA KURITHI:
Raia wa Tanzania kwa kurithi ni mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania, na
anatambuliwa kuwa raia wa Tanzania kutegemeana na kipindi alichozaliwa na uraia
wa wazazi wake wakati wa kuzaliwa kwake kama ifuatavyo:
Aliyezaliwa nje ya Tanganyika kabla ya Uhuru
Mtu aliyezaliwa nje ya
Tanganyika kabla ya uhuru (akiwa
ametokana na raia wa Uingereza na Makoloni yake au himaya ya Mwingereza)
alitambuliwa kuwa ni raia wa Tanganyika kwa kurithi endapo baba yake alikuwa
raia wa Tanganyika.
Aliyezaliwa nje ya Tanganyika baada ya Uhuru na kabla ya Muungano
Mtu aliyezaliwa nje ya
Tanganyika baada ya Uhuru na kabla ya Muungano alitambuliwa kuwa ni raia wa
Tanganyika kwa kurithi, ikiwa baba yake alikuwa raia wa Tanganyika.
Sheria ya Uraia ya Tanganyika
ya mwaka 1961 haikutoa fursa kwa mama kumrithisha uraia mtoto wake aliyezaliwa
nje ya nchi. Hivyo mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika katika vipindi tajwa hapo
juu hakutambulika kuwa ni raia wa Tanganyika kwa kurithi kupitia mama yake.
Aidha, mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika hakutambuliwa kuwa raia wa Tanganyika kwa kurithi iwapo baba yake
alikuwa raia wa Tanganyika kwa kurithi. Kwa tafsiri rahisi ni kwamba Raia wa
kurithi hawezi kurithisha tena uraia huo kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya
Tanganyika.
Aliyezaliwa nje ya Zanzibar kabla ya Muungano wa Tanzania
Mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar
kabla ya Muungano atakuwa raia wa Zanzibar kwa kurithi endapo baba yake ni raia
wa Zanzibar.
Vile vile, Sheria ya Uraia ya
Zanzibar (The Zanzibar Nationality
Decree, CAP 39, 1952) haikuruhusu
mama raia wa Zanzibar kurithisha uraia kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya
Zanzibar. Kwa maana nyingine, mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar katika kipindi hicho
hakutambuliwa kuwa ni raia wa Zanzibar kwa kurithi kupitia kwa mama yake.
Ieleweke
pia kuwa mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar hakutambuliwa kuwa raia wa Zanzibar
kwa kurithi ikiwa Baba yake alikuwa raia
wa Zanzibar kwa kurithi. Kwa tafsiri rahisi ni kwamba Raia wa Zanzibar kwa
kurithi hawezi kurithisha tena uraia huo kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya
Zanzibar.
Aliyezaliwa nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku na baada ya Muungano wa Tanzania
Mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania
siku na baada ya Muungano atakuwa raia wa Tanzania kwa kurithi endapo mzazi
wake mmoja ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa au kuandikishwa/tajnisi.
Ni
vyema ieleweke kuwa mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania hawezi kuwa raia wa
Tanzania kwa kurithi iwapo baba/mama yake ni raia wa Tanzania kwa kurithi.
Sheria ya Uraia Sura ya
357 ya mwaka 1995 (R.E, 2002) imetoa
fursa kwa mama ambaye ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa, tajnisi/kuandikishwa
kurithisha uraia wa Tanzania kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Tanzania.
Aidha,
mtu yeyote ambaye alikuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kwa kurithi, kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
tarehe 25/04/1964 ataendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
namna ile ile mara baada Muungano.
Mtu
yeyote kama hakutambulika kuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kwa kurithi kabla
ya Muungano, hatatambulika kuwa raia wa Tanzania kwa kurithi mara baada ya
muungano.
Haya
yameainishwa katika Sheria ya Uraia ya Tanzania Na.6, 1995 (Sura 357, Rejeo la
2002) kifungu cha 30.
URAIA WA TANZANIA KWA TAJNISI (NATURALIZATION)
Mtu yoyote ambae siyo raia wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuzaliwa au kurithi anaweza kuomba uraia wa Tanzania wa tajnisi
kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Sura 357 ya mwaka 1995, (R.E,2002).
Kwa mujibu wa sheria hiyo, Mheshimiwa Waziri mwenye
dhamana ya kusimamia masuala ya uraia nchini (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi),
ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kumpa au kutompa uraia wa Tanzania Mgeni
mwenye sifa anayeomba uraia.
Sifa za Kuomba Uraia wa Tajnisi;
Mgeni anaetaka kuomba
uraia wa Tanzania anapaswa kuwa na sifa zifuatazo:
(i) Mwombaji awe na umri kuanzia miaka 18 na uwezo
wa kufanya maamuzi yanayokubalika kwa mujibu wa sheria za nchi,
(ii) Awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa muda wa miezi 12 mfululizo kabda ya kutuma maombi ya Uraia,
(iii) Katika muda wa miaka kumi kabla ya miezi kumi na mbili hiyo awe ameishi
ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kihalali kwa muda usiopungua miaka
saba.
(iv) Awe anafahamu vizuri lugha ya Kiswahili au
Kiingereza,
(v) Awe na tabia njema,
(vi) Awe na manufaa kwa taifa, yaani awe alichangia
na anaendelea kuchangia katika ukuzaji wa uchumi, sayansi na teknolojia na
utamaduni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
(vii)
Awe anakusudia kuishi moja kwa moja ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ikiwa ombi lake la uraia litakubaliwa.
Taratibu za kuomba uraia wa Tajnisi.
Mgeni yeyote mwenye nia ya kuomba uraia wa tajnisi
mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea anatakiwa kufuata taratibu zifuatazo;
(i) Mwombaji anatakiwa
kujaza fomu za maombi ya uraia ambazo zinapatikana katika ofisi zote za Uhamiaji
za Wilaya, Mikoa, Afisi kuu ya Uhamiaji Zanzibar na Makao Makuu ya Uhamiaji Dar
es Salaam.
(ii) Mwombaji anatakiwa
kutoa matangazo ya nia yake ya kuomba Uraia wa Tanzania mara mbili mfululizo
kwenye magazeti yaliyosajiliwa Tanzania.
Mchakato
wa Kushughulikia Maombi ya Uraia
Ili kuhakikisha kuwa
wageni wanaopewa uraia ni wale wenye manufaa kwa Taifa, maombi yote yanapaswa
kupitia na kujadiliwa katika vikao vya Kamati za Ulinzi na Usalama za:
Ngazi
ya Kata au Shehia (kwa upande wa Zanzibar)
Katika ngazi ya Kata au Shehia
anayoishi mwombaji, ambapo atahojiwa na maombi yake kujadiliwa na kikao hicho
na hatimaye ombi lake kupelekwa ofisi ya Uhamiaji Wilaya kwa hatua zaidi.
Ngazi ya Wilaya
Katika ngazi hii, Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Wilaya itajadili maombi ya uraia yaliyowasilishwa kutoka
ngazi ya Kata au Shehia, hatimaye maoni na mapendekezo yake hupelekwa katika
ngazi ya mkoa.
Ngazi
ya Mkoa
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa nayo itajadili
maombi yaliyowasilishwa na kutoa maoni na mapendekezo yake kuhusiana na ombi
husika na hatimaye hutumwa kwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, ambaye atatoa ushauri
na mapendekezo yake kwa Mhe. Waziri mwenye dhamana ya masuala ya uraia wa
Tanzania kwa maamuzi.
Ombi la Uraia wa Tajnisi kwa
Mwanamke aliyeolewa.
Mwanamke mgeni ambaye ameolewa
na raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wowote wa uhai wa ndoa yake,
anaweza kuwasilisha maombi ya uraia wa Tanzania kwa tajnisi.
Ombi la uraia kwa mwanamke aliyeolewa
linatakiwa kuwasilishwa pamoja na viambatanisho vifuatavyo;
(i)Cheti cha ndoa
kilichosajiliwa na Mamlaka husika nchini
(ii) Pasipoti ya taifa lake
ambayo haijaisha muda wake
(iii) Kibali cha kuishi nchini
ambacho hakijaisha muda wake (Hati ya Mfuasi)
(iv) Vielelezo
vinavyothibitisha kuwa mume wake ni raia wa Tanzania.
Ombi la Uraia wa Tajnisi kwa
Mtoto
Sheria ya Uraia ya mwaka 1995 Sura 357 (RE 2002), inatoa fursa kwa mzazi au
mlezi halali wa mtoto (asiye raia) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kumuombea mtoto huyo Uraia wa Tanzania. Baada ya maombi rasmi kuwasilishwa, Waziri
mwenye dhamana ya uraia anaweza kuruhusu mtoto huyo aweze kupata uraia wa tajnisi.
Waziri mwenye dhamana na masuala ya uraia nchini (Waziri wa Mambo ya
Ndani) ndiye mwenye Mamlaka ya mwisho ya kutoa au kutotoa uraia wa Tanzania kwa
mwombaji yoyote kwa mujibu wa Sheria ya Uraia ya mwaka 1995 Sura 357, rejeo la 2002.
Makala hii
imeandaliwa na Timu ya Habari ya Operesheni Kimbunga -




No comments:
Post a Comment