Wiki
moja tangu Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe atishie kuwafukuza
kazi maofisa wa idara za usalama watakaobainika kujihusisha na biashara
haramu ya dawa za kulevya kupitishwa katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Polisi imemnasa raia wa Nigeria, Chubuzo
John, akiwa amebeba dawa hizo zenye uzito wa kilogramu nne.
Chubuzo aliyekuwa akisafirisha dawa hizo kupitia uwanja huo, alikamatwa
muda mfupi kabla ya kutaka kuondoka na ndege ya Shirika la Ndege la
Ethiopia kuelekea Roma, nchini Italia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alithibitisha kukamatwa kwa Chubuzo kwa tuhuma hizo.
Alisema raia huyo wa Nigeria alikamatwa wakati wa ukaguzi wa mizigo
akiwa amefungasha dawa hizo kwenye mikoba yake tayari kuzipeleka nchini
humo.
“Bado hadi sasa hatujafahamu ni aina gani ya dawa za kulevya alizokuwa
akizisafirisha kwenda Roma (Italia). Na hivi sasa tunamshikilia kwa
mahojiano. Huyu Mnigeria alikamatwa na polisi juzi saa 11:45 jioni
akijiandaa kuvusha dawa hizo alizokuwa amezipaki katika mizigo yake,”
alisema Kamanda Boaz.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Hadi jana mchana, polisi walikuwa wamezipeleka dawa hizo kwa Kamishna wa
Dawa za Kulevya nchini, ili kubaini ni aina gani ya dawa za kulevya
zilizokuwa zikisafirishwa kupitia uwanja huo uliopo Wilaya ya Hai,
mkoani Kilimanjaro.
“Hizo dawa tumempelekea Kamishna wa Dawa na yeye ndiye atakayesema
thamani yake ni kiasi gani na ni aina gani ya dawa alizokamatwa nazo
huyu raia wa Nigeria kabla ya kumburuza kortini kusomewa mashitaka
yanayomkabili kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema Kamanda Boaz.
Wiki iliyopita, Dk. Mwakyembe alifanya ziara ya kushtukiza KIA na
kuwaonya maofisa wa idara za usalama pamoja na maofisa wa umma
kutougeuza uwanja huo kuwa uchochoro wa kupitisha dawa za kulevya.
Pia aliwaonya maofisa wa idara ya uhamiaji kutojihusisha na biashara hiyo haramu kwa kuwa siku zao zinahesabika.
Dk. Mwakyembe alisema anatambua wafanyabiashara wa dawa za kulevya
wanaitumia KIA kama njia ya kusafirisha kwenda ughaibuni na kuwataka
wanaoendesha biashara hiyo haramu kuacha kwa kuwa serikali itachukua
hatua kali dhidi yao.
Alisema taarifa zinaonyesha kuwa Watanzania wengi na wageni wanaokamatwa
ughaibuni wakiwa na pasi feki za kusafiria, nyingi huonyesha zimetokea
KIA.
CHANZO:
NIPASHE




No comments:
Post a Comment