Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete anatarajia kuipanga upya safu ya Baraza lake la Mawaziri wakati wowote, huku baadhi ya naibu mawaziri wakipewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kuwa mawaziri kamili.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wake wa kutengua
uteuzi wa mawaziri wanne alioufanya siku tisa zilizopita, mawaziri hao
walishutumiwa kushindwa kuwajibika katika utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza Ujangili.
Ripoti ya kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira iliyoundwa kuchunguza operesheni hiyo, ilieleza
kuwa athari zilizotokana na operesheni hiyo zilisababishwa na wizara nne
zilizokuwa zikiongozwa na mawaziri hao.
Waliong’olewa katika sakata hilo ni Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk
Mathayo David.
Rais Kikwete anafanya mabadiliko ya baraza lake la
mawaziri ikiwa imepita miezi 18 tangu alipowang’oa mawaziri wanane
kutokana na tuhuma mbalimbali.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Historia inaonyesha kuwa Rais Kikwete amekuwa na
utaratibu wa kuwapa uwaziri wabunge ambao amewateua, huku akiwapandisha
naibu mawaziri kuwa mawaziri.
Kwa mujibu wa Ibara ya 66 (1) (e) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyofanyiwa
marekebisho inampa mamlaka Rais kuwateua wabunge 10, mpaka sasa
ameshawateua wanane na kubakiza nafasi mbili pekee.
Kati ya wabunge wanane walioteuliwa na Rais Kikwete, watano walipewa wizara za kuziongoza.
Wabunge hao na wizara zao kwenye mabano ni Shamsi
Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Profesa Makame
Mbarawa (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).
Wengine ni Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na
Madini), na Saada Mkuya na Janet Mbene (wote ni Naibu Mawaziri wa Wizara
ya Fedha).
Kutokana na utamaduni huo, Dk Asha-Rose Migiro
anapewa nafasi kubwa ya kuingia kwenye baraza jipya la mawaziri, kwani
naye hivi karibuni ameteuliwa kuwa mbunge.
Wabunge ambao wameteuliwa na Rais lakini hakuwapa uwaziri mpaka sasa ni Zakia Meghji, James Mbatia na Dk Asha-Rose Migiro.
Waliopandishwa
Pia Rais Kikwete amekuwa na utaratibu wa kuwapandisha baadhi ya naibu mawaziri kuwa mawaziri.
Amefanya hivyo kwa Dk Nchimbi ambaye kabla ya
kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa Naibu Waziri wa Habari,
Vijana na Michezo. Awali alikuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa.
Mwingine ni aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na
Utalii, Ezekiel Maige, ambaye kabla ya kushika nafasi hiyo alikuwa naibu
waziri wa wizara hiyo wakati huo ikiongozwa na Shamsa Mwangunga.
Kagasheki pia alipandishwa kutoka naibu waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi hadi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Rais Kikwete alipoingia madarakani alimpandisha
aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji na Mifugo wakati wa Serikali ya Awamu ya
Tatu, Anthony Diallo kuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo.
Mwingine aliyepandishwa ni William Ngeleja, ambaye
aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, baadaye alipandishwa
kuwa waziri kamili katika wizara hiyo.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
aliteuliwa katika nafasi hiyo baada ya kuitumikia nafasi ya naibu waziri
wa Wizara ya Ujenzi.
Naye aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara,
Dk Cyril Chami, aliteuliwa na Rais Kikwete kushika wadhifa huo baada ya
kuwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko.
Celina Kombani aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), baadaye alipandishwa na
kupewa Wizara ya Katiba na Sheria. Hivi sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Utumishi), ofisi aliyopewa kuiongoza tangu mwaka 2012.
Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Wizara ya
Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo, kabla ya kupewa nafasi hiyo alikuwa
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Wasomi wanasema
Wakitoa maoni yao juu ya uteuzi wa mawaziri baadhi ya wasomi
nchini wameitaka Idara ya Usalama wa Taifa kuhakikisha inapendekeza kwa
Rais majina ya watu wazalendo, licha ya kueleza kuwa tatizo la uongozi
linaathiriwa na mfumo mzima wa utawala.
Mchambuzi wa masuala ya Maendeleo na Sayansi ya
Siasa, Emmanuel Mallya alisema, “Nchi yetu inatakiwa kuwa na viongozi
wazalendo na wanaowatumikia wananchi kutoka ndani ya mioyo yao. Kiongozi
ambaye hata akiondoka leo ataacha taswira ya namna nzuri ya kuongoza.”
Mallya ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria
Tanzania (OUT) alisema kuwa pamoja na kuwa na kiongozi mzalendo, taifa
linatakiwa kuwa na mfumo mzuri wa utawala: “Idara ya Usalama imshauri
vyema Rais katika uteuzi huu.”
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam
(UDSM), Profesa Gaudence Mpangala alisema: “Anaweza kuteua wapya, au
akawapandisha naibu mawaziri kuwa mawaziri. Siwezi kutabiri ufanisi wa
mawaziri kwa sasa maana mfumo wetu wa utawala ndiyo tatizo.”
Huku akitolea mfano Wizara ya Nishati na Madini na
ile ya Maliasili na Utalii, Profesa Mpangala alisema zimekuwa
zikibadilishwa watendaji kila mara, lakini kila anayeingia anaonekana
hafai.
Vigezo vinavyoweza kuzingatiwa kuchagua mawaziri
Iwapo Rais Kikwete atazingatia utaratibu wake wa
kuteua waziri kutoka mkoa ambao waziri aliyeondoka, huenda nafasi
iliyoachwa wazi na Nchimbi italazimika kujazwa na baadhi ya wabunge
kutoka Mkoa wa Ruvuma ambao ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu,
Mhandisi Stella Manyanya, Jenister Mhagama (Peramiho), Vita Kawawa
(Namtumbo) au Mhandisi Ramo Makani (Tunduru Kaskazini).
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni
kuhusiana na uteuzi huo, Manyanya alisema kuwa watu wanaopendekeza jina
la waziri huangalia vigezo vingi, siyo tu taaluma ya mtu au utendaji
wake wa kazi.
“Watu hao hufanya kazi kwa siri kubwa, hata
nilipochaguliwa kuwa Mkuu wa Mkoa sikufahamu hadi dakika ya mwisho,”
alisema Manyanya.
Kwa upande wa nafasi iliyoachwa wazi na Kagasheki,
wabunge kutoka Kagera wanaotarajiwa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha
uwaziri ni Jason Rweikiza (Bukoba Vijijini), Charles Mwijage (Muleba
Kaskazini), Deogratius Ntukamazina (Ngara), na Asumpta Mshama (Nkenge).
Nafasi iliyoachwa wazi na Dk David Mathayo, ambaye
anatokea jimbo la Same Magharibi, mkoani Kilimanjaro, huenda ikampa
Rais Kikwete wakati mgumu kumteua waziri miongoni mwa wabunge wa CCM
waliopo mkoani humo kutokana na idadi yao kuwa ndogo.
Kati ya wabunge watano wa majimbo wa CCM waliopo
Kilimanjaro, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela ndiye pekee
ambaye hajawahi kuteuliwa kushika nafasi ya uwaziri.
Mbunge wa Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe ni Waziri wa Maji,
Mbunge wa Siha, Aggrey Mwanri ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi). Wengine ni Mbunge wa
Moshi Vijijini, Dk Cyril Chami, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na
Biashara.
Naibu mawaziri wanaoweza kupewa uwaziri kamili
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa kama Rais
ataamua kutumia utamaduni wake wa kupandisha naibu waziri kuwa mawaziri
kamili, baadhi ya majina yanayotajwa huenda kuwa mawaziri kamili ni
pamoja na
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Aggrey
Mwanri, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki.
Baadhi ya wabunge ambao majina yao yanatajwa kuwa
huenda wakateuliwa kuwa mawaziri ni Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu
Nchemba na (CCM) na Mbunge wa Kahama, James Lembeli.
Mawaziri waliohimili mitikisiko
Pamoja na kuwepo kwa panga pangua ndani ya baraza
la mawaziri, wapo baadhi yao ambao wamefanikiwa kudumu katika baraza
hilo tangu Rais Kikwete aingie madarakani ambao ni Sofia Simba, Profesa
Mark Mwandosya, Stephen Wassira, Dk Hussein Mwinyi na Dk John Magufuli.
Wengine ni Profesa Jumanne Maghembe, Dk Shukuru Kawambwa, Hawa Ghasia
na Dk Mary Nagu.
Katika baraza la mawaziri lake la kwanza, Rais
Jakaya Kikwete alimteua Sofia Simba kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Utawala Bora, mwaka 2010 alimhamishia Wizara Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto, ambako yupo hadi sasa.
Sofia Simba
Akizungumza na gazeti hili juzi kuhusiana na
changamoto anazokutana nazo na kwanini amefaulu kudumu muda mrefu, Simba
alisema kuwa anafanya kazi katika wizara ambayo haina ushawishi mkubwa
kwa jamii, hivyo watu wengi hawapendi kuifuatilia namna inavyofanya
kazi.
“Idara ya Maendeleo ya Jamii tunafanya vitu
ambavyo havina interest kwa wananchi hasa waandishi wa habari, maana wao
wanapenda kusikia habari za wizi na mambo mengine yanayotokea,” alisema
Simba.
Aliongeza kwamba amekuwa na bahati ya kufanya kazi
na watendaji wenye uwezo mkubwa na kwamba mawaziri walioondoka hivi
karibuni waliangushwa na watendaji wao.
“Kwa bahati mbaya wenzetu (mawaziri walioondolewa) wamepata watendaji ambao ndiyo hivyo tena,” alisema Simba.
Alipoulizwa kama anadhani ataendelea kuwepo kwenye
Baraza la Mawaziri iwapo litafanyiwa marekebisho, Simba alijibu kuwa
kila mbunge ni waziri mtarajiwa, hivyo inategemea Rais Kikwete anataka
kufanya kazi na nani.
Naye, Profesa Mark Mwandosya mwaka 2008 aliteuliwa
kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, mwaka 2010 baada ya kufanyiwa
marekebisho safu ya mawaziri aliteuliwa kuongoza Wizara ya Maji hadi
mwaka 2012 alipoteuliwa kuwa Waziri asiye na wizara maalumu.
Waziri mwingine aliyefanikiwa kukaa muda mrefu na
baraza la mawaziri ni Stephen Wassira, ambaye mwaka 2005 aliteuliwa
kuongoza Wizara ya Maji, kisha mwaka 2008 alihamishwa Tamisemi. Miaka
minne baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano
na Uratibu) nafasi anayoishikilia hadi leo.
Dk Hussein Mwinyi ni miongoni mwa mawaziri
waliofanikiwa ‘kucheza’ namba mbalimbali ndani ya baraza la mawaziri
bila kutoka nje ya uwanja.
Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa waziri
aliyeshughulikia masuala ya Muungano, mwaka 2008 alipewa kuongoza Wizara
ya Ulinzi na mwaka 2012 aliteuliwa kuiongoza Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii.
Kwa upande wake Profesa Jumanne Maghembe, mwaka
2006 aliteuliwa kuwa Waziri wa Kazi, nafasi aliyoishika kwa miaka miwili
hadi mwaka 2008 alipokabidhiwa mikoba ya kuiongoza Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi. Mwaka 2010 alipewa Wizara ya Kilimo, Chakula na
Ushirika kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Maji anayoiongoza hadi hivi
sasa.
Katika baraza la kwanza la Kikwete, Dk John
Magufuli aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, kabla ya kupewa wizara ya
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Mwaka 2010 alikabidhiwa Wizara ya Ujenzi.
MWANANCHI
MWANANCHI




No comments:
Post a Comment