Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.

Said Mwishehe
PANAPO MAJAALIWA ya Mungu, kesho tunaungana na mataifa mengine duniani kusheherekea mwaka mpya wa 2015. Hivyo, kwa hesabu za kalenda ya mwaka 2014, leo hii tunamaliza muda uliobaki kabla ya kuingia mwaka 2015.
Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kuendelea kutupa pumzi yake. Ametujaalia afya njema. Hili ni jambo la kushukuru. Pia nitumie nafasi hii kutoa pole kwa ndugu, rafiki na jamii zetu ambao leo hii hatunao tena. Wametangulia mbele za haki.
Hiyo inatokana na mapenzi yake muumba wa mbingu na ardhi. Tuwaombee dua njema huko waliko.Mbele zao, nyuma zetu. Wakati tunakaribia kuingia mwaka 2015, nitumie nafasi hii kuowambea wale wote wenye kusumbuliwa na magonjwa mbalimbali. Imani yangu Mungu atawaponya na kuwarejesha kwenye afya njema na hatimaye kuendele na ujenzi wa taifa.
Wakati tunajiandaa kuupokea mwaka mpya, kuna mambo mengi ambayo yametokea kwenye mwaka huu wa 2014. Yapo ambayo yametunufaisha kama taifa lakini wakati huo huo yapo ambayo yametufedhehesha.
Mwaka 2014 ulikuwa mwaka wa matukio mengi katika nyanja mbalimbali. Nikiri kuna mambo ya kujivunia na kuna mambo ya hovyo ambayo yametokea kwenye taifa hili ambalo linaendelea na juhudi za kusaka maendeleo yake.
Sote ni mashahidi Watanzania kwa nafasi zao mbalimbali wameendelea na ujenzi wa taifa leo. Wameendelea kudumisha umoja na mshikamano wao. Wameendelea kuungana kupigania maisha yao. Ni watu ambao hawataki kukataa tamaa. Wanafanya kila juhudi kuhakikisha taifa linasonga mbele.
Nikiri kauli
ambayo inaliumiza taifa hili ni kuendelea kuimba wimbo wa "Sisi
maskini". Wimbo ambao kwangu mimi unaniumiza kichwa. Sitaki hata kuusikia.
Sitaki kuusikia kwasababu ni sehemu ya adui wetu wa maendeleo yetu.
Sisi maskini
ni kauli ambayo imetukwamisha kwa miaka mingi sasa. Hata mwaka huu wa 2014,
kauli ya sisi maskini imeturudisha nyuma.
Kujiita kila
siku maskini ndio matokeo yake tunashinda kuishi maisha ya kuendelea kuomba
misaada. Kisa tu nchi yetu eti maskini. Kwangu
naamini sisi si maskini ila huenda tunakosa mipango na usimamizi mzuri wa
kufikia malengo yetu.hili ndilo tatizo ambalo linatusumbua kwa miaka mingi.
Mwaka 2015 ni
mwaka wa kubadili mitazamo na fikra zetu. Tukitumia vema rasilimali zetu,
tutapiga hatua. Kila kitu tunacho.tunachotakiwa ni mipango na usimamizi mzuri.
Tuache akili za kuwa tegemezi kwa kila jambo.
Inashangaza
tunapokuwa na msitu mkubwa wa misitu kama ule wa Sao hili Iringa halafu kijiti
cha kusafishia meno kinatoka China. Ama kweli! Inasikitisha
kuona imefika mahali eti kila kitu lazima kitoke nje. Kasumba hii inatokana na
yale yale ambayo wengi yametutawala kwenye akili zetu kuwa lazima tuwe
tegemezi.
Hatupaswi
kuwa na akili hiyo kwa mwaka 2015. Ni mwaka wa kutafakari kama taifa nini
tufanye ili tusonge mbele. Kwa bahati
mbaya tumekuwa na kundi kubwa ambalo linatumia muda mwingi kupiga soga vijiweni
kwa ajenda ambazo hazina mashiko ya kimaendeleo. Ni rahisi kusikia watu
wanajadili nani kavaa nini. Fulani analula nini?
Wanaojadili
tunapigaje hatua kama taifa ni wa chache. Hata hao tunaowategemea kutupigania
wamekuwa wa kuishi kwa matukio. Likija tukio hili wamo, likija lingine
wamo.Mafundi wa kuongoa kuliko kutenda. Inasikitisha
sana.Tumeyaona hayo mwaka 2014.Si vizuri yakajirudia tena mwaka 2015. Kufanya
kosa si kosa ila kurudia kosa, ndio kosa. Tusimamie kama nchi tuangalie maisha
yetu. Tumetoka wapi na tunakwenda wapi.
Tukisoma
vitabu vya historia tunaambia Tanzania na China zilianza harakati za kusaka
maendeleo mwaka mmoja. Nenda leo China kaingalie. Hatufanani
nayo kwa namna yoyote ile.Watu tulianza nao kwenye harakati za kutafuta
maendeleo, eti leo tunawapigia magoti kuwaomba msaada. Wachina
wameijenga nchi yao.Wameamua kusimama kidete kuhakikisha taifa lao linapiga
hatua na kuwa lenye nguvu duniani. Sishangai Marekani inapokwenda kuomba
misaada ya kifedha China.
Kwetu sisi
maendeleo yetu yamekuwa ya mwendo wa kinyonga. Wananchi wamekata tamaa ya
maisha. Kila kukicha wanasema afadhali ya jana. Ndio maisha ambayo tumeamua
kuishi. Imefika
mahali Wachina wameamua kuja nchini kwetu na kufanya kazi ambazo tumeshindwa
kuzifanya. Nenda Kariakoo jijini Dar es Salaam, Wachina wanauza maua.Wanauza
karanga.
Inasikitisha
inapofika mahali hata karanga tunashindwa kuuza. Tunasibiri Wachina waje wauze.
Halafu tumebaki kupiga kelele tu.Tumefika mahali pabaya. Sifa ya taifa
kupiga hatua za maendeleo linahitaji kuwa na siasa safi, utawala bora, ardhi na
watu.
Nikiri
tunaweza kuwa tumekosa siasa safi na uongozi bora lakini tuna ardhi ya kutosha
na watu. Kwa bahati mbaya watu wapo lakini kasi ya maendeleo haiendani na idadi
yetu. Kitendo cha
kukosa siasa safi imefika mahali, wanasiasa wengi wametugeuza kama vile kichwa
na mwendawazimu. Wanatuongopea watakavyo.
Wanajua
hatuna tunaloweza kulifanya. Hakika mwaka 2014, licha ya kufanya mambo ya
maendeleo, yapo ambayo tunapaswa kujiepusha nayo mwaka 2015. Msomaji wa
safu hii, baada ya kutoa maelezo hayo ambayo kwangu mimi kwa siku ya leo ni
kama utangulizi sasa nije kwenye ajenda yangu ya Jumatano ya leo.
Ajenda
yenyewe ni hili sakata la Escrow.Sakata ambalo limekuwa gumzo kwenye kila kona
ya nchi yetu. Limekuwa likizungumza na kila mtu. Kama hulizungumzi wewe basi
analizungumza mwenzio.
Sakata la
Escrow limetikisa nchi yetu kwa sehemu kubwa. Sote tunafahamu mjadala huo wa
Escrow unatokana na utata wa fedha wa sh. bilioni 306 zilizopo kwenye akaunti
ya Tegeta Escrow, wajanja kuamua kuzichukua.
Wanasiasa wa
kada mbalimbali wamekuwa wakilizungumza hilo kwa kina. Wamekuwa wakipambana kwa
hoja. Wamekuwa wakijadili na kuelezea umma kuhusu fedha hizo. Nikiri mwaka
2014, mjadala wa Escrow kwangu mimi naona ulikuwa ni mjadala uliochokuwa sehemu
kubwa ya mazungumzo kuliko mijadala mingine.
Ni kweli
kulikuwa na mjadala kuhusu Katiba mpya lakini ujio wa sakata la Escrow
umefunika kabisa mazungumzo ya Katiba inayopendekezwa. Kwa kuwa hata
wanasiasa wetu nao wanaishi kwa matukio. Wengi wao wameachana na ajenda ya
Katiba mpya ambayo wananchi wanahitaji kuelimisha licha ya wao wenyewe
kujisomea Katiba inayopendekezwa kabla ya kufanya uamuzi kwa kupiga kura ya
ndio au hapa.
Leo hii ili
mwanasiasa aonekane amezungumza jambo la maana basi anaamini akizungumzia
Escrow ndio nyota ya siasa inasafishika. Sina tatizo
na wanasiasa ambao wamelizungumzia sakata hilo hadi hapa lilipofikia. Tunajua
Bunge limetoa maazimio nane kwa Serikali.
Maazimio
ambayo kwa sehemu kubwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete inatakiwa kuamua kwa
kuchukua hatua dhidi ya wanaohusishwa na uchotaji fedha wa Escrow. Ndio maana
aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema ameamua kuachia
ngazi. Uamuzi huo
unatokana na ukweli kwamba ushauri wake kisheria hakueleweka. Jaji Werema
anasema amechafua hali ya hewa.
Pia
tunafahamu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi naye
amsimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi. Kisa sakata hilo hilo la Escrow.
Nani ambaye
hafamu kama aliyekuwa Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa
Anna Tibaijuka naye ametemwa kwenye baraza la mawaziri.
Kilichomuondoa
ni kupokea fedha za Escrow.Prof. Tibajuka aliwekewa kwenya akaunti yake binafsi
sh. bilioni 1.6.
Wakati
mjadala huo unaendelea, hakuna mwanasiasa ambaye ameweza kupata ujasiri wa
kuliambia taifa fedha hizo ni za umma au si za umma. Nani mwenye fedha hizo?. Ujasiri ambao
wanasiasa wetu walio wengi wanao hadi sasa ni kwamba sh. bilioni 306 za Escrow
ni za umma. Wamesema hivyo wakiwa bungeni na wanaendelea kusema hivyo nje ya
Bunge.
Kwangu mimi
na hata kwa Watanzania wengine, nimefurahishwa na hotuba ya Rais Kikwete.Hotuba
ambayo aliitoa Desemba 22 mwaka huu. Alikuwa anazungumza na wazee wa mkoa wa Dar
es Salaam. Kama kiongozi
wa nchi ameonesha kulifahamu vema suala hilo. Akatumia nafasi hiyo kuelezea
historia nzima ya sakata la Escrow.
Akaeleza
namna ambavyo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na IPTL walivyokuwa wanalipa. Pia, akaeleza
namna ambavyo akaunti ya Tegeta Escrow iliovyofunguliwa hadi hatua ya IPTL na
wanahisa wenzake kuuziana hisa na kisha kufunga akaunti ya Tegeta Escrow na
kuchukua fedha zilizomo.
Rais Kikwete
baada ya kutoa maelezo mengi ya kueleweka pengine kuliko yale yaliyokuwa
yanatolewa na wanasiasa walio wengi akatumia nafasi hiyo kuwahakikishia
Watanzania kuwa fedha hizo ni za IPTL. Rais Kikwete
katika hotuba yake alisema"Fedha hizo ni za IPTL maana ni malipo ambayo
yalikuwa yanalipwa kutoka Tanesco ambazo ni tozo la uwekezaji, lakini toafuti
yake fedha zilikuwa zinawekwa kwenye akaunti maalumu".
Kimsingi
hotuba ya rais imejibu swali la msingi ambalo Watanzania wengi walikosa
kulisikia.Pamoja na kusema fedha hizo ni za IPTL bado akauthibitisha umma kuna
kodi ya Serikali ndani yake. Hivyo
tunapoumaliza mwaka 2014, naamini rais amesema kile ambacho wengi tulipaswa
kukisikia.Akasisitiza uchunguzi ufanyike na kisha sheria ichukue mkondo wake. Akaagiza
mamlaka zinazohusika na uchunguzi zitakapokamlisha taarifa , yeye atakuwa na
uamuzi wa kufanya.
Baada ya
kulifafanua kwa kina suala hilo, rais akatumia nafasi hiyo kuweka wazi Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amemuweka kiporo. Bwana we! kauli hiyo ya Prof.Muhongo
kuwekwa kiporo imeamsha hasira za wanasiasa hasa za wapinzani. Wametoa matamko ya kumtaka Rais
Kikwete kumuwajibisha Prof.Muhongo kwa kumuondoa kwenye nafasi hiyo.
Wengine
wametangaza kufanya maandamano nchi nzima.Najiuliza sababu za msingi za
kufanya maandamano hayo. Najiuliza
hivi wanaotaka Prof.Muhongo aondolewe kwenye nafasi hiyo ni kweli wanashinikiza
kwa maslahi ya Taifa au kwa maslahi binafsi.
Hapa kuna
siri kubwa, ambayo wenye kumshinikiza rais amuondoe Prof.Muhongo kwenye nafasi
ya uwaziri wanaijua. Nani ambaye hajui kazi ambayo imefanywa na Prof.Muhongo
kwenye wizara hiyo. Amefanya
mambo makubwa kwa maslahi ya nchi.Waziri Muhongo kwa usimamizi wake mzuri umeme
umekwenda kwenye vijiji mbalimbali vya nchi yetu.
Nimezunguka
wilaya za nchi hii 129 hadi sasa.Naiona kazi ambayo Prof.Muhongo ameifanya
katika nishati ya umeme. Nani ambaye
hajui umuhimu wa nishati ya umeme kwa wananchi. Misimamo yake katika wizara
hiyo imefanikisha ujenzi wa bomba la gesi.Angekuwa Waziri legelege , bomba la
gesi kutoka Mtwara kuja(kwenda) Dar es Salaam lisingejengwa.
Alijua
anasimamia maslahi ya taifa.Pia najua kwenye eneo la gesi amekasirisha
wengi.Wapo ambao hawataki hata kumsikia.Leo si wakati wake kuzungumzia hilo. Wanasiasa wanataka rais amuondoe
Prof.Muhongo, hivi waziri mwingine ambaye atakwenda kwenye wizara hiyo na kukaa
kwa miezi nane iliyobaki ya utawala wa rais Kikwete anakwenda kufanya jambo
gani kubwa.
Kuna dhambi
gani Waziri Muhongo akiachwa amalizie muda ambao Rais Kikwete ameubakisha. Kwa kuwa tunaingia mwaka 2015, ni
bora niseme ukweli maana utaniweka huru.Naamini sioni sababu ya kumuondoa
Waziri Muhongo Wizara ya Nishati na Madini.
Tangu amekuwa
Waziri wa Nishati na Madini Waziri Muhongo amefanya kazi kubwa na nzuri.Hata
hao ambao leo wanamuandama wanajua. Nikiri najua, haya ninayoeleza kuna watu nawakera lakini ni bora
niwe huru kwenye kile ninachoamini.
Kauli ya
Mwishehe, kaushauri Rais wangu, Rais Jakaya Kikwete , nakuomba umuache Waziri
Muhongo amalizie kazi anayoifanya kwenye wizara hiyo.Binafsi sioni mahali
ambapo Waziri Muhongo amechukua fedha za Escrow.
Sioni mahali
ambapo Waziri Muhongo ameshauri fedha zitoke. Waziri Muhongo msimamo wake
unajulikana wazi kuhusu fedha hizo. Kwa bahati mbaya wanasiasa wetu wameng'ang'ania tu kumtaka rais
amuondoe Muhongo badala ya kutoa suluhu ya nini kifanyike ili hayo ambayo
yanatokea na kusababisha taifa kushindwa kuchukua kodi yake yasijirudie.
Wanasiasa
wanashindana kuita vyombo vya habari kumshinikiza rais kumuondoa Waziri
Muhongo. Naamini na
ndio ukweli wanafanya hivyo si kwasababu ya maslahi ya taifa , bali wanafanya
hivyo kwa msuko mwingine. Ipo siku nitausema.Kwenye hili nitasimamia ukweli.
Kwenye siasa
za Tanzania kuna mambo huwa yanakera sana. Moja ya mambo yanayokera ni pale mtu
anaposimama kujifanya anapigania maslahi ya taifa kumbe, kichwani kwake anawaza
tofauti. Kuna wakati
huwa najiuliza kwanini , wanashinikiza Prof. Muhongo aondolewe. Nawaza weee ,
lakini napata majibu tofauti tofauti. Moja ya jibu ambalo huwa nalipata ni
kwamba wanaogombea urais nao wana yao kwenye hilo.
Tena si wa
CCM tu, bali hata wa upinzani. Wanaona sakata la Escrow ni karata ya mwisho ya
kufanikisha malengo yao. Wengine
wanaamini kupitia sakata hilo itakuwa njia rahisi ya kuiangusha Serikali ya
Rais Kikwete bungeni.
Hivyo, kila
mmoja analiangalia kivyake na si kweli wote wanaopigania hilo ni kwa ajili ya
maslahi ya taifa. Ingekuwa ni maslahi ya taifa wangetuambia kwenye sh. bilioni
306 za Escrow za umma ziko sh. ngapi? Nimalizie kwa kueleza tunaingia mwaka 2015, tudumishe upendo, umoja
na mshikamano wetu. Najua wapo ambao watakaosema nimetumwa. Sijatumwa.
Sitajali.
Kubwa zaidi
kila Mtanzania ana haki ya kutoa maoni yake kwa kile anachokiamini anaweza
kuchangia alau kidogo hasa kwa kuzingatia mwaka 2014 umebakisha saa chache tu
wa uhai wake. Karibu mwaka
2015, nitumie nafasi hii kuwataka mafanikio mema kwenye mwaka wa uchaguzi
wanasiasa wote. Mwaka ambao kila anayetaka kugombea udiwani, ubunge au urais
anarudi kuomba kura kwetu.
Nawaheshimu
wanasiasa wote na wa vyama vyote. Kwenye ukweli nipo pamoja nanyi na kwenye
uongo nitakuwa kando yenu.
Tuwasiliane
0713833822
No comments:
Post a Comment