Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto meza kuu), Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Injinia Hamad Masauni (kulia meza kuu) wakifurahi jambo pamoja na Watendaji Wakuu wa Idara ya Uhamiaji (kushoto) na Wakuu wa Idara wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (kulia), wakati wa kikao cha kujadili masuala mbalimbali ya utendaji kazi ndani ya Idara hiyo na Wizara kiujumla. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Wakwanza upande wa kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Simba Yahya, na wakwanza upande wa kushoto ni Kaimu Kamishna wa Uhamiaji, Victoria Lembeli. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mhe. Charles Kitwanga ameagiza yafanywe mabadiliko makubwa katika Vitengo
mbalimbali vya Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma na kuimarisha uadilifu
katika Vitengo hivyo.
Mheshimiwa Kitwanga ametoa
maagizo hayo leo wakati alipofanya kikao na Viongozi wa Idara ya Uhamiaji
ambapo pia kilihudhuriwa na Viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
wakiwemo Wakuu wa Idara na Vitengo vya Wizara.
Kikao hicho kilifanyika katika Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi.
Katika kikao hicho, Mheshimiwa
Kitwanga ameagiza watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji walioko Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Kilimanjaro, wahamishwe na kupelekwa maeneo mengine nchini, wakiwemo wale wa
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Wengine watakaohamishwa ni
kutoka Kitengo cha Pasipoti, Uhasibu, Hati za Ukaazi na Kitengo cha Upelelezi,
vyote vya Makao Makuu ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.
Aidha ameagiza pia kuwa Wakuu
wote wa Vitengo vya Upelelezi vya wilaya zilizopo jijini Dar es Salaam, na pia
wale wa Vituo vya Tunduma, Mtukula, Holili na Kasumulo, wahamishiwe maeneo
mengine, na pia watumishi wote waliokaa kwa zaidi ya miaka mitatu katika Vituo
hivyo.
Amesema hatua hii
inayochukuliwa sasa ni mwanzo tu wa
mabadiliko makubwa yatakayofanywa katika Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma
zinazotolewa na Idara hii ambayo ni moja ya Idara muhimu za Serikali.
Amesema katika kuisafisha
Idara hii, uangalifu mkubwa utachukuliwa ili kuhakikisha kuwa hakuna mtumishi
anayeonewa wala kupendelewa, lakini lengo kubwa ni kuvunja mtandao wa wapokea rushwa na wale
wasiowajibika.
Amesema kufuatana na utafiti
uliofanywa hivi karibuni umeonyesha kuwa matatizo ya rushwa katika Idara ya
Uhamiaji yanashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 30, asilimia 20 ni
uongozi mbovu na asilimia 20 ni matumizi mabaya ya madaraka. Asilimia 15
inahusisha vitendea kazi wa mifumo hafifu ya kufanya kazi, asilimia 10 huduma
mbovu na asilimia 5 ukabila na upendeleo.
Amewataka Viongozi na watumishi
wote wa Idara ya Uhamiaji kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na
maadili ya kazi na waepuke vitendo vya kupokea rushwa na kusaidia wahamiaji
haramu na wauza madawa ya kulevya.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
23
Februari, 2016
No comments:
Post a Comment