HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » LEO KATIKA HISTORIA: MTAMBUE HAYATI RASHIDI MFAUME KAWAWA ALIYEPEWA JINA LA "SIMBA WA VITA"

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Hayati Rashidi Mfaume Kawawa alizaliwa tarehe 27 Mei 1926 katika kijiji cha Matepwende, Wilaya ya Songea, Mkoani Ruvuma, Tanzania. Alianza elimu ya msingi huko Liwale, Lindi mnamo 1941 - 1942 na kuendelea na masomo ya sekondari katika shule ya Dar es Salaam Secondary School. ambapo mmojawapo wa wanafunzi wengine ni marehemu mzee Kanyama Chiume mpigania uhuru toka Malawi aliyeishi uhamishoni nchini Tanzania kwa muda mrefu. Wengine katika shule hiyo wakati huo ni pamoja na kina Abdul Sykes, Ali Sykes, Hamza Aziz na Faraji Kilumanga.


Aliendelea na masomo yake huko Tabora Boys kati ya 1951-1956. Alikuwa ni Waziri Mkuu wa Tanganyika mwaka 1962 wakati Mwalimu Nyerere alipoamua kwenda mikoani kujenga chama na kufanya shughuli za kisiasa. Baadaye aliteuliwa tena kuwa Waziri Mkuu mwaka 1972-1977, Makamu wa Pili wa Rais na Waziri wa Ulinzi na JKT 1977 mpaka 1980. Alikuwa miongoni mwa wahamasishaji wakubwa wakati wa vita ya kumng'oa nduli Idi Amin ambapo alitembelea wapiganaji wetu waliokuwa mstari wa mbele kule Uganda. Hii ilimpatia jina la "Simba wa Vita" jina ambalo lilimkaa vyema kwa muda mrefu.



Kabla ya kuingia katika harakati za kupigania Uhuru Mzee Kawawa alikuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa Shirikisho la Wafanyakazi mwaka 1955 ambapo alichaguliwa kuwa Katibu wake Mkuu wa kwanza. Ni katika nafasi hii ndiyo aliweza kuanza kushiriki kwa nguvu zaidi katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika akihamasisha wafanyakazi. Kabla ya hapo alikuwa ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi wa Serikali. 
Februari 1956 Mzee Kawawa aliacha kazi yake ya Shirikisho la Wafanyakazi kutokana na kuwa mwajiriwa wa serikali kitu ambacho kilimkataza kuhusisha na siasa na kuamua kuingia katika harakati za kudai uhuru kupitia TANU. Alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya TANU mwaka 1957, Makamu mwenyekiti wa TANU mwaka 1960.

Mwaka 1964 baada ya Muungano Mzee Kawawa alikuwa ni Makamu wa Pili wa Rais akiwa ni msaidizi wa Rais wa Muungano kwa upande wa mambo ya Bara. Pia anakumbukwa na Watanzania kutokana na harakati zake katika utekelezaji wa majukumu ya chama na Serikali ngazi ya kitaifa na kimataifa. Miongoni mwa kumbukumbu hizo ni pale aliposimamia kikamilifu uanzishwaji wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Julai 10 mwaka 1963, baada ya kufanyika uamuzi sahihi wa viongozi.

Kuanzishwa kwa JKT kulitokana na mawazo ya hayati Mzee Kawawa ‘Simba wa Vita,’ baada ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, wakati huo Gold Meir, katika sherehe za uhuru nchini Ghana.
Katika siasa amewahi kushika nafasi mbalimbali ikiwemo ile ya Ukatibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi na Makamu Mwenyekiti wa CCM na amekuwa mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu ya CCM. Mzee Kawawa alikuwa ni mtoto wa kwanza kati ya watoto nane na mojawapo ya kazi zake za awali ilikuwa ni uchezaji wa filamu za uhamasishaji na akawa ndiye mcheza filamu wa kwanza kiongozi mweusi. Simba wa Vita,

Mzee Rashidi Mfaume Kawawa, alifariki dunia tarehe 31 Desemba 2009 katika hospitali ya taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam. Alikuwa mwanasiasa mashuhuri katika historia ya Tanzania. Pia alikuwa mcheza sinema, aliigiza katika sinema Muhogo Mchungu.

Mola ailaze roho yake mahala pema peponi. Amina.

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: