Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
Serikali ya Tanzania imetoa tamko
kuwa kwa sasa haina mpango wowote wa kuteketeza meno ya tembo yaliyohifadhiwa
ambayo yametokana na vitendo vya ujangili na vifo asilia vya tembo.
Tamko hilo limetolewa hivi karibuni
na Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Balozi
wa Marekani hapa nchini Bw. Mark Childress alipotembelewa na balozi huyo ofisini
kwake kujadili maendeleo ya sekta ya Maliasili mchini.
Prof. Maghembe alisema hayo baada
Balozi huyo wa Marekani hapa nchini kutoa pendekezo kwa Serikali ya Tanzania
kuchoma sehemu meno ya tembo yaliyohifadhiwa ili kutoa ujumbe mzito duniani juu
ya dhamira ya Serikali kukomesha biashara hiyo haramu.
"Naomba niweke wazi kuwa kwa
sasa hatupo tayari kuteketeza meno haya, tunaweza kuyatumia kwenye tafiti za
kisayansi au vielelezo kwa ajili ya kesi za ujangili ambazo zipo mahakamani na
nyingine ambazo bado zinafanyiwa uchunguzi" Alisema Prof. Maghembe.
Zipo nchi mbalimbali duniani ambazo
zimechukua hatua ya kuteketeza meno yake ya tembo yaliyohifadhiwa ikiwemo nchi
jirani ya Kenya na Malawi ambapo inaaminika kuwa kufanya hivyo ni njia mojawapo
ya kushawishi Ulimwengu kukomesha biashara hii haramu ya meno ya tembo.
Nchi nyingine ni Chad, Ubelgiji,
Ufaransa, China, India, Marekani na Ureno. Kwa upande wa nchi ambazo zina
msimamo sawa na Tanzania katika kuendelea kuhifadhi meno yake ya Tembo ni
pamoja na Afrika ya Kusini, Botswana na Zimbabwe.
Akizungumzia kuhusu kuendeleza sekta
ya Maliasili nchini, Prof.Maghembe amemuomba Balozi wa Marekani Bw. Mark Childress
kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukuza sekta hiyo kwa kuleta
wawekezaji mbalimbali kutoka Marekani kuja kuwekeza Tanzania pamoja na kusaidia
kwenye mapambano dhidi ya Ujangili.
Aliongeza kuwa Tanzania ina fursa
nyingi ambazo zinahitaji uwekezaji mkubwa ikiwemo hoteli za kitalii, fukwe za
kisasa na kuendeleza vivutio mbalimbali vilivyomo hapa nchini.
Prof. Maghembe amemshukuru balozi
huyo kwa misaada mbalimbali kutoka Serikali ya Marekani ya kuendeleza sekta ya
Maliasili nchini ukiwemo wa hivi karibuni wa mbwa maalum (Snifer Dogs) kwa
ajili ya kusaidia utambuzi wa rasilimali za Maliasili zinazoweza kutoroshwa nje
ya nchi kupitia bandari na viwanja vya ndege.
Katika taarifa iliyowasilishwa kwenye
kikao baina ya Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe na Balozi wa Marekani
hapa nchini Bw. Mark Childress imeonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita Serikali ya Marekani imetoa misaada mbalimbali ambayo jumla yake ni
dola za kimarekani Milioni 41.35 katika kusaidia eneo la uhifadhi hapa nchini.
Akizungumzia mahusiano baina ya
Tanzania na Marekani Balozi Mark Childress alimueleza Prof. maghembe kuwa
Serikali ya Marekani itaendeleza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi hizi
mbili ambapo pia ofisi yake ya ubalozi imeshatafuta wadau mbalimbali ambao wapo
tayari kusaidia fedha, vifaa na mafunzo kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi na mapambano
dhidi ya ujangili.
(Na Hamza Temba - Wizara ya Maliasili na Utalii)
(Na Hamza Temba - Wizara ya Maliasili na Utalii)
No comments:
Post a Comment