HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » SPIKA AWANG’OA WENYEVITI WATANO WA KAMATI ZAKE KUTOKANA NA TUHUMA ZA RUSHWA

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Spika John Ndugai amefanya mabadiliko ya wajumbe 27 wa Kamati za Kudumu za Bunge yaliyowang’oa wenyeviti watano, huku mmoja akipoteza nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bunge.
Hatua hiyo imekuja wakati kukiwa na tuhuma za rushwa dhidi ya wabunge wa baadhi ya kamati na kusababisha baadhi kujiuzulu ujumbe wakishinikiza uchunguzi ufanyike ili waliohusika wawekwe hadharani na kuchukuliwa hatua.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliacho cha Bunge inasema Spika Ndugai amefanya mabadiliko hayo kwa kuzingatia mahitaji mapya na changamoto zilizojitokeza baada ya kuunda kamati hizo siku 59 zilizopita.
Waliong’olewa uenyekiti ni Richard Ndassa, ambaye alikuwa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji (PIC), Dk Mary Mwanjelwa (Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira), Martha Mlata (Kamati ya Nishati na Madini).
Waliovuliwa umakamu mwenyekiti ni Dk Raphael Chegeni (Kamati ya Huduma za Maendeleo ya Jamii) na Kangi Lugola (Kamati za Hesabu za Serikali).
“Mabadiliko haya yamefanywa chini ya Kanuni ya 116(3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge ambayo inatoa mamlaka ya kuteua wabunge kuunda kamati mbalimbali za Bunge,” inasema taarifa hiyo.
Kwa kuhamishwa kutoka kamati wanazoziongoza, wabunge hao wamepoteza nafasi zao za uenyekiti, wakati Mwanjelwa, ambaye alipata nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge kutokana na kuwa mmoja wa wenyeviti wa kamati hizo, amepoteza wadhifa huo wa kuwa mmoja wa wenyeviti watatu ambao humsaidia Spika kuongoza shughuli za Bunge.
“Sifahamu chochote,” alisema Dk Mwanjelwa, mmoja wa wenyeviti watatu wa Bunge, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu mabadiliko hayo.
“Ninachoweza kusema uamuzi wa Spika ndiyo wa mwisho, ila sina ninachofahamu kuhusiana na mabadiliko haya. Yaani ndiyo nimesoma kwenye mtandao muda si mrefu kabla hamjanitafuta.”
Taasisi za Serikali zinazotuhumiwa kutoa fedha kwa wajumbe wa Kamati za Bunge, ambazo zina jukumu la kuzisimamia, ni Shirika la Nyumba (NHC), Bima ya Afya (NHIF), Shirika la Umeme (Tanesco) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo alisema suala la taasisi yake kutoa rushwa kwa wabunge limewashangaza, na wanasubiri vyombo vya uchunguzi kutoa matokeo kuhusu tuhuma hizo.
“Matokeo ya uchunguzi kuhusu tuhuma hii ndiyo ambayo yanaweza kuanika bayana kama kweli tunahusika au lah. Ni jambo ambalo hata sisi limetushangaza,” alisema.
Kutokana na mabadiliko hayo, kamati ambazo viongozi wake wameondolewa zitalazimika kufanya uchaguzi wa viongozi.
Kamati zinazotakiwa kupata wenyeviti wapya ni ya Nishati na Madini, Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii ambayo itatakiwa kufanya uchaguzi wa mwenyekiti na makamu wake, wakati zitakazochagua makamu ni ya Hesabu za Serikali ya Mitaa (LAAC) na ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Waliohamishwa wazungumza
Akizungumzia suala hilo, Dk Chegeni alisema wajumbe wawili wa kamati yake, Zitto Kabwe (Kigoma Mjini) na Hussein Bashe (Nzega Mjini), wamemuandikia Spika barua za kujiondoa kwenye nafasi zao ili kupisha uchunguzi wa rushwa.
“Wajumbe wa kamati wamesikitishwa na taarifa hizi na kwa pamoja tumeamua kuchukua hatua. Tumemuandikia Spika barua ya kupisha uchunguzi ili kujiridhisha na madai yaliyobainishwa. Wajumbe wote waliohudhuria kikao cha leo wamesaini,” alisema Dk Chegeni.
Zitto aliiambia Mwananchi kuwa amemuandikia Spika barua ya kujiondoa, akitaka uchunguzi ufanyike na atakayehusika achukuliwe hatua kali.
Bashe alithibitisha kujiondoa akitaka uchunguzi ufanyike na watuhumiwa wote watajwe kwa majina ili hatua zichukuliwe.
“Utumishi wangu kwa kamati uko palepale nisingependa kuhamishwa lakini watuhumiwa wajulikane,” alisema Bashe.
Akizungumzia taarifa zilizochapishwa na gazeti moja jana, Dk Chegeni alisema: “Si kweli. Hata huyo katibu anayeelezwa kutumwa hakuwa nasi mpaka mwisho wa ziara pale Bima ya Afya. Alitoa udhuru kuwa mwanaye anaugua na akaruhusiwa kuondoka mapema tu. Leo (Jana) kamati imewauliza wajumbe na makatibu wote na wamekana kuhusika.”
Baada ya kujiridhisha na kutohusika kwa wajumbe wake, Dk Chegeni alisema kamati imepitisha maazimio matatu, ambayo ni kutaka uchunguzi ufanyike ili ofisi ya Spika ijiridhishe, watakaobainika wachukuliwe hatua za kikanuni na kisheria, na gazeti lililoandika habari hiyo lithibitishe tuhuma hizo na likishindwa liiombe msamaha kamati.
“Jana (juzi) nilitumwa na mwenyekiti wangu nihudhurie kikao Spika kilichokuwa kifanyike saa 5:00 asubuhi, lakini kiliahirishwa. Leo (jana) hajahudhuria kikao chetu na kanijulisha kuwa anahudhuria kikao hicho kikichoahirishwa jana (juzi). Sina taarifa za mahojiano na Takukuru,” alisema Lolencia Bukwimba akimzungumzia Ndassa.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi alisema hajajiuzului ujumbe wa kamati kama habari zilivyoenea, lakini yeye pamoja na wajumbe wenzake wa Kamati ya Huduma za Jamii wamemtaka Spika awaeleze kilichotokea kwa kuwa ndiye kiongozi wao.
“Kwa mfano mimi nijiuzulu nini wakati si mtuhumiwa?” alihoji.
“Nikijiuzulu, maana yake naacha kazi za kibunge.”
Alisema anashangaa habari kama hizo zinatokea wapi wakati hajasikia kama kuna mbunge yeyote aliyehojiwa dhidi ya tuhuma hizo.
Kuhusu tuhuma za rushwa, Mbilinyi alisema si rahisi kwa kitu hicho kutokea kwa kuwa wabunge hawawezi kuwatuma makatibu wa kamati kufuata fedha za rushwa.
“Kwa sababu huwa tunawaona kama wapelelezi, hivyo si rahisi mtu akamuamini kiasi cha kumtuma akamchukulie mzigo,” alisema.
Pia alisema kwa wakati huu ambao Bunge ni changa, haiwezi kuwa rahisi wakakubaliana kuchukua rushwa kwa kuwa bado wabunge hawajafahamiana vizuri.
Mbunge wa Jimbo la Bukene, Selemani Zedi alisema hajapata taarifa rasmi za kuhamishwa kutoka kamati ya PIC kwenda ya Katiba.
“Nitawajibika kwenye kamati nitakayopangwa kwa sababu spika anayo mamlaka ya kunipanga popote,”alisema.
Kuhusu vitendo vya rushwa, alivitaka vyombo husika kufanya uchunguzi ili atakayebainika kuhusika achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Mwaka 2012, wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini walituhumiwa kupokea hongo kutoka kwenye makampuni ya mafuta ili waunge mkono azimio la kushinikiza aliyekuwa katibu mkuu wa wizara husika, Eliackim Maswi ang’olewe.
Wakati huo, Spika Anne Makinda aliahidi kuwapeleka watuhumiwa kwenye Kamati ya Maadili na Haki za Bunge ili wachunguzwe na kuahidi kuwa matokeo ya ripoti hiyo angeiwasilisha bungeni.
Siku hiyo, Spika Makinda pia alitangaza kuivunja kamati ya nishati.

Imeandikwa na Tumaini Msowoya, Julius Mathias na Elizabeth Edward

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: