Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
BAADA ya benki kutangaza ongezeko la asilimia 18 kwenye huduma za miamala ya fedha,
Sasa ni zamu ya watumiaji wa simu kupata maumivu baada ya kampuni za mawasiliano hayo kuanza kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika manunuzi ya muda wa maongezi, ikiwamo kwa njia ya vocha, kabla ya mteja kuanza kupiga simu.
Mara tu baada ya serikali kufanya marekebisho ya VAT, Sura 148, yaliyotangazwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alipokuwa akisoma bajeti ya serikali bungeni kwa mwaka wa fedha 2016/17 katikati ya mwaka, benki zilitangaza ongezeko hilo ili kuhimili uendeshaji.
Na katika kile kinachoonekana kama maumivu kwa watumiaji wa simu ambao wanakadiriwa kuwa milioni 39.8 nchini, sasa wameanza kukatwa asilimia 18 ya VAT kwa kila muda wa maongezi wanaoununua kupitia vocha, kurushiwa au kupitia njia za benki za simu (mfano Airtel Money na Tigo Pesa).
Wasemaji wa kampuni za Airtel na Tigo kwa nyakati tofauti jana, walikiri kuwakata wateja wao asilimia 18 ya VAT kwa kila muda wa maongezi wanaoununua au kuhamishiana kutoka simu moja kwenda nyingine kwa maelezo kuwa hatua hiyo imetokana na "maagizo ya Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA)".
Juzi usiku, mwandishi alinunua vocha ya Sh. 1,000 ya Airtel na alikatwa Sh. 152.54 iliyoelezwa kuwa ni VAT baada ya kuiweka kwenye simu yake ya mkononi.
Hata aliponunua muda wa Sh. 915 kwenye akaunti yake ya Airtel Money, alikatwa Sh. 139.58 huku ujumbe mfupi wa maandishi ulioingia kwenye simu ukisomeka "umepokea muda wa maongezi wa Sh. 915.00. Tozo la VAT 18% Sh. 139.58."
Katika kufuatilia kwa kina makato hayo, mwandishi jana alinunua vocha ya Sh. 1,000 ya Tigo na kuiweka kwenye simu yake ya mkononi na alikatwa kiwango kile kile ambacho juzi alikatwa alipoweka kwenye simu yenye 'sim card' ya Airtel.
"Umefanikiwa kuongeza Sh. 1,000. VAT Sh. 152.54. Salio lako jipya ni ... (kiasi kilichokuwamo kwenye simu)," ulisomeka ujumbe mfupi wa maaandishi (SMS) uliongia kwenye simu ya mwandishi baada ya kukwangua vocha ya Tigo na kuweka muda wa maongezi wa Sh. 1,000 kwenye simu yake ya mkononi.
Hata hivyo, wakati wa Bunge la Bajeti lililofanyika kuanza Aprili 19-Juni 30, mwaka huu, serikali haikueleza kama kutakuwa na makato ya kodi kwenye muda wa maongezi unaonunuliwa na wateja wa simu.
Dk. Mpango alipokuwa akisoma bajeti ya serikali kwa mwaka huu wa fedha bungeni Juni 8, alisema serikali inatoza kodi ya VAT kwenye ada za huduma za kibenki zinazotozwa na benki zote nchini ili kupanua wigo wa kodi.
Waziri huyo alisema ushuru wa bidhaa unaotozwa kwenye ada ya miamala ya uhawilishaji wa fedha, hautakatwa kwenye fedha zinazotumwa au kupokewa, bali katika ada inayotozwa na benki au kampuni ya simu.
Alifafanua kuwa sheria iliyokuwapo ilikuwa inatamka kwamba ada hiyo itatozwa katika kutuma fedha tu, hivyo baadhi ya kampuni za simu na benki zilikuwa zikitumia mwanya wa sheria hiyo kupunguza wigo wa kodi kwa kutoza ada wakati wa kupokea tu.
Kwa mujibu wa TCRA, Tanzania ilikuwa imefikisha jumla ya watumiaji wa huduma ya mawasiliano ya simu milioni 39.8 kufikia Desemba mwaka jana.
Tigo ilikuwa na jumla ya wateja milioni 11.116 ikishika nafasi ya pili mbele ya Airtel waliokuwa na wateja milioni 11.048 katika nafasi ya tatu.
Vodacom walikuwa wanaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wateja wapatao milioni 12.714, sawa na asilimia 32 ya jumla ya watumiaji wote wa huduma za mawasiliano ya simu nchini.
KAULI YA AIRTEL, TIGO
Alipotafutwa na Nipashe jana kuzungumzia suala hilo, Jackson Mmbando, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Airtel, alisema makato ya VAT kwenye muda wa maongezi yanayofanyika sasa yametokana na maelezo ya serikali.
"Ukinunua vocha ya Airtel au muda wa maongezi kutoka Airtel Money, unatozwa asilimia 18 ya VAT, hii ni sahihi kabisa na hiyo ni kutokana na maelekezo ya Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kwa sisi watoa huduma ya mawasiliano kufanya hivyo na kumjulisha mteja kwa ujumbe mfupi ili awe na ufahamu wa wazi kwenye matumizi ya muda wake wa maongezi alionunua," alisema.
Mmbando alidai makato hayo si mapya kwa maelezo kuwa VAT ilikuwa ikikatwa hata hapo awali.
Naye Mkuu wa Uhusiano wa Serikali na Masuala ya Udhibiti wa Tigo, Sylivia Balwire, alisema makato yanayofanyika sasa kwenye ununuzi wa muda wa maongezi ni ya kisheria.
Alisema waliagizwa na TCRA mwishoni mwa mwaka jana kukata wateja wao kodi ya VAT kwenye muda wa maongezi wanaoununua na kuwaarifu wateja wao kuhusu makato hayo.
"Suala la makato haya ni kwa mujibu wa sheria za kodi zinazoelekeza kuwa kila mwananchi anawajibu wa kulipa kodi," alisema Balwire na kufafanua zaidi:
"Ulipaji huu wa kodi ulikuwapo toka zamani. Kwa sasa tunakata kodi na kumwonyesha mteja kuwa amekatwa kodi, jambo ambalo ni tofauti na zamani ambapo mteja alikuwa anakatwa lakini haonyeshwi makato hayo.
"Kukatwa kodi kwenye vocha ambayo mteja anaweka kabla hajaitumia ni utaratibu tu kama ilivyo kwa mteja anapoenda kununua bidhaa na kupewa risiti ya bidhaa aliyonunua.
"Na sisi sasa tunamwonyesha mteja kiwango cha matumizi na ulipaji wake wa kodi aliyokatwa. Utaratibu huu unafanyika ikiwa ni sehemu ya kufuata utaratibu wa serikali.
"Na sisi kama kampuni ya simu, tunaendesha shughuli zetu kwa mujibu wa sheria za serikali. Hali hiyo isichukuliwe kuwa Tigo ndiyo tumeanzisha, isipokuwa ni zoezi tu la kawaida, ambalo linalenga kuhakikisha kila mwananchi anawajibika kulipa kodi.
"Zoezi hili liliratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kwa kutushirikisha wadau wote wa kampuni za simu tangu mwaka jana."
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment