Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akisitisha uteuzi wa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) mapema hii leo jijini Dar es Salaam, katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Michezo Yusuph Singo na kushoto ni Msajili wa Vyama vya Michezo nchini Bw. Ibrahim Sapi Mkwawa.
Picha na Eliphace Mrawa - Maelezo
Na. Shamimu Nyaki WHUSM
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe, amesitisha uteuzi wa Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Baraza la Michezo la Taifa kuanzia leo Julai 10 2017 kufuatia Baraza hilo kushindwa kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Michezo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam leo Dkt Mwakyembe ameeleza kuwa, amelivunja Baraza hilo kwa mamlaka aliyopewa na Sheria ya BMT Na.12 ya mwaka 1967 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria Na.6 ya mwaka 1971 pamoja na kanuni zake za mwaka 1999.
Waziri Mwakyembe amechukua uamuzi huo kutokana na maagizo aliyopewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa katika hotuba yake ya kuahirirsha Bunge Mjini Dododma Julai 5 mwaka huu, ya kufanya mapitio na kulitathmini upya Baraza hilo.
“Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliniagiza nilifanyie mapitio na kulitathmini upya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ili kujiridhisha na usimamizi wake wa shughuli za michezo nchini, na kwamba ikidhihirika kwamba usimamizi wa BMT wa michezo nchini si imara basi ninaweza kulivunja Baraza lililopo na kuunda upya.” Alisema Waziri Mwakyembe.
Aidha Waziri Mwakyembe ameeleza kuwa Baraza hilo limeshindwa kutafuta njia bora za kuondoa changamoto ambazo zilikua zinahitaji utashi na dhamira ya kujituma, ikiwemo Viongozi wa michezo kushika nafasi zaidi ya moja, kushindwa kusimamia ushiriki wa wanamichezo wa Tanzania na wa nje katika michezo mbalimbali.
Pia Waziri Mwakyembe alizitaja sababu nyingine za kuvunjwa kwa BMT kuwa ni Uchaguzi wa vyama vya michezo nchini kugubikwa na ubabe na rushwa, mapromota wa mchezo wa ngumi nchini kuendesha shughuli zao bila kusajiliwa, pamoja na kanuni za vyama vya michezo kukosa uhakiki wa kubaini upungufu kuhusu masuala ya fedha.
Hata hivyo Sektretarieti ya Baraza itaendelea kufanya kazi katika kipindi hiki kwa kushirikiana kwaukaribu na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo wakati taratibu za kumpata mwenyekiti na wajumbe wapya zikiendelea kufanyika kwa mujibu wa Sheria.
No comments:
Post a Comment