Ugumba ni
hali ya kutoweza kupata ujauzito kwa kipindi cha mwaka mmoja au zaidi
kwa wenzi ambao wamekuwa wakifanya mapenzi bila kutumia njia zozote za
uzazi wa mpango. Hali hii inaweza kutokea kutokana na mwanaume au
mwanamke, ingawa baadhi ya watu wamekuwa wakidhani wanawake peke yao
ndio ambao hupata tatizo hilo.
Utasa ni Nini?
Utasa ni hali ya mwanamke kutoweza kabisa kushika ujauzito au mwanaume kutoweza kabisa kusababisha ujauzito kwa mwanamke.
Kuna Tofauti Gani Kati ya Ugumba na Utasa?
Mtu tasa
hana uwezo wa kupata mimba au kumpa mtu mimba kabisa, wakati mgumba ana
uwezo wa kuja kupata mimba iwapo tatizo likaondolewa.
Nini Husababisha Ugumba?
Kuna sababu
mbalimbali ambazo huweza kupelekea ugumba kwa mwanaume au mwanamke,
tutaenda kuona baadhi ya sababu ambazo hujitokeza mara kwa mara.
Wanaume
Tatizo la
ugumba kwa wanaume mara nyingi hutokana na kiasi kidogo cha mbegu za
kiume, mbegu za kiume zinazoshindwa kutembea, mbegu za kiume zenye umbo
lisislo la kawaida na kuziba kwa mijira ya mbegu za kiume.
Tatizo kwenye mbegu za kiume linaweza kutokana na;
- Kuvuta sigara
- Dawa kama matumizi ya bangi kwa wingi,
- Mionzi
- Unywaji wa pombe
- Kemikali kama DDT, risasi (lead)
- Kuziba kwa mirija ya kupitisha manii na shahawa; mbegu za kiume zinashindwa kupita.
Wanawake
Ugumba kwa wanawake mara nyingi hutokana na sababu kuu mbili ambazo ni;
- Kuziba kwa mijrija ya kupitisha mayai
- Ovari kushindwa kutoa mayai ya uzazi.
Mirija ya kupitisha mayai inaweza kuziba kutokana na;
- Ugonjwa wa Pelvic Inflammatory Disease (PID) ambao unatokana kuwa na magonjwa ya zinaa yasiyotibiwa kama kisonono na klamidia.
- Utoaji mimba usio salama (unsafe abortions)
- Upasuaji maeneo ya kiunoni
- Ugonjwa wa endometriosis
Ovari kushindwa kutoa mayai ya uzazi inaweza kutokana na;
- Umri mkubwa wa mwanamke, hasa miaka 35 – 40 na kuendelea.
- Uvutaji wa sigara
- Saratani ya Ovari
- Mionzi
- Ugonjwa wa Polycystic ovarian disease
Sababu nyingine za ugumba kwa mwanamke zinaweza kuwa;
- Makovu katika mji wa uzazi kutokana na kutoa mimba.
- Mabonge ya kizazi (fibroids)
- Kuziba kwa shingo ya uzazi
- Kulegea shingo ya uzazi
- Kisukari
- Matatizo ya tezi ya shingo
- Kufanya mazoezi ya kupitiliza (excessive exercising)
Tabia Hatarishi
Tabia hizi huweza kuongeza uwezekano wa mtu kupata hali ya ugumba au utasa maishani mwake;
- Kutoa mimba kiholela, hupelekea kuwa na makovu katika mji wa uzazi na kulegeza shingo ya uzazi.
- Magonjwa ya zinaa yasiyotibiwa, hupelekea mirija kujaa maji au kuziba kwa makovu baada ya maambukizi kuisha.
- Kufanya kazi kwenye mazingira yenye joto kali sana, hii huathiri zaidi wanaume. Hupelekea utengenezwaji wa mbegu ambazo ni chache au hazina nguvu za kutosha kurutubisha yai la mwanamke.
- Uvutaji sigara
Vipimo Vya Kujua Ugumba
Vipimo
mbalimbali vinapatikana ili kuwezesha kujua tatizo la ugumba linatokana
na nini. Licha ya uwezo wa vipimo hivi, sababu ya ugumba katika asilimia
10 au zaidi ya watu wenye tatizo hili inaweza isijulikane kabisa. Ni
vizuri kwa wenzi wote wawili wenye tatizo hili kuonana na daktati kwa
ajili ya ushauri na vipimo.
Kwa wanaume hufanyika;
- Kipimo cha manii (seminalysis) kuona kama manii zipo za kawaida na kwa kiwango kinachoatakiwa. Manii huchukuliwa kwa kondomu maalum wakati wa kufanya mapenzi au kwa kupiga punyeto.
- Homoni za kiume kwenye damu; kipimo hiki hupima homoni za testosterone na Follicle Stimulating Hormone(FSH) ambazo huusika katika utengenezaji wa mbegu za kiume.
Kwa wanawake kuna vipimo vingi ambavyo huweza kufanyika, vikiwemo;
- Hysterosalpingography - hutazama mirija ya uzazi (falllopian tubes) kama imeziba au la. Pia huonesha kama tumbo la uzazi lina vivimbe.
- Ultrasound - kipimo hiki huonesha kama kuna vivimbe kwenye tumbo la uzazi, pia kwenye ovari kama kuna magonjwa yanayoweza kusababisha ugumba kama polycystic ovarian syndrome.
- Homoni za kike katika damu - kipimo hiki hupima homoni za oestrogen na Follicle stimulating hormone ambazo huuusika kwenye kuandaa yai la uzazi kutoka kwenye ovari na upandikizaji kwenye mji wa uzazi.
- Endometrial biopsy - tishu za mji wa uzazi huchukuliwa kuchunguza kama yai la uzazi limetoka. Pia huweza kuonesha kama kuna saratani ya mji wa uzazi au vinyama kwenye mji wa uzazi.
Matibabu ya Ugumba
Sababu ya
ugumba inapojulikana matibabu yanaweza kufanyika na hali hii ikaisha,
ingawa wengine licha ya sababu kujulikana bado wanaweza kushindwa kupata
watoto baada ya matibabu hayo. Hivyo, matibabu ya tatizo hili
yanahitaji uvumilivu na uelewa kuwa wakati mwingine yanaweza yasiwe na
mafanikio haraka au kabisa kama tunavyotarajia. Kuna njia mbalimbali za
kutibu ugumba, hizi zote zikijumuisha kuondoa tatizo linalosababisha
mimba ishindwe kutunga au kusaidia mimba itunge.
Kuna njia za
upasuaji hasa pale ambapo kuna vivimbe kwenye tumbo au mirija kuziba,
dawa kwa ajili ya kusaidia mayai ya uzazi yatoke na teknolojia za
kusaidia kuzaa (assistive reproductive technologies). Pia
ushauri kutoka kwa mtaalamu wa afya ni sehemu muhimu ya matibabu,
ukijumuisha siku ambazo ni rahisi mwanamke kushika ujauzito.
Upasuaji.
Mirija
iliyoziba, vivimbe kwenye mji wa uzazi au kuta za uzazi kushikamana
huweza kutibiwa kwa njia za upasuaji. Matibabu haya husaidia kuongeza
uwezekano wa wenzi kupata mtoto.
Dawa.
Matatizo ya
ugumba yanayotokana na ovari kushindwa kutoa mayai ya uzazi huweza
kutibiwa kwa dawa. Dawa hizi hutumika kuziwezesha ovari kutoa mayai ya
uzazi ili yaywe tayari kurutubishwa. Mara nyingi huweza kusababisha
kutoa mayai mengi katika mzunguko mmoja na kusababisha ujauzito wa
watoto wengi (mapacha au zaidi) pale yanaporutubishwa.
Teknolojia za kusaidia kuzaa (assistive reproductive technologies).
Hizi ni njia
za kitaalamu ambazo zinatumika kusaidia wenzi kupata ujauzito kutokana
na tatizo kwa mwanaume au mwanamke. Njia hizi ni kama Artificial Insermination na In Vitro Fertilization.
- Artificial Insermination. Njia hii hutumika pale ambapo mbegu za kiume zipo kwa kiasi kidogo. Mbegu za kiume hukusanywa na kuingizwa kwenye mji wa uzazi kwa njia za kitaalamu.
- In Vitro Fertilization. Njia hii hutumika hasa pale mirija ya mwanamke imeziba kabisa. Mayai na mbegu za kiume hukusanywa kitaaalamu na kisha yai kuchavushwa. Baada ya hapo yai lililochavushwa hupandikizwa kwenye mji wa uzazi.
Kuongeza uwezekano wa kupata mtoto na mwenzi wako, inashauriwa;
- Acha kuvuta sigara.
- Punguza vinywaji vyenye caffeine.
- Kufanya mapezi siku 1 kabla ya yai kutoka (ovulation).
- Kuacha kusafisha ukeni kwa kemikali (douching).
Njia za Kuzuia Ugumba
- Pata matibabu ya magonjwa ya kisukari, tezi ya shingo(thyroid) na magonjwa ya zinaa kama unayo.
- Pata mlo kamili wenye virutubisho vya kutosha hasa mlo wenye mboga za majani na matunda kwa wingi.
- Acha kuvuta sigara
- Acha unywaji holela wa pombe
Tatizo hili
huathiri wenzi wengi kisaikolojia kwa kuleta hasira, majuto, msongo wa
mawazo na hata kusababisha mvurugano katika mahusiano yao. Katika nchi
zetu za kiafrika, wanawake wamekuwa wahanga wakubwa wa tatizo hili. Ni
vizuri wenzi washirikiane katika hili, kwa kupeana moyo na kufuatilia
matibabu kwa pamoja. matibabu yanaposhindwa kabisa kuleta mafanikio,
wenzi wanaweza kuasili mtoto/watoto kama watakuwa na utayari.
SASA SULUHISHO LAKO LIPO NDUGU USIKATE TAMAA LABDA LEO HII MAKALA HII NI MKOMBOZI KWAKO.
Chanzo: Doctor Joh
Chanzo: Doctor Joh




No comments:
Post a Comment