Mwezi mmoja baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusitisha kuchezwa kwa nyimbo 15 zisizokuwa na maadili, zikiwemo mbili za Diamond Platinumz, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Kheri James ameshutumu hatua hiyo.
Akizungumza leo Jumatatu Machi 26, 2018 na wanachama wa umoja huo, James amewataka viongozi wenye jukumu la kusimamia tasnia ya muziki kuacha kufanya kazi ya hakimu.
James ametoa kauli hiyo baada ya hivi karibuni Diamond kuhojiwa na kituo cha Redio cha Times ya jijini Dar es Salaam na kumtuhumu Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza kufungia nyimbo za wasanii zikiwamo mbili za ‘Hallelujah’ na ‘Wakawaka’ bila kuzingatia hasara na usumbufu wanaoupata wakati wakiziandaa.
“Viongozi wanaoshughulika na masuala ya sanaa na utamaduni wasiifanye kazi hii kama kazi ya uhakimu bali waifanye kama kazi ya Ualimu kwa kuwafundisha watu namna ya kufanya”- amesema James na kuongeza;
“Serikali ya CCM imeahidi ajira kwa vijana, Vijana wameamua kujiajiri kwenye sanaa. Walimu wetu ni kuwawezesha kwenye sanaa na sio kuwakatisha tamaa kwahiyo tusitumie kigezo cha sheria na taratibu kuwaangamiza watu ambao tungeweza kuwaelimisha na wakafanya vizuri zaidi.
“Leo tuna wasanii ambao wameitangaza nchi yetu vizuri na wanalipa kodi kwa kazi zao sasa leo tunakwenye kupoteza mabalozi wazuri na walipakodi kwa makosa madogo ambayo yanaweza kurekebishwa na tukaendelea kufanya vizuri. Kama tutaaendelea kuwaacha vijana wakiangamizwa kwa kitu kinaitwa kanuni na taratibu za sheria basi hakuna kijana atakayebaki hapa”
No comments:
Post a Comment