Mpenzi msomaji, ni siku nyingine
tena ambayo kwa mapenzi ya mwenyezi Mungu tumeweza kuiona na hatuna budi
kumshukuru Mungu kwa wema wake.
Napenda kuchukua nafasi hii
kukuarika wewe ndugu msomaji, ili tuweze kwenda pamoja katika kujifunza
na kujikumbusha mambo muhimu mbalimbali yahusuyo afya zetu, mambo muhimu
kabisa kuhusu dawa na matumizi yake kwa ujumla.
Katika somo letu la leo tutajifunza
au kujikumbushia mambo makuu matatu, mambo hayo ni maana halisi ya dawa,
wakati ambao mtu anahitajika kutumia dawa na pia
tutajifunza/kujikumbusha kuhusu matumizi salama ya dawa.
Tukianza na kipengele cha kwanza
ambacho ni kuhusu maana halisi ya dawa, ndugu msomaji inawezekana kabisa
neno dawa siyo mara yako ya kwanza kulisikia, na pindi ulisikiapo
tayari kuna picha inayojengeka akilini mwako kuhusu neno au kitu hiki.
Dawa ni kitu chochote ambacho asili yake yaweza kuwa ni wanyama, mimea
au chembechembe maalumu ambazo zimeandaliwa kitaalamu/kisayansi kwa
matumizi ya kuzuia magonjwa, kutibu magonjwa, kuwezesha vipimo
mbalimbali vya magonjwa kufanyika au pia kubadilisha mfumo wa utendaji
kazi katika mwili. Hiyo ndiyo maana ya dawa.
Kabla ya kuanza matumizi ya dawa, ni
vyema kufahamu ni wakati gani mtu anahitajika kutumia dawa. Katika hali
ya kawaida hakuna mtu anayependa atumie dawa. Ila katika hili huwa mtu
kimsingi analinganisha faida na hasara za kutumia au kutokutumia dawa
pindi afya yake inapokuwa siyo imara. Mfano ni faida zipi utapata endapo
utaitumia dawa?, ni hasara zipi utapata endapo utaamua kutokutumia
dawa?.
Baada ya kujiridhisha katika majibu ya baadhi ya maswali kama
hayo, ndipo inafika tamati kwamba utumie au usitumie dawa. Pamoja na
kujiridhisha katika majibu ya maswali hayo, bado kuna haja ya kufahamu
kuwa dawa itatumika tu endapo mtumiaji kulingana na hitaji lake kiafya
atatakiwa kutumia ili atatue moja ya mambo yafuatayo ikiwemo, kutumia
kwa lengo la kuzuia ugonjwa au kupunguza athari zinazoweza kusababishwa
na ugonjwa fulani, mfano hivi karibuni serikali pamoja na wataalamu wa
afya wamekuwa wakielimisha jamii kuhusu matumizi ya dawa aina ya SP
(Sulphadoxine/Pyrimethamine) ambayo matumizi yake ni kwa lengo la kuzuia
madhara yanayoweza kusababishwa na malaria kwa mama mjamzito. Katika
hili, dawa itatumika kwa lengo la kuzuia na siyo kutibu. Ndugu msomaji
mfano mwingine ni kuhusu chanjo kama vile chanjo za surua, hutolewa ili
kuzuia ugonjwa na siyo kutibu.
Wakati ambapo pia mtu anahitajika
kutumia dawa ni katika kutibu. Hii ni baada ya kufahamika kuwa mtu analo
tatizo gani kiafya ndipo uamuzi wa kutumia dawa husika unafanywa.
Huwezi kuamua kutumia dawa kutibu tatizo usilolifahamu. Inawezekana
matumizi ya dawa yakawa hayana manufaa kwako.
Pia kuna wakati daktari wako
atakupatia/kukushauri utumie dawa fulani ili kwa namna moja au nyingine
iwezekane kukufanyia kipimo fulani na hatimaye aweze kujua tatizo la
kiafya ulilonalo na kuamua njia sahihi zaidi ya kuweza kukusaidia.
Wakati mwingine mtu atahitajika
kutumia dawa ili kubadili mfumo wa utendaji kazi katika mwili wake.
Mfano dawa zinapotumika katika kumlaza mtu na kumfanyia operesheni
maarufu kwa jina la dawa za kaputi au nusu kaputi. Pia dawa zinazotumiwa
kuongeza nguvu mfano kwa wanamichezo wasiyokuwa waaminifu ili waongeze
ufanisi katika kukimbia au katika kushindana kimichezo.
Ndugu msomaji, pamoja na mtu
kuhitajika kutumia dawa ni muhimu kufahamu namna bora ya kuitumia dawa
ili dawa hiyo iweze kuwa na manufaa kwake kwa kumsaidia kiafya, lakini
pia kuitumia bila ya kuleta madhara au kupunguza madhara yanayoweza
kusababishwa na matumizi mabovu ya dawa hiyo.
Matumizi salama ya dawa yanaanzia na
kutumika kwa dawa pale TU inapohitajika. Mtu kutumia dawa wakati
haihitajiki ni kujisababishia matatizo yasiyokuwa ya lazima. Kama unalo
tatizo ni vyema kupata ushauri wa wataalamu wa afya kabla ya kuanza
matumizi ya dawa.
Jambo lingine ni usahihi wa dozi,
kama umeshauriwa kutumia kipimo fulani cha dawa basi tumia kipimo hicho.
Kinyume na hapo utakuwa aidha umetumia dozi ndogo ambayo haitakusaidia
au dozi kubwa ambayo pia itakusababishia madhara makubwa kiafya). Muda
wa kutumia dawa pia ni muhimu. Kama ni kila baada ya masaa nane basi iwe
hivyo, mfano umeandikiwa dawa aina ya Paracetamol/Panadol vidonge
vyenye uzito wa miligramu 500 utumie 2 mara 3. Hii ina maana kwamba siku
nzima ina masaa 24 na endapo dawa husika inatakiwa itumike mara tatu
inamaana kuwa masaa 24 ya siku nzima, uyagawanye mara 3 ndipo
itafahamika kuwa uitumie kila baada ya masaa mangapi. Katika mfano huu,
panadol 2 mara 3 maana yake ni kuwa umeze vidonge viwili kila baada ya
masaa nane kwani 24 ukigawanya kwa 3 jibu lake ni 8 ambayo ni kila baada
ya masaa hayo 8 ndipo umeze dawa hiyo, bila kujali ulianza kuimeza
asubuhi, mchana au jioni/usiku.
Urefu wa dozi ni kitu cha kuzingatia
katika matumizi salama ya dawa. Endapo umeandikiwa dozi ya siku saba
basi itumie dawa kwa siku saba. Kinyume na hapo utasababisha vijidudu
vya magonjwa viwe sugu katika dawa na endapo utahitajika siku nyingine
kuitumia dawa husika utakuta dawa hiyo haikusaidii tena. Kitaalamu hali
hii hujulikana kama Antimicrobial Resistance.
Katika kutumia dawa huwa inaambatana
na baadhi ya masharti. Mfano usinywe vinywaji fulani au tumia chakula
kabla ya kumeza dawa au usiihifadhi dawa fulani katika eneo lenye joto.
Hii husaidia dawa ifanye kazi kwa ufanisi na pia kukupunguzia baadhi ya
madhara yasiyokuwa ya lazima, mfano kula chakula kabla ya kumeza dawa
aina ya Aspirini (Acetyl Salicylic Acid) vidonge husaidiwa dawa
isikwangue au kuunguza tumbo ili usipate vidonda vya tumbo.
Dawa hutumika kulingana na aina ya
hitaji la mtu kiafya. Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakipeana dawa kwa
kuaminishana kuwa wanamatatizo yanayofanana. Inawezekana ni kweli lakini
siyo lazima wote kutumia dawa ya aina moja. Mfano wote mnaweza kuwa na
tatizo la kuhisi maumivu ya kichwa, mmoja wenu akawa na dawa aina ya
Diclofenac vidonge, ukimpatia mwenzako aitumie huwezi kujua ana matatizo
gani mengine ya kiafya mfano akiwa na tatizo la Presha ukimpatia naye
atumie dawa hii utakuwa hujamsaidia kwani kwa mtu mwenye presha kubwa
dawa hii haimfai. Au kupeana Aspirini vidonge kwa mtu mwenye vidonda vya
tumbo dawa hii haimfai.
Ndugu msomaji, jambo lingine ni
kuhusu aleji ya dawa kwa baadhi ya watu. Kama kuna dawa umewahi kuitumia
na ikakuletea madhara ni vyema ukamfahamisha daktari wako kabla
hajapendekeza wewe utumie dawa gani kulingana na aina ya tatizo
ulilonalo, na pia kama dawa uliyopewa imekusababishia madhara acha
kuendelea kuitumia na fika katika kituo cha kutolea huduma za afya kwa
msaada zaidi.
Endapo dawa itatumika pindi inapohitajika, na pia ikitumika katika utaratibu unaofaa, itakuwa na manufaa kwa mtumiaji.
IMEANDALIWA NA DOCTOR JOH BLOG
IMEANDALIWA NA DOCTOR JOH BLOG
No comments:
Post a Comment