Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Joseph Mkirikiti akishiriki katika zoezi la kupanda Miti
Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Joseph Mkirikiti, amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa wa Lindi kusimamia na kuhakikisha Maafisa Misitu wanaandaa mpango kazi na kuwasilisha taarifa ya matumizi ya fedha ambazo wamepokea na kuzifanyia kazi kutoka kwa Mfuko wa Misitu Tanzania( TaFF).
Mkirikiti amesema hatua hiyo itaziwezesha Halmashauri kurejeshewa fedha kwaajili ya utekelezaji wa shughuli za upandaji miti kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
” Fedha hizo zinazopaswa kurejeshwa katika Halmashauri ni zinazotoka na wafanyabiashara wa mazao ya misitu ambapo wanapaswa kulipa tozo ya asilimia 5 ya makusanyo kutoka misitu ya asili kwa ajili ya kugharamia shughuli ya upandaji miti Wilayani” amesema Mkirikiti.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa muongozo huo wa uvunaji na biashara ya mazao ya misitu, tozo ya asilimia tano ya fedha za upandaji miti inatozwa kwenye mazao ya misitu kama vile kuni, mkaa, magogo, na nguzo.
“Kuna fedha ambazo zinapaswa kurudishwa katika halmashauri zetu kwa ajili ya kuratibu shughuli hizi ila watu mnaohusika mnafanya uzembe wa kutokutekeleza majukumu yenu ,Wakurugenzi msiwafumbie macho hawa watu wanaotaka kuturudisha nyuma, Kila mtumishi wa serikali azingatie majukumu yake na hakikisheni hizo fedha kwa Halmashauri ambazo hamjazipata watu wenu wawasilishe vitu vinavyotakiwa ili zipatikane” amesema Mkirikiti.
Naye Mtendaji wa mradi Usimamizi Shirika rasimali za uvuvi Thomas Chale amesema shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), watashirikiana na viongozi kuhakikisha mazingira ya Mkoa wa Lindi na Wilaya zake yanatunzwa kama inavyopaswa.
No comments:
Post a Comment