Dawa zenye steroidi za kupaka zaweza kugawanywa katika makundi makuu
saba, kulingana na uwezo wa ufanyaji kazi wake. Na msingi mkuu wa matumizi ni
kutumia kundi lenye uwezo wa chini kadri iwezekanavyo kwa jinsi itakayomfaa
mgonjwa.
Kundi la I-Zenye uwezo wa
juu kabisa.
Kundi la II-Zenye uwezo wa
juu.
- Mometasone furoate
- Desoximetasone
Kundi la III, IV, V na VI-Zenye uwezo wa kati
- Fluticasone propionate
- Triamcinolone acetonide
- Desonide
- Fluocinolone acetonide
- Hydrocortisone
Kumekuwa na wimbi la matumizi ya dawa za kupaka zenye steroidi
miongoni mwa wanajamii bila ya kupata ushauri wa wataalamu wa ngozi.Wengi wa
watumiaji huzitumia kama vipodozi. Wahanga wakubwa ni wanawake ingawa na
wanaume pia wamekuwa wakijihusisha na matumizi mabaya ya dawa hizi. Madhara
wapatayo watu hawa wanaotumia dawa hizi zenye steroidi za kupaka kiholela, ni
wazi kwa muonekano wa ngozi zao. Pia kuna madhara mengineyo mengi ndani ya
mwili ambayo mtumiaji holela anaweza kupata, hii ni kwa sababu dawa hizi pia
zina uwezo wa kusharabiwa mwilini.
Dawa hizi za kupaka zenye steroidi huwa hazina madhara endapo mtumiaji
atatumia kama alivyoandikiwa na daktari wa ngozi, chini ya uangalizi na
ufuatiliaji wa watataalamu wa afya. Dawa hizi za kupaka kwa mfano ni kama Dermovate®,
Diprosone®,Sonaderm®,Gentrisone®,Safi®,Elyvate®,Betason®, Betacort® na
nyinginezo nyingi.
Dawa za kupaka zenye steroidi
husharabiwa mwilini na kuingia katika damu, na kiasi kinachosharabiwa hutegemea na ukubwa wa eneo la
ngozi mtu anapaka na kiasi cha dawa anachopaka kwenye ngozi. Zile zenye uwezo
wa chini husharabiwa katika maeneo mengine ya ngozi isipokuwa kiganja, lakini
zile zenye uwezo wa juu husharabiwa kwenye ngozi na pia katika kiganja. Kiasi
kikubwa cha dawa husharabiwa zaidi katika maeneo ambayo ngozi ni nyembamba,
mfano karibu na macho, sehemu za siri na sehemu za mikunjo ya ngozi.
Madhara katika ngozi yanayosababishwa na utumiaji holela wa steroidi
za kupaka yatategemea na kiasi anachopaka mtumiaji na uwezo wa steroidi
anayopaka, lakini madhara haya kwa ujumla ni kama ifuatavyo; kupungua kwa kinga
ya ngozi, ambapo itapelekea mtumiaji kupata uambukizi wa fangasi hata bakteria
katika ngozi kwa urahisi, na kwa uchache pia malengelenge na hata mkanda wa
jeshi. Husababisha matatizo kama chunusi
na ukavu wa ngozi. Ngozi kuwa nyembamba ambayo hupelekea michiri, ngozi
kuchubuka kwa urahisi, rashezi kuzunguka mdomo, kupoteza nywele na kuungua jua
kwa urahisi. Kutanuka kwa mishipa ya damu, ambayo husababisha kuonekana kwa
mishipa ya damu katika ngozi,pia wekundu katika ngozi huonekana mtumiaji
anapoacha kutumia.
Dawa hizi zaweza kuleta madhara mwilini endapo zitatumika kiholela.Kiasi
kikubwa cha dawa za kupaka zenye steroidi,mojawapo au zaidi kutoka
makundi ya steroidi, husharabiwa katika kiwango ambacho huathiri kazi
za tezi ya adrena. Tezi hii inahusika
na utengenezaji wa steroidi za asili mwilini, ambazo ni muhimu katika kuiweka
miili yetu katika afya njema . Steroidi hizi katika dawa za kupaka zinaposharabiwa na kuwepo mwilini,
mrejesho wa taarifa kutoka katika ubongo hupelekwa katika tezi ya adrena, na tezi hii huacha kutengeneza steroidi za asili.
Endapo mtumiaji ataendelea kutumia dawa hizi kwa muda mrefu, tezi hii husinyaa
kwa kuwa haifanyi kazi kwa muda mrefu. Endapo mtumiaji ataacha kwa ghafla
matumizi ya steroidi hii atakuwa mgonjwa na udhaifu wa mwili utakuwa dhahiri,na
endapo ataendeleza matumizi ndivyo atazidi kuathirika kadri siku zinavyosonga.
Madhara atakayopata mtumiaji holela endapo kiasi kikubwa kitasharabiwa ni ugonjwa
ujulikanao kama Cushing syndrome, dalili
za ungonjwa ni uso wa mviringo, kuota nundu ya mafuta kati ya mabega.Alama za
michirizi katika ngozi ambazo husababishwa na ngozi kuwa nyembamba na kutanuka,
au kutanuka kwa mishipa ya damu . Pia kukusanyika kwa maji mwilini(edema), shinikizo la juu la damu,
udhaifu wa mifupa na mara chache pia kisukari. Matibabu ya ugonjwa ni uangalizi
wa karibu na jinsi ya kumwachisha mgonjwa matumizi ya steroidi, ili kurejesha
mfumo wa asili.Matibabu huwa na mafanikio endapo mtumiaji atawahi kutibiwa.
Steroidi katika dawa hizi husharabiwa na kupita placenta. Kwa hiyo mama mjamzito awe makini na kupata ushauri wa daktari. Steroidi pia hutolewa katika maziwa ya mama anayenyonyesha. Uangalizi maalumu huhitajika endapo mama anayenyonyesha atakua anatumia dawa hizi. Kwa watoto, steroidi huathiri ukuaji wa mtoto, kwa hiyo watoto ni kundi ambalo pia huhitaji ungalizi maalumu katika matumizi haya ya dawa za steroidi za kupaka.
Kuna vipodozi vyenye steroidi ambavyo huuzwa kinyume cha sheria,
steroidi hizi katika vipodozi hivi hupatikana katika makundi ya steroidi
tuliyoyaona awali. Madhara yake ni sawa pia kama tulivyoyaona hapo awali.Kipodozi
maarufu ambacho hutumika sana na kinamama ni Caro®light (kipodozi
kilichopigwa marufuku). Chukua tahadhari endapo unaamua kubadilisha aina ya
kipodozi. Wasiliana na mfamasia au mtaalamu wa ngozi endapo una mashaka na aina
mpya ya kipodozi unachotaka kutumia.
Endapo wewe ni mtumiaji holela wa dawa za kupaka zenye steroidi,
wahi haraka hospitali au kwa daktari wa ngozi kwa ajili ya ushauri na
matibu. Wasiliana na mfamasia wako kwa ushauri juu ya matumizi bora ya
dawa za kupaka
zenye steroidi. Kamwe usichukue maamuzi mwenyewe, usishawishiwe na
rafiki au ndugu
kutumia dawa hizi zenye steroidi pasi na ushauri wa daktari wa ngozi.
Hakikisha
umeelewa maelekezo ya jinsi ya kutumia dawa kwa kuuliza maswali.
No comments:
Post a Comment