HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» » » Sethi avuliwa ukurugenzi wa IPTL akiwa mahabusu

Huku akikabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, Harbinder Sing Sethi ameondolewa katika orodha ya wakurugenzi wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL).

Uamuzi wa kumuondoa Seth katika ukurugenzi umefikiwa na bodi ya wakurugenzi ambayo pia imemvua madaraka ya kuwa mwenyekiti mtendaji wa IPTL, baada ya kushindwa kushiriki na kuhudhuria mikutano ya bodi.

Seth anadaiwa kushindwa kuhudhuria vikao vya bodi bila kuruhusiwa na wakurugenzi wenzake kwa miezi sita mfululizo tangu Juni 19, 2017 alipokamatwa na kushitakiwa. 

Hayo yamo kwenye taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa IPTL, Ambroce Lugenge wakati akitoa muhtasari wa maazimio yao wakati wa mkutano mkuu wa tatu uliofanyika Aprili 10.

Mkutano huo ulikuwa na ajenda kuu ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili kampuni hiyo na uendeshaji wa mambo yanayohusu IPTL.

Sethi anakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababisha Serikali hasara ya Dola22.198 milioni za Marekani na Sh309.5 bilioni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kusutu. 

“Bodi ilijadili kuhusu kesi namba 27 ya 2017 ya uhujumu uchumi inayomkabili ndugu Harbinder Sing Sethi na athari yake kwa kampuni, muundo wa kiutendaji wa kampuni ikiwemo na uongozi, udhibiti na ushushaji wa gharama pamoja na uwepo wa kesi mbalimbali mahakamani dhidi ya kampuni au ya kufunguliwa na kampuni,” alisema Lugenge.

Taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana ilisema bodi ilimtunuku Sethi ukurugenzi wa heshima kwa msingi kuwa “aliongoza” kampuni hiyo kutoka katika hatari ya kufilisiwa kutokana na kesi iliyokuwa imefunguliwa na kampuni ya VIP Engineering and Marketing kati ya mwaka 2002 hadi 2013.

Kutokana na uamuzi huo, Sethi hataruhusiwa kwa namna yoyote ile kushughulikia masuala yanayohusu kampuni hiyo au kuingia makubaliano yoyote kwa niaba ya kampuni. 

“Bodi imeelekeza uongozi mpya, hasa menejimenti kuwafikia wadau ikiwa ni pamoja na Serikali ili kuangalia namna bora ya kutatua madai yote dhidi ya kampuni, ikiwemo hasara inayodaiwa kusababishwa na ndugu Sethi kwa mamlaka husika, iliyopelekea kukamatwa na kushtakiwa kwake ibebwe na kampuni na kuyatafutia ufumbuzi kwa masilahi ya umma,” alisema Lugenge katika taarifa hiyo.

Pia, alisema bodi imeagiza menejimenti mpya kukaa na Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) ili kubaini kodi stahiki na kuweka mazingira bora ya kuzilipa haraka iwezekanavyo baada ya kubaini kiasi kisicho na pingamizi. 

Lugenge katika taarifa hiyo alisema bodi hiyo imemteua Joseph Makandege kuwa mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo ili kuongoza uboreshaji kiutendaji, uteuzi ulioanzia Aprili 10.

Alisema katika mkutano, bodi ilijadili na kufikia maazimio katika vipengele vingine 10 vya ajenda, ambavyo vilikuwa vinachangia kwa kiasi kikubwa kuamua mwelekeo na hatima ya kampuni hiyo.

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: