Tanzania yashukuru China, UNESCO ufadhili sekta ya elimu ya ufundi
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Tanzania imeishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na UNESCO kwa kuendelea kuunga mkono maendeleo ya elimu ya juu ya ufundi barani Afrika kwa lengo la kujenga nguvu kazi ya kiufundi na bunifu kwa maendeleo ya mataifa hayo.
Kauli imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Carolyne Nombo katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof William Anangisye akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa mradi wa kuimarisha uwezo wa taasisi za elimu ya juu katika kuendeleza ufundishaji unaozingatia soko la ajira na ujifunzaji CFIT awamu ya tatu.
Mradi huo unaotambulika kama China Fund In Trust Project Phase III (CFTI-III) unaendeshwa katika nchi sita ikiwamo Tanzania. Nchi nyingine ni Côte d’Ivoire, Ethiopia, Gabon, Senegal na Uganda.
Mradi huo ambao pia unalenga kuimarisha uhusiano kati ya vyuo vikuu na viwanda unatekelezwa kwa muda wa miaka 4 kwa bajeti ya Dola za Marekani milioni 7.5.
Nombo alisema kutokana na mradi huo vyuo vikuu vimeanza kuwa na rasilimali watu bora pamoja na miundo mbinu ya kufundishia na utafiti ili kuweza kutoa elimu stahiki ya kiufundi kwa vijana ili kufikia hitaji halisi la soko.
Alisema kupitia mradi huo mataifa yameweza kubadilika na kukabiliana na uhaba wa wanafunzi wanaochukua masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati
Pia amesema kwamba ni mtarajio yake kwamba China kupitia Unesco wataendelea kusimamia mradi huo kwa miaka mingine ili kuweza kuhakikisha kwamba mitaala inaboreka na vijana wanaotoka wanakidhi haja ya soko la ajira.
Naye Balozi wa China nchini,Chen Mingjian pamoja na kuipongeza Tanzania kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano huo mkubwa wa mwaka, alisema amefurahishwa kuona kwamba Mpango Kazi wa Ushirikiano wa China na Afrika wa Dakar (2022-2024), Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Ufadhili wa UNESCO-China umekuwa na mafanikio makubwa.
Alisema kutokana na mafanikio hayo serikali yake itaendelea kutekeleza mradi huo na utazingatia haya ya kuuendeleza kwa miaka mingine minne yaani kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2026.
"Kwa kutoa ufadhili huu, China inasaidia kukuza maendeleo ya teknolojia ya habari na kuboresha uwezo na kiwango cha mafunzo kwa taasisi za elimu na wafanyakazi katika nchi za Afrika. " alisema balozi huyo na kuongeza kuwa China iko tayari kufanya kazi na pande zote kutekeleza Mpango Kazi wa Dakar, kuimarisha ushirikiano wa elimu, na kuchangia katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi zote na kujenga jumuiya ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja katika enzi mpya.
China ni mojawapo ya vyanzo vikubwa zaidi vya ufadhili vya kiserikali vya UNESCO vinavyoorodheshwa mara kwa mara kati ya wafadhili wakuu 20 wanaotoa michango ya hiari, na mchangiaji mkubwa zaidi wa michango iliyotathminiwa kwenye bajeti ya kawaida ya UNESCO.
Madhumuni ya jumla ya CFIT III ni kuongeza uwezo wa taasisi za elimu ya juu ili kukabiliana na mahitaji ya ujuzi kwa maendeleo ya taifa kwa kuwezesha ushirikiano kati ya taasisi za elimu ya juu na sekta, kuimarisha ufundishaji unaozingatia soko la ajira, na kuimarisha ujifunzaji unaozingatia uwezo.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu , Sayansi na utamaduni (UNESCO) nchini, Michel Toto akikaribisha washiriki wa kongamano hilo la siku tatu, alitoa shukurani kwa serikali ya China kwa kutoa fedha zinazowezesha kuleta mabadiliko katika elimu barani Afrika.
Pia aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa msaada wake thabiti na kujitolea kwa Mradi wa CFIT III ili kukuza elimu ya ufundi stadi.
"Ni kupitia maono ya uongozi wa Wizara, tumeanzisha ushirikiano imara, kukusanya rasilimali kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa Mradi wa CFIT III nchini Tanzania." alisema Toto.
Alisema UNESCO wamefurahishwa na mtazamo na dhamira ya Serikali kuchagiza Maboresho ya Sekta ya Elimu yanayoendelea ambayo yatapatanisha na viwango vya kimataifa na mazoea bora.
Alisema mradi wa CFIT III unakamilisha kikamilifu mageuzi ya elimu yanayofanyika Tanzania ili kuendeleza Ajenda ya Elimu 2030.
"Kupitia mradi wa CFIT III, tunakuza ushirikiano kati ya taasisi za elimu ya juu na sekta hiyo, kukuza mbinu za ufundishaji zenye mwelekeo wa soko la ajira, na kuimarisha ujifunzaji unaozingatia uwezo. Hii huwapa wanafunzi ujuzi na maarifa yanayohitajika kwa soko la ajira na mahitaji ya jamii yanayoendelea" alisema Toto
Nchini Tanzania, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) ni wanufaika wa moja kwa moja wa Mradi wa CFIT III.
Post a Comment