Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Issa Mzenzi, ametembelea "APC Hotel and Conference Centre" iliyopo Bunju jijini Dar es Salaam, na kufanya mazungumzo na wafanyakazi wa hoteli hiyo kwa lengo la kujionea utendaji kazi pamoja na kuimarisha ufanisi wa huduma.
Katika ziara hiyo ya kikazi, Prof. Mzenzi alipata fursa ya kuzungumza na wafanyakazi wa hoteli hiyo, akiwahimiza kufanya kazi kwa weledi, nidhamu na kujituma ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wateja na wageni wanaotumia huduma za hoteli hiyo. Pia alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya hoteli hiyo ili kujionea hali halisi ya utoaji huduma na miundombinu iliyopo.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Prof. Mzenzi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi, akibainisha kuwa mafanikio ya taasisi yoyote yanategemea mshikamano na uwajibikaji wa kila mfanyakazi.
“Ni muhimu kila mmoja wetu akatimiza wajibu wake kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili ya kazi, ili kuendelea kujenga taswira nzuri ya taasisi na kuvutia wateja zaidi,” alisema Prof. Mzenzi.
Aidha, alibainisha kuwa APC Hotel and Conference Centre ni moja ya vitega uchumi muhimu vinavyochangia mapato ya taasisi, hivyo ni lazima ihudumiwe kwa kiwango cha juu kinachokidhi mahitaji ya soko la ushindani katika sekta ya ukarimu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa APC Hotel and Conference Centre, CPA Wenceslaus Mkenganyi, alimshukuru Prof. Mzenzi kwa ziara hiyo, akisema imewapa hamasa kubwa wafanyakazi na kuwahakikishia kuwa wataendelea kuongeza juhudi katika utoaji wa huduma bora kwa wateja.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za uongozi mpya wa NBAA za kutembelea na kujifunza utendaji wa taasisi na vitega uchumi vyake, pamoja na kusikiliza changamoto na maoni ya wafanyakazi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi kwa ujumla.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Issa Mzenzi akitembelea maeneo mbalimbali ya hoteli ya APC iliyopo Bunju jijini Dar es Salaam ili kujionea hali halisi ya utoaji huduma na miundombinu iliyopo.Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Issa Mzenzi akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa hoteli ya APC mara baada ya kutembelea na kujionea hali halisi ya utoaji huduma na miundombinu iliyopo.
Mkurugenzi Mtendaji wa "APC Hotel and Conference Centre", CPA Wenceslaus Mkenganyi akimkaribisha Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa Issa Mzenzi alipotembelea hotel hiyo inayomilikiwa na Bodi hiyo.




















No comments:
Post a Comment