HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » Chadema: Mhando ashitakiwe


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemtaka Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi William Mhando.


Kauli hiyo, imetolewa na Waziri Kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.

Msimamo wa Mnyika, umekuja siku moja baada ya Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, kutangaza kumfukuza kazi Mhandisi Mhando kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na mgongano wa kimaslahi.

Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), alisema hatua ya kumfukuza kazi Mhando pekee haitoshi, bali Serikali inatakiwa kurejea katika hotuba yake aliyoitoa Julai 27, mwaka huu, katika Bunge la Bajeti.

“Sasa umefika wakati kwa DPP kufanya uchunguzi wa haraka dhidi ya Mhando na wenzake ili kuweza kuwachukulia hatua za kisheria, ikiwemo kuwafikisha mahakamani.

“Julai 27, mwaka huu, nilitoa hotuba kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani na kuchukua hatua zaidi za kuwezesha Mhando na wenzake kufikishwa mahakamani, huku nikimtaka DPP kufanya hivyo haraka.

“Pamoja na kufukuzwa kwake na Bodi ya TANESCO, inapaswa kueleza hatua ilizochukua dhidi ya watendaji wengine wa TANESCO walioshirikiana naye kwa namna moja au nyingine na iwapo bodi hiyo haitachukua hatua za haraka nitaiweka hadharani.

“Taarifa ya kamati iliyoundwa na bodi kuchambua taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kueleza hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa na Rais Jakaya Kikwete dhidi ya Bodi yenyewe,” alisema Mnyika.

Alisema kwa mujibu wa kumbukumbu za Bunge, alikuwa wa kwanza kuibua bungeni tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya Mhando na wenzake.

Kutokana na tuhuma hizo, alisema Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo wakati wa majumuisho Julai 28, mwaka huu alikubaliana na hoja zake.

“Pamoja na uchunguzi wa kawaida unaoendelea, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inamtaka Mkurugenzi wa Mashitaka aamuru hatua za uchunguzi wa kijinai zichukuliwe dhidi ya Mhando kuhusu tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Alisema hatua ya kufukuzwa kazi kwa Mhando na watendaji waliohusika zisigeuzwe kuwa kafara ya kuficha uzembe na udhaifu wa Serikali.

Alisema taarifa za utendaji wa TANESCO kuhusu mpango wa dharura wa umeme pamoja na ununuzi wa mafuta, uliokuwa ukifanyika zilikuwa zikiwasilishwa kwenye vikao vya Wizara ya Nishati na Madini na vikao vya Baraza la Mawaziri.

Oktoba 29, mwaka huu Bodi ya Wakurugenzi ilitangaza rasmi kumfukuza kazi Mhandisi Mhando baada ya kumtia hatiani.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari juzi na Mwenyekiti wa Bodi, ilisema Mhando amekutwa na makosa mbalimbai yakiwamo ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma.

CHANZO: MTANZANIA

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: