HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » Wabunge Wataka Serikali Tatu



WAPENDEKEZA MAWAZIRI WASIWE WABUNGE, VITI MAALUMU VIFUTWE, URAIS MIAKA 35

WABUNGE jana walijilipua baada ya baadhi yao kupendekeza kuwa muundo wa Muungano ubadilishwe kuwa wa Serikali tatu na kwamba, mawaziri wasiwe  wabunge.
Pamoja na mapendekezo hayo, wengine walitaka umri wa kugombea urais ushushwe na kuwa miaka 35, badala ya sasa ya miaka 45.
Wakitoa maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba mjini Dodoma jana, wabunge hao pia walitaka viti maalumu vya ubunge vifutwe, badala yake wanawake warejee kugombea ubunge majimboni.
Katika mkutano huo, zaidi ya wabunge 36 walitumia nafasi hiyo kutoa maoni yao kuhusu masuala mbalimbali yenye masilahi kwa taifa, waliyoona yanafaa kuingizwa kwenye Katiba Mpya, ambayo mchakato wa ukusanyaji maoni ya uundwaji wake, unaendelea.

Muungano
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya alitaka muundo wa muungano ubadilishwe na kuwa wa Serikali tatu, badala ya uliopo sasa aliosema una kasoro nyingi.
Moja ya kasoro hiyo ni wawakilishi kuruhusiwa kuingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, huku wabunge wa Bara wakiwa hawana uwakilishi katika Baraza la Wawakilishi.
“Mwenyekiti, tuwe na Serikali tatu katika muungano, vinginevyo kila mmoja abaki na chake," alisema.
Pia alitaka viti maalumu vifutwe, badala yake wanawake wawekewe majimbo ya wilaya, ambayo watagombea na wenzao.
Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo naye alitaka muundo wa muungano uwe wa Serikali tatu pamoja na kuruhusiwa kwa mgombea binafsi katika  nafasi mbalimbali.
Alisema kuwa mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wasitokane na wabunge kwa sababu hawataweza kufanya kazi kwa ufanisi na ni mgongano wa kimasilahi.
Mbunge wa Mkanyangeni (CUF), Mohamed Mnyaa alitaka kuwapo na Serikali tatu katika muungano.
Alisema kama Tanzania Bara watakataa kuita nchi yao Tanganyika basi wanaweza kuiita jina lolote hata Mzizima.
“Muungano uwe wa Serikali tatu, Tanganyika wawe na nchi yao na sisi tuwe na Zanzibar yetu, kama bara hawataki kuiita nchi yao Tanganyika basi wanaweza kuiita hata Mzizima,”  alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Chakechake, (CUF), Mussa Haji Kombo alitaka muundo wa Muungano uliopo ubadilishwe badala yake uwe wa mkataba.
Alisema muundo uliopo hivi sasa unawanyima haki Wazanzibar, akitoa mfano wa suala la mafuta alilosema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), haina uwezo wa kufaidi raslimali yake bila ya kuwasiliana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
“Tuvunje muungano huu, tuanzishe ushirikiano mpya  wa mkataba,” alisema.
 

Mawaziri
Akitoa maoni yake, Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR- Mageuzi) Moses Machali alisema kuwa mawaziri wasiwe wabunge ili kuondoa mgongano wa kimasilahi.
Alisema kuwa ni vigumu kwa wabunge kumdhibiti waziri ambaye ni mbunge mwenzao kama ilivyo sasa.
Alipendekeza kuwa, Katiba Mpya itamke kuwa mtu akipatikana na kosa la kuhujumu nchi anyongwe pamoja na kuwapo kwa Serikali ya Majimbo, ambayo itasaidia Serikali kutoa huduma kwa wananchi.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Kessy alitaka umri wa mtu kuruhusiwa kugombea urais upunguzwe kutoka miaka 45 ya sasa hadi miaka 35.
Alisema kuwa umri huo utasaidia kupatikana rais kijana, ambaye anaweza kuhimili vishindo kwa kutembea mikoani bila ya kuchoka, badala ya kuwa na rais mzee atayekuwa akienda kutibiwa nchini India mara kwa mara.
Mbunge huyo alipendekeza pia wabunge wawe na kikomo kwa kutumikia vipindi viwili na kwamba, viongozi wastaafu wasiruhusiwe kuwapo bungeni akieleza kuwa hivi sasa wengi wanatumia muda mwingi kusinzia.
Kessy alipendekeza pia Baraza la Mawaziri lipunguzwe ukubwa akitaka wawe mawaziri 14 na manaibu mawaziri wawe 24.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, alitaka kuwapo Tume Huru ya Uchaguzi na mwenyekiti wake akiteuliwa na Rais, lakini athibitishwe na Bunge.
Pia alitaka viti maalumu vya ubunge vifutwe na badala yake wanawake waende katika majimbo kugombea sambamba na wanaume.
Msigwa alisema kuwa kuendelea kuwa na wabunge wa viti maalumu ni kuwafanya waendelee kujiona wanyonge, wakati hivi sasa kuna wanawake wenye uwezo mkubwa sawa na wanaume.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zakia Meghji alitaka muundo wa muungano uliopo ubaki kama ulivyo isipokuwa kero ndogondogo za muungano ziondolewe.
Alisema suala la uchumi wa Zanzibar linatakiwa kuangaliwa upya ili kuwafanya Wazanzibar kunufaika na raslimali zao.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alisema muundo wa muungano ubadilishwe kuwe na rais mmoja na mawaziri wakuu wawili wa kutoka Zanzibar na Bara.
Alipendekeza Rais akae madarakani kwa kipindi cha miaka saba na baada ya hapo asiruhusiwe kugombea tena.

Zitto pia alizungumzia umri wa kugombea urais akitaka uwe miaka 35 na kwamba wanaotaka umri wa miaka 45 hawana hoja.
Mbunge huyo amekuwa akikaririwa akitaka umri wa urais uwe miaka 35, akisema anaweza kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.
Kauli hiyo imekuwa ikimletea mgogoro mkubwa kati yake na viongozi wa chama chake akiwamo mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei.
Mbunge wa Tarime (CCM), Nyambari Nyangwine alitaka umri wa kugombea urais uwe miaka 35, ili kutoa nafasi kwa vijana kushika nyadhifa za juu za uongozi wa nchi.
Pia alitaka Kiswahili kiwe lugha rasmi  na kwamba mikataba yote muhimu ya uwekezaji isainiwe bungeni.
Nyangwine alitaka Katiba Mpya itamke kuwa watu wanaopatikana na makosa ya kuhujumu nchi wanyongwe.

CHANZO: MWANANCHI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: