Jaji Mark Bomani
ASEMA WANATUMIA ZAIDINGUVU KULIKO MAARIFA
KUJIRUDIA kwa matukio ya polisi kutumia silaha
za moto dhidi ya raia, kumepokewa kwa hisia tofauti, huku Mwanasheria
Mkuu wa Kwanza wa Serikali, Jaji Mark Bomani akilitaka jeshi hilo kuacha
kutumia nguvu wanapokuwa katika operesheni zao.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti kuhusu tukio
la hivi karibuni la kupigwa risasi mwandishi wa habari wa gazeti la
Tanzania Daima, watu wa kada mbalimbali walisema, kitendo cha polisi
kutumia nguvu sio busara.
Jaji Bomani kitendo cha polisi kutumia nguvu
badala ya busara katika operesheni zao kinaweza kuleta uhasama kati ya
wananchi na jeshi hilo.
“Kwa ujumla matumizi ya nguvu kwa polisi si mazuri na nadhani tunatakiwa kubadilika katika hilo.” alisema Jaji Bomani.
Bomani alieleza kuwa kwa ujumla polisi wanatumia
vibaya silaha zao ingawa bado hajapata uhakika wa jinsi tukio la
kujeruhiwa kwa Matutu lilivyokuwa .
Alisema tukio la Mwangosi lilikuwa baya zaidi
lakini picha anayoiona na kuihusisha na tukio la juzi, ni kuwa kuna
matumizi mabaya ya mashambulizi ya polisi kwa raia.
Hata hivyo wakati Jaji Bomani akieleza hayo
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji mstaafu
Amiri Ramadhan Manento alisema kila tukio linalofanywa na polisi
linatakiwa kufanyiwa uchunguzi kabla ya kuanza kulizungumzia.
Jaji Manento alisema akiwa ni mwanasheria hawezi
kutoa hitimisho ya tukio la kujeruhiwa kwa Matutu kabla ya uchunguzi wa
kisheria kufanyika.
“Tunahitaji kujua mambo mengi, ya michakato ya
makosa ya jinai, (criminal procedure) kwa mfano polisi walipoingia
walifanya nini, walipotoka, ni maneno gani walimuuliza mtu wa kwanza
waliyekutana naye.
Tunahitaji kujua iwapo walitumia kizuizi cha usalama(safe cage) katika silaha zao au la” alisema Jaji Manento
Alisema kulingana na taarifa zilizopo katika
magazeti bado unahitajika uchunguzi wa kujua ni namna gani polisi
waliingia ndani ya nyumba hiyo.
Aidha Jaji huyo mstaafu alisema hawezi kuwahukumu
polisi moja kwa moja kwani hakuna ushahidi kuwa walikuwa wakimwinda
mwandishi, bali inawezekana waligundua kuwa ni mwandishi baada ya
kumjeruhi.
Alisema hili ni tukio la tofauti na lile la kuuwa kwa Mwangosi
kwani Mwangosi alikuwa kashika vifaa vyake vya kazi lakini hapa Matutu
hakuwa na kitambulisho chochote kuwa ni Mwandishi.
“Unajua polisi wanafuata amri na sheria na wapo
kwa ajili ya kulinda raia wake, hivyo hatuwezi kusema kuwa walikuwa
wakimwinda mwandishi, kwa sababu hata polisi naye amejeruhiwa kwa panga
katika tukio hilo,” alisema Jaji Manento
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Dk Kitila
Mkumbo alisema kuwa jeshi la Polisi limekuwa halifanyi kazi zake kwa
kufuata weledi hali inayosababisha kuongezeka kwa matukio ya raia
kupigwa risasi na Taasisi ya serikali yenye dhamana ya kuimarisha
usalama wa raia hao.
“Matukio haya yanaweza kuathiri amani ya nchi kwa
sababu wananchi wakikosa imani na serikali yao wanaweza kufanya jambo
lolote bila kufuata sharia, matokeo yake amani inatoweka” alisema Dk
Mkumbo.
Dk Mkumbo aliongeza kuwa ni vema IGP Saidi Mwema
akatilia mkazo juu ya kufanya kazi kwa weledi ili kuimarisha utendaji
kazi wa jeshi la polisi na kulipa taswira mpya katika jamii.
Mkuu wa Idara ya Fedha waskuli ya Biashara chuoni
hapoDk Esther Ishengoma alisema kuwa jeshi la Polisi linadhamana ya
kulinda usalama wa raia na mali zao, litaendelea kubeba dhamana hiyo,
jambo la msingi ni kudhibiti nidhanu ya askari wanapokuwa wakitekeleza
majukumu yao.
“Ukiangalia matukio yanayotokea utaona kuna baadhi
ya askari polisi wanaolichafua jeshi kwa kufanya mambo kinyume cha
sheria, ni vema suala la nidhamu likaimarishwa ili kuongeza ufanisi,”
alisema Dk Ishengoma.
Mkazi wa Mbagala Mtongani Solomon Isaiah alisema
matendo yanayofanywa na polisi ya kujeruhi na kuua raia ndani ya
kipindi kifupi ni dalili za kutokuwepo utawala bora nchini na usimamizi
mzuri wa ngazi za juu ndani ya Polisi.
“Hawa polisi hawajitakii kufanya hivyo bali
wanatekeleza amri za viongozi wao wa ngazi za juu, hivyo basi lawama,
hatua za kisheria na mabadiliko yafanyike kwenye ngazi hizo za juu za
polisi ndipo wahamie kwa polisi wenyewe” alisema Isaiah.
Matukio ya kuua na kujeruhi raia yanayotekelezwa
na jeshi la polisi yamezidi kuongezeka siku hadi siku nchini licha ya
wadau na wananchi kupigia kelele matendo hayo hali ambayo imezidi
kugharimu maisha ya Watanzania wengi wasio na hatia kwa kuchukua sheria
mkononi.
Hivi karibuni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC) kiliazimia kuishtaki Serikali kwa Mahakama ya Kimataifa ya
masuala yaUhalifu(ICC) ili ichukue hatua zaidi juu ya mfululizo wa
matukio ya kutisha yanayofanywa na jeshi la polisi kwa Wananchi baada ya
Serikali kushindwa kuchukua hatua stahiki.
Kauli hizo imekuja siku moja baada ya polisi kulizungumzia tukio hilo kwamba lilitokea wakati wakiwa wanajihami.
CHANZO: MWANANCHI
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela akizungumzia
tukio la mwandishi huyo kupigwa risasi alisema alijeruhiwa baada ya
kuanza kumshambulia askari kwa Panga.
Hata hivyo ufafanuzi wa kamanda huyo unatofautiana
na ule wa Matutu na mashuhuda wa tukio hilo, ambao walisema kuwa polisi
walivamia nyumba ya mwandishi huyo iliyopo maeneo ya Kunduchi huku
wakimtaka mwanamke mmoja waliyemtaja kwa jina la mama J.
Katika maelezo yake Matutu alisema polisi hao
walifika nyumbani kwake wakimtaka mkewe baada ya kumfananisha na mtu
mwingine, kwamba wakati akiwa katika harakati za kumtenganisha mke
polisi hao baada ya kuhisi huenda wakawa majambazi ndipo polisi hao
wakampiga risasi ya bega.
Habari hii imeandaliwa na Florence Majani, Peter Elias na Nuzulack Dausen
Habari hii imeandaliwa na Florence Majani, Peter Elias na Nuzulack Dausen



No comments:
Post a Comment